Amedeus Willium anauliza: Naomba kuuliza faida za chaya kwenye mwili wa binadamu
Mkulima Mbunifu: Majani ya chaya ni chanzo kikubwa cha madini ya chuma, protini, kalshiamu, Vitamini A, C, foliki, asidi na Vitamini B.
Protini: Inajenga misuli. Mlo mmoja tu wa chaya ni sawa na kiwango cha protini kinachopatikana kwenye yai.
Madini ya chuma: Kwa afya ya damu na nguvu nyingi. Chaya ina kiasi kikubwa cha madini ya chuma mara mbili zaidi ya kiasi kinachopatikana kwenye spinachi.
Kalshiamu: Kwa mifupa yenye nguvu, chaya ina kiasi kikubwa cha kalshiamu kuliko mbogamboga zingine zote.
Vitamini A: Inazuia upofu, inapunguza kiwango cha maambukizi ya magonjwa ya kuhara. Vitamini C, foliki asidi na Vitamini B; Vyote hivi ni muhimu sana kwa afya.
Kwa watoto wa miezi 6 hadi miaka 2,chaya halisi ni nzuri sana kwa kupata protini na vitamini hasahasa wakati ambapo wameachishwa kunyonya maziwa ya mama. Supu ya chaya ni nzuri sana kwa watoto wa miaka 2 na kuendelea, na inaweza kutumika kama mlo ikichanganywa na vyakula vingine.
Mama anayenyonyesha ambaye anakula chaya ana maziwa mengi na bora kwa ajili ya mtoto wake.