Kilimo cha bustani kinahusika na uzalishaji wa mazao ya aina ya mboga, matunda, viungo na mimea ya mapambo. Kilimo cha bustani ni chanzo cha ajira na pato kwa wakulima na watu wengine.
Mboga na matunda vinatupatia virutubisho vya kujenga, kutia nguvu na kulinda mwili.
Unapowaangalia wakulima utagundua wengi wamejikita katika uzalishaji wa mazao ya bustani, kwa lengo la kukidhi mahitaji ya familia pekee.
Unaweza kupanua wigo kuzalisha kwa kulenga soko kubwa na kupata kipato cha kudumu. Ni muhimu kuhakikisha kunakuwapo mifumo mizuri kuanzia kwenye uzalishaji, uhifadhi, usindikaji na upatikanaji wa taarifa sahihi za masoko.
Haya yakifanyika, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa faida kubwa na kuwawezesha kukua kiuchumi.