- Kilimo, Mifugo

Kabla ya kuingia shambani kuzalisha andaa mpango biashara

Sambaza chapisho hili

Kila mara wakulima wanashauriwa kuweka kilimo katika mtazamo wa kibiashara. Wakulima wanaochukua na kuufanyia kazi ushauri huo, kisha kufanya shughuli za kilimo kitaalamu na kwa mtazamo wa kibiashara ,wanapata faida.


Kuwa na wazo ni aina gani ya kilimo unayoweza kuifanya kibiashara pekee haitoshi. Huo ni mwanzo tu. Ni lazima kukusanya au uwe na pesa/mtaji kwa ajili ya kugharamia shughuli hiyo, na mwisho utakapouza bidhaa zako au huduma utakayotoa uweze kupata pesa zaidi. Hapo ndipo wazo la biashara linatekelezeka.

Mpango wa biashara
Unapoomba mkopo, ambapo kwa kawaida mkopeshaji ni benki na taasisi nyinginezo za fedha, utaulizwa mpango wa biashara yako unayokopea fedha hizo. Hata kama haujakopa au hauna nia ya kukopa pesa, kuelewa mpanga wako wa biashara ni muhimu. Inakuwezesha kujia unafanya nini na kama unachofanya kitaleta faida au unapoteza muda wako tu!

Mpango wa biashara unatoa tafsiri ya malengo yako katika mageuzi ya kibiashara. Kwa nini unafikiri malengo hayo yatafikiwa, na nini mikakati ya kuyafikia malengo hayo?

Kwa bahati mbaya wakulima wengi hawajaelimika katika kufanya shughuli zao za kilimo kibiashara na kuwa na mpango wa biashara. Bila kuwa na mpango wa biashara ni vigumu sana kuweza kumshawishi mtu au taasisi ya fedha kuwekeza katika mradi wako.

Mpango wa biashara hubadilika kulingana na ukubwa wa biashara unayolenga, utaalam utakaotumika, na ni nani walengwa katika mradi huo.

Muhtasari wa wazo lako
Lengo ni kutoa mtazamo mzima wa biashara husika na ushirika huo, unaelezea kwa ufupi biashara husika, bidhaa au huduma zitakazojumuishwa, uchambuzi wa  soko la bidhaa/huduma hizo kwa
ufupi, mikakati ya kupata soko, na pia uchambuzi kwa ufupi ni jinsi gani fedha hizo zitasimamiwa kuahakikisha zinafanya shughuli lengwa.

Hii iwe wazi na ya kueleweka ili kutoa mtizamo mzuri wa biashara unayokusudia. Ni lazima uwe wazi kabisa kuelezea lengo la fedha unazokopa/omba. Muhtasari unaotoa ni lazima kuelezea kwa uhakika kuwa biashara yako itafanikiwa. Muda mzuri wa kuandika muhtasari ni baada ya kuandika mchanganuo wa biashara na kisha uunganishe mwanzoni mwa mpango wako wa biashara.

Wazo la biashara
Hutoa taarifa juu ya bidhaa utakazouza au huduma utakayotoa.

Mpango wa soko
Unajumuisha mambo yote unayofanya kutafuta wateja, ni nini wanachohitaji, na namna ya kuwafikia. Sehemu hii itaelezea bidhaa na huduma zako kwa undani, pia bei za bidhaa au huduma zako, na ni wapi biashara ama ofisi yako itakapokuwa na mbinu utakazotumia kusambaza bidhaa zako.

Mfumo wa biashara
Hii inaelezea mfumo wa biashara yako kisheria, mfumo uliochagua unategemeana na faida na hasara ambazo kila sharia inazo. Uchaguzi huu unaweza kuwa wa mtu binafsi, ushirika au kampuni isiyokuwa na kikomo, au ujamaa.

Katika sehemu hii, pia unatakiwa uoneshe ni kwa jinsi gani ulivyofikiria mahitaji ya kisheria na ni kwa jinsi gani umeweza kufuata katika utaratibu mzima wa kuanzisha biashara yako.

Mipango ya fedha
Unahitaji kuwa na bajeti. Sehemu hii itasaidia kuweza kupangilia faida na mtiririko mzima wa fedha katika biashara yako mpya. Hii ina maana ya fedha zinazoingia (mapato) na zinazotoka (matumizi). Ukishatengeza bajeti ni rahisi kutumia taarifa hiyo kufanya hesabu ya fedha unazohitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara yako.

Huu unaitwa mtaji, na unatakiwa kuonesha chanzo cha mtaji huo. Hii ina maana ya kuonesha ni chanzo kipikitakachochangia asilimia flani katika fedha hizo.

Angalizo

  • Kuandika mpango mzuri wa biashara hakukuhakikishii kufanikiwa lakini ni njia moja wapo ya kupunguza uwezekano wa kuanguka kibiashara.
  • Kujaribu huleta mafanikio. Anza kuandika leo na upate uzoefu utakaokuletea mafanikio.
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *