Nchini Tanzania kilimo cha migomba kimekuwepo kwa miaka mingi. Kilimo hiki ni maarufu sana kwa sababu zao la ndizi limekuwa likitumika kama chakula kikuu kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera, Kilimanjaro na Mbeya.
Zao la migomba limekuwa muhimu, na kufuatiwa na mazao ya mahindi, mpunga, mtama, muhogo, viazi na mazao ya jamii ya kunde kama vile maharagwe.
Zao la ndizi linaweza kuwa moja kati ya mazao ya biashara iwapo litazalishwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hilo, ikiwa ni pamoja na kupanda aina bora ya migomba inayozaa ndizi zinazotambulika katika masoko ya kimataifa.
Nchini Tanzania mikoa inayoshughulika na kilimo cha migomba na kuzalisha zao la ndizi kwa wingi ni pamoja na Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Kigoma, na Pwani.
Matumizi
Kilimo cha migomba kina faida nyingi, baadhi ya faida za migomba na zao la ndizi ni: –
- Zao la chakula na la biashara.
- Kutengenezea pombe pamoja na kulisha mifugo.
- Kutengenezea mbolea (mboji)
- Matandazwa shambani (mulch), kutoa kivuli, na kutoa nyuzi.
- Kutengenezea vitu vya sanaa pamoja na kamba.
- Malighafi ya kutengeneza vyakula na vinywaji mbalimbali.
- Hutumika kutengenezea dawa.
- Majani hutumika kama miamvuli, sahani, vikombe na kata na magome yake hutumika kuezekea.
Uzalishaji
Zao la ndizi likizalishwa kwa utaalamu unaokubalika huweza kutoa mazao yenye ubora wa hali ya juu na kuongeza uzalishaji kwa eneo. Mambo yafuatayo yafaa kuzingatiwa katika uzalishaji wa zao hili.
Hali ya hewa
Kiasi cha chini cha mvua kifaacho ni 100mm kwa mwezi au 1200mm kwa mwaka. Mwinuko ni kutoka usawa wa bahari hadi mita 1800 juu ya usawa wa bahari. Zaidi ya mwinuko huo migomba haikui vizuri.
Kiasi cha joto kinachofaa ni nyuzi joto za sentigredi 25 hadi 30 chini ya nyuzi joto 16 migomba haikui vizuri. Migomba hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha, kina kirefu, usiotuamisha maji na pia usiwe na chumvi.
Aina za ndizi
Kuna aina nyigi sana za ndizi. Nchini Tanzania ndizi zinazozalishwa, zipo za aina nyingi ambazo hutofautiana kwa majina kutokana na eneo au mkoa unaozalisha.
Hata hivyo zinaweza kugawanywa katika makundi mawili. Aina ambayo huliwa kwa kuzichoma, kukaanga au kupikwa zikichanganywa na vyakula vingine kama vile nyama. Aina za ndizi hizo ni pamoja na Mzuzu, Mshale, Matoke, Bokoboko na Mkono wa Tembo.
Aina nyingine ni zile ambazo huliwa kama matunda, aina hizo ni kama vile Kisukari, Kimalindi, Mzungu na Mtwike.
Kuna aina nyingine za ndizi ambazo kwa sasa huzalishwa hapa nchini ambazo zina fahamika kwa ubora wake katika masoko ya ndizi ya kimataifa. Aina hizi ni pamoja na Williams, Grand Naine, Pazz, Jamaica, Gold Finger, Nyingine ni Uganda green, Embwailuma Giant na Chinese Cavendish.
Utayarishaji wa shamba
- Safisha sehemu inayohusika kwa kutumia zana ulizonazo.
- Ng’oa visiki vyote na mizizi yake yote
- Lima sehemu hiyo kwa kutumia jembe la mkono, rato, au trekta ili kuwezesha mizizi laini ya migomba kupenya ardhini kwa urahisi.
- Baada ya visiki na magugu yote kuondolewa na hivyo ardhi kuwa wazi, uchimbaji wa mashimo ya kupandikiza machipukizi au miche ya migomba unaweza kufanyika.
Nafasi ya kuchimba mashimo
Mashimo yatachimbwa kwa nafasi inayokusudiwa kutumika kati ya mashina ya migomba na kati ya mistari kama ifuatavyo:-
- Migomba inaweza kupandwa kwa nafasi ya umbali wa mita 2.75 kwa 2.75 kwa migomba mifupi kama Kimalindi na Kisukari.
- Umbali wa mita 3 kwa mita 3 kwa migomba ya urefu wa kati kama Jamaica na Mshale.
- Umbali wa meta 3.6 kwa meta 3.6 kwa migomba mirefu zaidi kama Uganda green.
Uchimbaji mashimo
Uchimbaji mashimo inafaa ufanywe mapema kiasi cha juma moja hadi mwezi kabla ya muda wa kupanda. Shimo lichimbwe kwa kutenganisha udongo wa juu na wa chini.
