Toka nilipoanza kupata na kusoma nakala za Mkulima Mbunifu mwaka 2011, nimepata mafanikio makubwa katika ufugaji na kilimo. Aidha, nimegundua kuwa, ukiamua na kufanya kwa vitendo kama Mkulima Mbunifu linavyosisitiza, umaskini kwa mkulima ni historia tu.
Jarida la Mkulima Mbunifu lilianza kutekeleza majukumu yake ya kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji (wakubwa na wadogo) kuanzia Julai mwaka 2011. Elimu hii inamsaidia mkulima kufaidika na kuendeleza shughuli za kilimo na ufugaji kwa gharama nafuu zaidi huku akilinda afya yake, wanyama, mimea pamoja na mazingira.
Ni dhahiri kuwa wakulima wengi wanaopata na kusoma jarida hili wanafanya kwa vitendo yale waliyoyapata na wameendelea kuhitaji elimu hii kwa kiasi kikubwa.
Ili kuthibitisha hilo, mfugaji na mkulima anayeishi kijiji cha Ngujin, kata ya Ngujin Wilayani Mwanga Bw. Richard Laurent anaeleza furaha yake juu ya yale aliyofanikiwa kufahamu na kufanya kupitia MkM.
Laurent anatanabaisha kuwa alianza kujikita katika shughuli za ufugaji kuanzia mwaka 2004 (ng’ombe mmoja na kuku 2) bila mafanikio, kwani ng’ombe huyo alidhoofika na hata ndama waliozaliwa walikufa kutokana na magonjwa. Kuku nao waliongezeka kidogo sana na hawakuwa na afya hivyo akaamua kuwauza. Akiwa amekata tamaa kabisa katika shughuli za ufugaji mwaka 2011 alikutana na jarida hili.
Mkulima Mbunifu lilimsaidia kujifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na namna ya kuboresha mifugo toka ng’ombe wa kienyeji hadi wa kisasa, tiba za asili na namna ya kutibu mifugo bila shida na kuondokana na magonjwa ambayo ndiyo hasa yalikuwa yakididimiza shughuli za ufugaji wake.
Baada ya kulisoma jarida na kuelewa vizuri mada za ufugaji, alinunua ng’ombe mwingine mmoja wa maziwa na kuku 6 kisha akaanza kufuga kulingana na muongozo alioukuwa akipata kwenye jarida hili.
Mafanikio
Alifanikiwa kuongeza mifugo hiyo hadi kufikia ng’ombe watano na kuku 300. Ng’ombe hao walikuwa wakizaa ndama na aliwauza kwa lengo la kusomesha watoto pamoja na kukuza mradi wake. Richard anasema, hadi kufikia mwaka 2013 aliweza kuongeza mbuzi, kondoo pamoja na sungura (ambao huwafuga kwa lengo la kutengeneza mbolea za bustani).
Alifakiwa kuwa na mradi mkubwa uliomfanya kufahamika na kuweza kushika nafasi ya kwanza kiwiliya kama mfugaji bora, katika wilaya ya Mwanga. Mwaka huu 2014 ameongoza wilaya yake katika maonesho ya Nane Nane na kushika nafasi ya tatu.
Kwa nini Mkulima Mbunifu
Richard anaeleza kuwa, bila MkM asingevutiwa kufanya shughuli za ufugaji kwa malengo makubwa na kuweza kufuga mifugo yake kiasi cha kuwa na afya na kumuwezesha kuingia katika ushindani. Anaeleza kuwa elimu aliyokuwa akiipata kupitia nakala za jarida hili ndizo alizotumia katika ufugaji wa mifugo yake.
Bw. Richard Laurent anapatikana kwa namba +255 753 498 643