[dropcap]M[/dropcap]ananasi ni matunda yanayolimwa kwa wingi katika mikoa ya Pwani, Kigoma, Morogoro, Tanga, Mwanza na Dar es Salaam.
Zao hili ambalo ni la chakula na biashara, huzalishwa kwa wastani wa tani 214,840 kwa mwaka, sawa na asilimia 17.9 ya mazao yote ya matunda.
Mambo ya kuzingatia wakati wa kuzalisha mananasi
Ubora wa mananasi hutegemea jinsi yalivyozalishwa hivyo ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo bora cha zao hili wakati wa uzalishaji ili kupata matunda yenye ubora na yanayotakiwa katika masoko na katika matumizi ya walaji.
Virutubisho vilivyopo katika tunda la nanasi
Kuna aina mbalimbali za virutubisho ambavyo hupatikana katika tunda la nanasi nazo ni; Maji asilimia 87, Nguvu kilokari 48, Sukari gramu 12, Madini ya chuma miligramu 0.4, Vitamini C miligramu 34, Vitamini B miligramu 11 na Vitamini A I.U 15.
Uhifadhi wa mananasi
Ili mananasi yasiharibike kwa haraka, ni vyema yahifadhiwe kwenye chumba chenye nyuzi joto 7 hadi 13 za sentigredi na hewa yenye unyevu wa asilimia 85 hadi 90. Katika hali hiyo mananasi yanaweza kuhifadhiwa kwa muda wa wiki mbili hadi tano bila kuharibika.
Kusindika mananasi
Nanasi huliwa kama tunda na huweza kusindikwa ili kuzuia kuharibika na hivyo kupatikana kwa bidhaa kama jamu, juisi, mananasi makavu na vipande vya mananasi visivyokaushwa.
Kusindika nanasi ili kupata juisi
Ili kupata juisi inayotokana na mananasi kuna vitu vinahitajika kama vifaa, malighafi, pamoja na hatua za kufuata katika utengenezaji.
Vifaa
- Kisu kisichoshika kutu
- Mashine ya kukamua juisi
- Meza iliyofunikwa kwa bati la aluminium
- Sufuria
- Jiko
- Chujio
- Chupa
- Kipima joto
Malighafi
- Mananasi yaliyokomaa na kuiva vizuri
- Sukari nyeupe
- Maji safi na salama
Jinsi ya kutengeneza
- Chagua mananasi bora yaliyoiva vizuri
- Osha kwa kutumia maji safi na salama
- Menya kwa kisu kikali ili kuondoa maganda
- Kata vipande vidogovidogo na viweke ndani ya mashine ya kukamua juisi
- Kamua juisi kwa kutumia mashine
- Chuja kwa kutumia chujio au kitambaa safi
- Chemsha juisi uliyoikamua kwa muda wa dakika ishirini kwenye joto la nyuzi 80 hadi 90 za sentigredi
- Epua
- Fungasha juisi ikiwa bado ya moto kwenye chupa zilizochemshwa
- Weka maji kiasi cha nusu ya kimo cha chupa na chemsha kwa muda wa dakika 20
- Epua na acha chupa zipoe
- Weka nembo
- Hifadhi sehemu yenye ubaridi
Nanasi lenye ukubwa wa kawaida linalokadiriwa kuwa na uzito wa kilo moja na nusu linaweza kutoa zaidi ya nusu lita juisi.
Matumizi
- Kiburudisho
- Kikata kiu
Virutubisho vinavyopatikana kwenye gramu 100 za juisi ya mananasi ni kama vifuatavyo:
- Maji asilimia 90
- Vitamini C miligramu 46
- Vitamini A I.U 15
- Madini ya miligramu 19
- Fosiforasi miligramu 12
- Potasiamu miligramu 98
- Nguvu kilokalori 118
- Wanga gramu 1
- Sukari gramu 10.5
Kusindika mananasi kupata jamu
Vifaa
- Sufuria
- Kisu kisichoshika kutu
- Mashine ya kukamulia juisi
- Meza iliyofunikwa kwa bati la aluminiamu
- Mwiko
- Chupa zenye mifuniko imara
- Mizani
- Lakiri na lebo
Malighafi
- Mananasi yaliyoiva vizuri
- Sukari safi nyeupe
- Malimao yaliyokomaa vizuri
Jinsi ya kutengeneza
- Chagua mananasi yaliyoiva vizuri
- Osha mananasi kwa maji safi
- Menya ili kuondoa maganda kwa kutumia kisu maalumu cha kumenyea matunda
- Kata katika vipande vidogo kwa kutumia kisu kikali
- Kamua malimau kupata juisi
- Changanya juisi ya malimau na vipande vya mananasi
- Pima uzito wa mchanganyiko huo kwa kutumia mizani
- Weka sukari katika uwiano wa kilo moja ya sukari kwa kilo moja ya mchanganyiko huo
- Koroga hadi sukari iyeyuke
- Chemsha kwa wa kadiri hadi jamu iwe tayari
Jinsi ya kutambua kama jamu imeiva
- Pima kwa kutumia kipimo maalumu (refractometer) ili kupata asilimia kati ya 68 na 72 ya sukari au pima kuona kama jamu imeiva kwa kutumia kipima joto ambacho husomeka nyuzi joto 105.5 za sentigredi
- Njia nyingine ni ya kutumia mwiko. Chota jamu kwa kutumia mwiko na ipoze haraka. Ikishapoa, imimine kwenye kisahani, ukiona inadondoka katika matone mazito ni dalili kuwa jamu imeiva
- Fungasha kwenye chupa safi
- Weka lakiri na lebo
- Hifadhi mahali safi kwenye baridi pasipo na mwanga mkali
Matumizi
Jamu hutumikwa pamona na vitafunwa mbalimbali kama vile mkate, mihogo na maandazi ili kuongeza ladha
Gramu 100 za jamu ya mananasi ina virtubisho vifuatavyo:
- Nguvu kilokari 1144
- Vitamini C miligramu 10
- Sukari gramu 65.7
- Maji asilimia 29.8
- Wanga gramu 66.7
Kusindika mananasi ili kupata vipande visivyokaushwa.