Vipimo vya shimo ni vyema vikazingatiwa. Iwapo utachimba shimo la mviringo litafaa liwe na kipenyo cha sentimeta 60 hadi 90 na kina cha sentimeta 60 hadi 90.
Iwapo utachimba shimo la mstatili au mraba litakuwa na urefu, upana na kina cha sentimeta 60 hadi 90, kutegemea kiasi cha mbolea kilichopo na kiasi cha mvua kinachonyesha sehemu hiyo.
Kuchagua machipukizi bora
Machipukizi mazuri yanayofaa kwa mbegu ni yale yenye sifa zifuatazo:
- Liwe chipukizi sime, yaani lenye majani membamba.
- Litoke kwenye mgomba (shina) wenye afya nzuri, usiokuwa na
magonjwa, minyoo ya mizizi, wala vifukuzi vya migomba.
- Litoke kwenye mgomba wenye sifa ya kuzaa mikungu mikubwa.
- Liwe na afya nzuri na lisiwe na dalili za ugonjwa, wadudu, au mayai ya vifukusi.
- Urefu uwe kati ya meta 1 na meta 2
Utunzaji wa shamba na mimea
Uwekaji wa matandazwa (mulching)
Kazi hii ni vyema ikafanywa mara baada ya kupanda kama inawezekana. Matandazo yawe ni makavu na unene wa sentimeta 15 ili kuhifadhi unyevu, kuzuia magugu na yakioza yataongeza mbolea.
Uongezaji wa mbolea
Baada kupanda ni vyema kuongeza mbolea madebe 2 kuzunguuka shina la migomba kila baada ya miaka miwili au mitatu. Mbolea hii inatakiwa kuchanganywa na udongo na kufunikwa kwa matandazo.
Umwagiliaji maji shambani
Migomba huhitaji maji mengi, hasa wakati wa kiangazi. Inafaa kumwagilia ili kutokupunguza ukubwa na wingi wa ndizi zinazotarajiwa kuvunwa kwa mwaka. Kiasi cha maji kinachotakiwa kwa wiki ni milimita 25, yaani eneo linalo zunguka shina la migomba lilowe kabisa.
Kupunguzia machipukizi
Inatakiwa kupunguza mimea ya migomba kwa kila shina na kubaki mimea mitatu tu, yaani Mgomba wenye ndizi (Mama), Mgomba mkubwa ambao bado haujazaa lakini unakaribia kuchanua (Mtoto), Mgomba mchanga uliochipua hivi karibuni ( Mjukuu)
Uondoaji wa ncha mwishoni mwa matunda
Baada ya mkungu kutoa ndizi, ua hunyauka na kubakiza ncha mwishoni mwa matunda. Ncha hizo hupaswa kuondolewa kwani husaidia kupunguza uwezekano wa kujeruhi matunda wakati wa kusafirisha jambo ambalo kupunguza ubora wa tunda.
Ahsanten kwa mafundisho yenu tunanufaika nayo sana sana lakin naomba kujua na aina za majani na nyasi kwa mifugo kwa majina yake.
Habari,
Karibu sana Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia makala zetu za Mkulima Mbunifu.
Kuhusu nyasi, zipo za aina mbalimbali sangari, fefe, boma, gombakanzu na mengine mengi. Mengine hufahamika kulingana na jamii ya eneo husika
Ahsante sana.
Karibu sana. Kama unahitaji msaada wowote wa kilimo na ufugaji, tafadhali usisite kuwasiliana nasi
Za majukumu mkulima mbunifu naomba kujua ni kipindi yapaswa kuandaa mashimo kwa mikoa ya nyanda za juu kusini na je naweza panda migomba aina 3 tofauti ndani ya shamba Moja lenye ekari Moja??
Habari,
Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma machapisho ya MkM.
Migomba huhitaji Kiasi cha chini cha mvua kifaacho ni 100mm kwa mwezi au 1200mm kwa mwaka. Mwinuko ni kutoka usawa wa bahari hadi mita 1800 juu ya usawa wa bahari. Zaidi ya mwinuko huo migomba haikui vizuri.
Kiasi cha joto kinachofaa ni nyuzi joto za sentigredi 25 hadi 30 chini ya nyuzi joto 16 migomba haikui vizuri. Migomba hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha, kina kirefu, usiotuamisha maji na pia usiwe na chumvi.
Kwa maana hiyo hakikisha hali ya hewa hii ndiyo iliyo katika eneo lako na ni vyema kupanda msimu wa mvua au kama hakuna mvua uwe na umwagiliaji.
Uchimbaji wa mashimo unafaa ufanywe mapema kiasi cha juma moja hadi mwezi kabla ya muda wa kupanda.
Pia unaweza kuotesha aina mbalimbali za migomba katika shamba moja lakini ni vyema upande katika mistari kila aina ya mgomba/ndizi
Ni mbolea gani nzuri ya kuweka kwenye mashimo yako ya migomba
Habari,
Tumia mbolea ya samadi iliyoiva vizuri au mboji ndiyo mbolea inayotakiwa kwenye migomba