“Nilikuwa naotesha ekari tatu za mahindi na maharage lakini niliishia kuvuna chini ya gunia 10 za mahindi lakini pia nikipata maharage kidogo sana”.
Hivyo ndivyo alivyoanza kueleza Bi. Edvester O. Yambazi (68), mkazi wa Sanya Juu ambaye kwasasa ameamua kufanya kilimo cha mahindi huku akiotesha zao funikizi aina ya Canavalia.
Safari ya kilimo
Bi. Yambazi anaeleza kuwa, aliteseka kwa muda mrefu kwenda shambani na kuwekeza gharama nyingi katika kilimo ikiwa ni kununua mbegu, kulipa wafanyakazi wa kuotesha, kufanya palizi lakini hatima yake aliishia kupata mavuno yasiyolipa hata gharama za kilimo licha ya kupata faida.
“Nilianza kufanya kilimo tangu mwaka 1968 mara tu nilipoolewa, lakini hatukuwahi kupata mafanikio makubwa mpaka nilipokuja kugundua kuwa kuna tatizo shambani kwangu ambalo linanihitaji kutumia zao funikizi ili kurutubisha udongo na hatimaye kupata mavuno mengi”.
Elimu ya Canavalia aliipata wapi
“Nilipokea elimu hii mara baada ya kukutana na waelimishaji kutoka ECHO kupitia kwenye mafunzo yalioandaliwa na shirika la Floresta huko Siha. Nilielimishwa kuwa ardhi yangu itakuwa imepoteza rutuba hivyo yanipasa kuirudisha kwa kuotesha zao hili ambalo ni faida kwa udongo lakini pia ni zao la kibiashara”.
Anasema kuwa, waelimishaji pia walimpa stori ya kweli kutoka kwa mwanamama anayelima canavalia huko Maili Sita, ambapo aliomba namba zake na kuanza kuwasiliana naye.
Mama huyo aliweza kumhadithia habari ya kweli na akaamua kununua kilo 20 za canavalia kutoka kwa huyo mama kwa shilingi laki mbili fedha za kitanzania, na kuja kuotesha katika shamba lake la hekari 3.
‘’Niliotesha mbegu hiyo kwa kuchanganya na mahindi, yaani miraba miwili ya mahindi na mraba mmoja wa canavalia”.
Matokeo baada ya kuotesha
Kwanza ilinipunguzia gharama za palizi kwani eneo lililooteshwa canavalia palizi yake ni mara moja tu pindi inapokuwa bado fupi lakini baada ya hapo hakuna magugu yanayoota tena, hivyo ilinisaidia kufanya palizi mara moja.
Mahindi yaliota makubwa sana kiasi kuwa watu kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakija kutazama shamba mara kwa mara na wakiuliza ni mbegu gani ya mahindi nimeotesha.
Mavuno
Bi. Yambazi anaeleza kuwa, katika msimu huo wa mwanzo wa kuotesha canavalia alifanikiwa kuvuna gunia za mahindi zaidi ya 50 jambo ambalo kwake ni faida kubwa sana kwani hakuwahi kuvuna kwa wingi kiasi hicho.
Anaongeza kuwa, alifanikiwa pia kuvuna gunia 7 za canavalia za kilo 100 kila gunia ambazo alikuwa akiuza kwa shilingi 10,000 kwa kilo japo kuna wakati huwauzia wengine kwa bei ya chini kidogo ili nao wapate mbegu za kuotesha.
Faida alizopata kwa kulima canavalia
Kwanza, husaidia kurudisha rutuba ya udongo iliyopotea na kwa haraka sana hivyo kufanya udongo kuzalisha kwa wingi zaidi na kupatikana kwa mazao yenye ubora.
Pili, unaweza kuotesha kwa kuchanganya na mahindi hivyo huwezi kuacha shamba likiwa na zao la canavalia peke yake.
Tatu, zao funikizi la canavalia ni zao la biashara kwani unapovuna utauza kwa wengine ambao nao hununua kwa ajili ya kuliotesha kwenye mashamba yao.
Nne, gharama za palizi hupungua kwani utalazimika kupalilia mara moja tu nah ii ni kutokana na kuwa zao hili huua magugu.
Tano, kadri unavyootesha mara kwa mara ndipo ambapo unaongeza zaidi rutuba ya shamba lako.
Sita, zao la canavalia unaweza ukaliacha bila kuling’oa na likaendelea kuchipua msimu unaofuata wa mwaka japo mavuno yake yatakuwa ni madogo kulinganisha na awali lakini urutubishaji wa udongo utakuwa ukiendelea.
Msimu wa kuotesha
Canavalia kwa nchi yetu ni vyema zaidi likaoteshwa katika msimu wa mwanzo wa mvua za mwaka hasa miezi ya pili katikati au mwezi wa tatu mwishoni.
Wito kwa wakulima
”Nawaomba wakulima hasa walio katika maeneo yanayotegemea mvua kwa kilimo na hata ambao ardhi zao zimechoka kutokana na kemikali kuacha kuendelea kuichosha ardhi kwa kemikali hizo na badala yake waoteshe canavalia ili kurutubisha na kuweka rutuba ya udongo sawa”, alisema.
Wito kwa Mkulima mbunifu
Bi. Yambazi anashukuru na kuomba shirika la Mkulima Mbunifu liweze kusambaza elimu hii kupitia majarida yake kwani msingi wa kilimo hai hutokana na rutuba hivyo wahakikishe wanawaelimisha wakulima kurudisha rutuba kwa kulima canavalia na si kulisha mazao sumu za viwandani ambazo ni athari kwa afya.
Bi. Advester Onai Yambazi anapatikana kwa simu namba 0712 787 446. Itaendelea toleo lijalo