Vifaa
- Kisu kisichoshika kutu
- Meza iliyofunikwa na bati la aluminiamu
- Mizani
- Vifungashio (chupa au makopo maalumu)
Malighafi
- Mananasi yaliyoiva vizuri
- Sukari safi nyeupe
- Maji safi na salama
- Ndimu zilizokomaa vizuri
- Ndimu zilizokomaa vizuri
Jinsi ya kutengeneza
- Chagua mananasi yaliyokomaa na kuiva vizuri, yasiyoshambuliwa na magonjwa au wadudu waharibifu
- Osha matunda kwa maji safi na salama
- Menya kuondoa maganda
- Ondoa moyo wa nanasi
- Kata vipande vidogo
- Weka vipande kwenye chupa zilizochemshwa
- Tayarisha maji ya sukari kwa kuchanganya sukari na maji ya ndimu, kisha yachemshe. Kiasi cha sukari kinategemea matakwa ya mtumiaji
- Mimina mchanganyiko huo kwenye vipande vya mananasi hadi ufunike matunda
- Funga chupa kwa ,funiko safi
- Panga chupa kwenye sufuria
- Weka maji kwenye sufuria hadi kufikia nusu ya kimo cha chupa
- Chemsha chupa hizo kwa muda wa dakika 20
- Ipua na acha zipoe
- Weka lakiri na lebo kisha hifadhi mahali safi pasipo na mwanga mkali
Matumizi
Huliwa kama tunda
Virutubisho vitokanavyo na mananasi yaliyo kwenye maji ya sukari
- Nguvu kilokari 282
- Maji asilimia 83.5
- Vitamini C miligramu 34
- Vitamini A I.U 110
- Wanga gramu 15
- Sukari gramu 25
Kusindika mananasi kwa kukausha
Mahitaji
- Kaushio
- Kisu kisichoshika kutu
- Mifuko ya plastiki au chupa za kioo au plastiki zenye mifuniko imara
- Meza iliyofunikwa na bati la kukatia
Malighafi
- Mananasi yaliyokomaa na kuiva vizuri
- Maji safi na salama
- Jinsi ya kukausha
- Chagua mananasi yaliyoiva vizuri
- Osha mananasi kwa maji safi na salama
- Menya ili kuondoa maganda
- Kata katika vipande vidogo vyenye unene wa milimita tatu hadi tano.Unenen ukizidi vipande vya mananasi havitakauka vizuri na kwa wakati mmoja
- Panga vipande hivyo kwenye trei za kaushio bora
- Kausha kwa muda wa siku 3 hadi 5 kutegemea hali ya jua
- Fungasha kwenye mifuko au chupa safi
- Hifadhi katika sehemu kavu nayenye ubaridi isiyo na mwanga mkali
Jinsi ya kutambua kama vipande vya mananasi vimekauka.
- Chukua kipande cha nanasi unachodhani kimekauka na kisha kikunje
- Mananasi yaliyokauka hukunjika kwa urahisi bila kukatika na hurudia katika umbo lake la awali yakikunjuliwa
- Mananasi yaliyokauka hayatakiwi kuonyesha dalili za unyevu au kukatika yakikunjwa
Matumizi
Huliwa kama tunda
Vurutubisho vinavyopatikana katika gramu 100 za vipande vya mananasi yaliyokaushwa
- Nguvu kilokari 320
- Sukari gramu 20
- Wanga gramu 61
- Vitamini C miligramu 24
- Maji gramu 12
Kwa maelezo zaidi wasiliana na mtaalamu Bi. Lucy Mvungi kwa simu +255 755 565621
Ni nini falsafa yako ya kilimo? Tushirikishe kwa kuacha maoni yako hapa chini ama kuandika barua pepe kwa info@mkulimambunifu.org