- Kilimo

Mkulima wa kilimo ikolojia na mnufaika wa jarida la Mkulima Mbunifu

Sambaza chapisho hili

David pallangyo (65) ni mkulima anayepatikana kijiji cha Embaseni, wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha. Yeye na mkewe Bi. Elieshi Ayo (60) wamejaliwa kuwa na familia ya watoto 6, kati ya hao 4 ni wa kiume na 2 ni wa kike. Mazao anayoyategemea katika shamba lake ni mahindi, kahawa na ndizi. Pia, ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa.

David alianza shughuli za kilimo mwaka wa 1992 baada ya kuacha kazi ya uafisa nyuki katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara. Sababu kuu ya kuacha kazi ni ili kumsaidia kwa karibu baba yake mzazi ambaye alikua mgonjwa sana. Kwa kuwa hakuwa na shughuli yoyote ya kumuingizia kipato, alianza kujihusisha na kilimo hususani zao la mahindi. Hii ni baada ya mkewe kupata mafunzo ya utengenezaji wa mboji katika taasisi iliyofahamika kwa jina la Sustainable Harvest.

Mwaka 2012, katika maonyesho ya kilimo, alifanikiwa kukutana na Mkulima Mbunifu katika banda lao na kuvutiwa na elimu zilizotolewa. Akaanza rasmi kulifuatilia jarida na kujifunza mambo mengi ya kilimo cha mimea pamoja na ufugaji. Kupitia jarida la Mkulima Mbunifu aliweza kubuni dawa mbalimbali za mifugo na kuhifadhia mazao ya nafaka dhidi ya wadudu waharibifu, kazi iliyompa umaarufu na kipato kikubwa kupitia mauzo ya dawa hizo za asili.

Mbali na Mkulima Mbunifu, mkulima huyu alipata mafunzo kutoka taasisi nyingine katika utengenezaji wa mboji pamoja na ukuzaji wa kahawa. Mafanikio katika kilimo Kilimo kimeweza kumpa mafanilkio mbali mbali kama vile;

  • Kipato kwa ajili ya kusomesha watoto.
  • Chakula bora na cha kutosha kwa familia yake.
  • Kuboresha na kurutubisha udongo kupitia matumizi ya mboji na matumizi ya pembejeo nyingine asili.
  • Kupata masoko mazuri ya bidhaa alizozalisha.

Gazeti la Mkulima
Mbunifu lilimfanya kutambulika zaidi, hasa baada ya kuandika kuhusu ubunifu wake wa dawa ya kuhifadhia nafaka katika toleo la 28, mwaka 2015.

  • Kujifunza mambo mengi ya kilimo na ufugaji kupitia kushiriki semina mbalimbali na mafunzo baada ya kujiingiza katika kilimo.

Changamoto katika kilimo
Katika kufanya kilimo, Bw. Pallangyo amekuwa akikutana na changamoto kubwa, ambazo ni;

  • Mabadiliko ya tabianchi ambayo hupunguza uzalishaji au kukosa kabisa mazao hasa panapokosekana mvua za kutosha au kuwepo kwa mvua za kupita kiasi, hasa kwa zao la mahindi.
  •  Wadudu waharibifu na magonjwa, mfano mdudu aitwaye= kantangaze/boko haramu ambao wamesababisha hasara kubwa kwa kipindi kirefu.

Kudhibiti tatizo la mdudu kantangaze
”Nimekua nikisumbuliwa sana na changamoto ya wadudu waharibifu kama kantangaze, anayeitwa boko haramu na wakulima, kwa kipindi cha miaka 5 sasa kwenye zao la mahindi, hali ambayo husababisha uzalishaji mdogo sana. Nimenunua dawa mbalimbali lakini kila baada ya muda mfupi wadudu wanarudi tena kutokana na mabaki ya mayai yao.

Niliamua kuwashirikisha wataalamu kutoka Mkulima Mbunifu na kunielekeza dawa ya asili iliyonitoa katika changamoto ya mdudu huyu’, anasema Bw. David Pallangayo. Na, anaendelea kueleza jinsi ya kutengeneza dawa hii ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Vifaa

  1. Jivu
  2. Mafuta ya taa
  3. Chombo/sehemu ya kuchanganya

Hatua za kuandaa

  1. Andaa chombo kipana. mfano wa beseni au unaweza kutumia turubai ndogo kwa ajili ya kuchanganya.
  2. Pima jivu kiasi cha kilo 3 hadi 5 kisha weka kwenye chombo.
  3. Pima mafuta ya taa kiasi cha robo mlita (¼).
  4. Nyunyuzia mafuta ya taa kwenye jivu huku ukiwa unayageuzageuza ili mafuta ya taa yaweze kuchanganyika vizuri na jivu.
  5. Baada ya kuchanganya, utapata jivu lenye unyevu na harufu ya mafuta ya taa likiwa bado kwenye mithili ya poda ama unga.
  6. Dawa yako itakua tayari kwa matumizi.

Matumizi
Unaweza kutumia kwa zao la mahindi, nyanya na mbaazi. Dawa hii hufukuza na kuua wadudu kantangaze ambao wanashambulia zaidi mahindi, matunda machanga ya nyanya na mbaazi.

Chukua kiasi cha gramu 100 – 150 za dawa hii na kunyunyuzia katika shina, eneo lilnaloshambuliwa. Matokeo ya dawa hii huonekana baada ya masaa 12 hadi 24 ambapo wadudu wote watakua wamekufa na wengine kuondoka kabisa kwenye zao.

Angalizo

  • Kuzidisha kiwango cha mafuta inaweza kusababisha mabaka kwenye majani ya mmea.
  • Tumia dawa hii mara baada ya kuiandaa na ni vizuri kunyunyizia mimea wakati wa jioni kwa matokeo ya haraka kwa sababu mdudu huyu hushambulia mazao zaidi wakati wa usiku.

Ushauri kwa wakulima
Wakulima waongeze ubunifu zaidi katika kuhakikisha wanazalisha chakula bora kwa njia zilizo rafiki kwa afya zao, ardhi na mazingira kwa ujumla ili kupunguza madhara ya pembejeo za sumu kwenye afya na mazingira.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *