Uyoga ni moja ya vyakula muhimu katika mwili wa binadamu, vinavyoupa mwili nguvu na virutubisho vya kujenga mwili.
Uyoga ni mmea uliopo katika kundi la mimea aina ya fangasi, na umetajwa na wataalamu mbalimbali kuwa na faida kwenye suala la afya kwa binadamu ikiwa ni pamoja na kuondoa seli mfu zilizoko mwilini.
Kilimo cha uyoga ni rahisi na unaweza ukavuna na kuuza moja kwa moja sokoni au kutumia nyumbani. Pia unaweza kuongezea thamani kwa kukausha na kuuza baadaye.
Uyoga unaweza kukaa mpaka miezi sita (6) bila kuharibika endapo utakaushwa vizuri, kwani utaendelea kua na virutubisho vyake.
Njia za kukausha uyoga
Uyoga unaweza kukaushwa kwa njia mbili, aidha kwa kutumia kaushio maalumu la umeme (electric drier) au kwa wazi kwa kutumia kaushio la la jua (solar drier).
Mahitaji muhimu ili kukausha uyoga
Vifaa
- Kisu kwa ajili ya kukatia uyoga
- Sufuria
- Kuni
- Kibao ambacho kitatumika kukatia uyoga
- Karatasi ya kuweka uyoga ili ukauke
Malighafi
- Uyoga
- Chumvi
- Maji
Namna ya kukausha
Andaa uyoga kwa ajili ya kukausha, kwa kuukauga maeneo yote na kuondoa uyoga ulioharibika.
- Ondoa taka zote ambazo zitakuwa kwenye uyoga.
- Tenganisha sehemu ya juu ya uyoga pamoja na shina lake ili kusaidia wepesi wa maandalizi.
- Safisha/osha vizuri ili kuondoa uchafu na udongo.
- Baada ya kuosha, kausha kwa kitambaa kikavu.
- Kata vipande vipande na weka kwenye sufuria kulingana na kiasi cha uyoga ulicho nacho, ukichanganya na maji kiasi pamoja na chumvi.
- Andaa moto kisha bandika sufuria yenye uyoga jikoni na chemsha kwa dakika chache.
- Uyoga ukishachemka toa na tandaza kwenye gunia safi kisha weka sehemu yenye jua moja kwa moja na penye hewa ya kutosha kwa zaidi ya masaa 3 mpaka ukauke.
- Uyoga ukishakauka hifadhi tayari kwa ajili ya matumizi.
Jinsi ya kuhifadhi
Ili kuzuia kuharibika kwa uyoga, inapaswa kuwekwa katika sehemu safi ya kutunzia isiyopitisha maji, unyevu, hewa na kutokuliwa na wadudu na kuweka sehemu kavu.
Mazao yaliyokaushwa yatakuwa salama kama yatahifadhiwa kwa njia ambayo yatabaki katika hali ya ukavu na bila kuingiliwa na wadudu.
Muhimu
Kumbuka kuwa, uyoga unaweza kunyonya unyevu pamoja na harufu kwa haraka, hivyo ni marufuku kuhifadhi bidhaa kavu ya uyoga karibu na chumvi, mafuta au mazao mengine ambayo huongeza unyevu wa hewa, au yale ambayo yanaweza kupeleka harufu.
Ningependa kujua hatua kwa hatua namna ya kuzalisha uyoga tangu kuandaa mashamba hadi kuvuna
Habari
Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa swali lako
Kuhusu namna ya kuzalisha uyoga, ningependa kuunganisha na mkulima mzalishaji wa uyoga Bi. Penina Mungure aliyeko Arusha kwa simu namba 0754 875 165. Huyu atakusaidia
Karibu