- Kilimo Biashara, Mafuta, Usindikaji

Usindikaji wa karanga kupata mafuta

Sambaza chapisho hili

Karanga hutumika kama kiungo katika mapishi mbalimbali au kukaangwa ili kutumika kama vitafunwa lakini pia kusindikwa ili kupata mafuta, siagi na rojo.

Karanga zina virutubisho vingi kama vile; maji asilimia 7, nguvu kilokari 570, protini gramu 23, mafuta gramu 45, wanga gramu 20, kalishamu miligramu 49, chuma miligramu 3.8, patasiamu miligramu 680, vitamini B miligramu 15.5 na vitamini A (I.U 110).

Kusindika karanga kupata mafuta

Hakikisha karanga unazotaka kusindika kwa ajili ya kupata mafuta hazina ukungu wala uchafu wowote. Hii ni kwa sababu ukungu kwenye punje za karanga husababisha saratani.

Kukamua mafuta na kuengua

Vifaa

Vifaa vinavyohitajika ni pamoja na jiko, kikaango, mwiko, mashine ya kusaga, vifungashio, ungo, lakiri, lebo na sufuria.

Malighafi

Punje za karanga zilizokomaa, kukauka vizuri na ambazo hazina ukungu pamoja na maji

Hakikisha karanga za kusindika hazina uchafu na zimekauka vizuri

Jinsi ya kutengeneza mafuta

  • Kaanga karanga hadi ziwe na rangi ya kahawia nyepesi.
  • Menya na pepeta ili kutoa maganda kisha saga punje za karanga zilizomenywa kwa kutumia mashine.
  • Weka unga wa karanga kwenye sufuria, kisha ongeza kiasi kidogo cha maji safi na salama yaliyochemshwa kwenye karanga zilizosagwa.
  • Koroga kwa kutumia mwiko hadi kupata uji laini au rojo.
  • Baada ya hapo acha mchanganyiko huo kwa dakika 15 ili utulie na kisha engua mafuta kwa kuyachota.
  • Rudia kukoroga na kusubiri kwa dakika 15 na kuengu hadi mafuta yote yaishe.
  • Ukiona mafuta hayatoki wakati unakoroga na kusubiri, ni dalili kuwa mafuta yamekwisha.
  • Jaza mafuta kwenye chombo safi kilichochemshwa na chenye mfuniko.
  • Weka nembo na lakiri kisha hifadhi mahali pakavu pasipo na mwanga mkali.
  • Njia hii ina ufanisi wa asilimia 66 ya usindikaji wa mafuta.

Kukamua mafuta kwa kutumia mashine ya mkono aina ya daraja (bridge press)

Vifaa

Mashine ya kusaga, mashine ya kukamua mafuta, sufuria, kikaango, mifuko migumu ya nguo ya pamba, ungo, lebo, lakiri, bakuli kubwa, jiko na mwiko.

Malighafi

Punje za karanga zilizokomaa, kukaushwa vizuri na ambazo hazina ukungu pamoja na maji.

Jinsi ya kukamua mafuta

  • Kaanga punje za karanga hadi ziwe na rangi ya kahawia nyepesi.
  • Pukuchua na pepeta kwa kutumia ungo kutoa maganda.
  • Saga karanga kwa kutumia mashine ili kupata unga.
  • Weka unga kwenye bakuli kubwa lisilokuwa na matundu kisha weka bakuli hilo ndani ya sufuria yenye maji kiasi yanayochemka ili unga upate joto.
  • Koroga unga huo kwa kutumia mwiko kwa dakika 20.
  • Endapo unatumia mashine ya daraja, weka unga uliopata joto ya vitambaa vigumu na vyenye ukubwa wa sentimita 20 kwa 20 na ujazo wa nusu kilo.
  • Panga vifuko vyenye unga kwenye kinu cha kukamulia mafuta na kamua mafuta kwa kuzungusha muhimili.
  • Chuja kwa kutumia chujio safi kisha fungasha mafuta kwenye chupa safi zilizochemshwa.
  • Weka lebo na lakiri kisha hifadhi mahali safi na pakavu pasipo na mwanga mkali.

Kukamua mafuta kwa kutumia mashine ya mkono aina ya Ram

Mashine ya Ram huendeshwa kwa mikono na ina uwezo wa kukamua mbegu mbalimbali za mafuta.

Vifaa

Mashine ya Ram, ungo, sufuria ya kusafishia karanga, sufuria ya kukingia mafuta, vifungashio, jiko, lebo na lakiri pamoja na chujio safi.

Mahitaji

Punje za karanga safi, maji pamoja na chumvi.

Jinsi ya kukamua mafuta

  • Chagua punje za karanga zilizokomaa na kukauka vizuri.
  • Safisha kwa kupepeta na kupembua ili kuondoa vumbi, takataka, na punje zilizoharibiwa na wadudu na ukungu.
  • Osha punje kwa maji safi na salama kisha weka karanga kwenye mashine kulingana na ujazo wa mashine.
  • Weka sufuria kwenye sehemu ya mashine ili kukinga mafuta yatakayokamuliwa.
  • Kamua kwa kukandamiza mhimili wa mashine mpaka mafuta yote yawe yamekwisha.
  • Pima ujazo wa mafuta kisha ongeza maji na chumvi. Katika kila lita 10 za mafuta ongeza maji lita moja na gramu 200 za chumvi.
  • Chemsha hadi maji yote yaishe. Sauti ya kuchemka ikiisha ni dalili kuwa maji yamekwisha.
  • Ipua, acha yapoe kisha chuja kwa kitambaa au chujio safi.
  • Fungasha kwenye vyombo safi na vikavu kisha weka lebo na lakiri.
  • Hifadhi kwenye sehemu safi, kavu na yenye mwanga hafifu.

Matumizi ya mafuta ya karanga

Mafuta haya hutumika kuongeza ladha kwenye vyakula na huongeza nguvu na joto mwilini.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Usindikaji wa karanga kupata mafuta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *