Majani ya malisho ya umuhimu mkubwa kwa mfugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo. Bila malisho ya kutosha mfugaji atagaramika kwa kununua nyasi hasa wakati wa kiangazi.
Kuwa na malisho ya kutosha inampa mkulima amani na hakikisho kwamba mifugo wake wanapata lishe ya kutosha nyakati zote. Ikiwa mfugaji hataweka mikakati ya kuzalisha na kuhifadhi malisho basi mifugo hawatakuwa wenye afya na uzalishaji wao utakuwa wa hali ya chini. Hivyo, ni vyema mkulima kutenga eneo la kutosha kuzalisha nyasi hasa wakati wa msimu wa mvua na kuhifadhi kwa matumizi ya baadaye.
Kupanda nyasi ni sehemu moja tu, usimamizi mzuri utahakikishia wingi na ubora wa nyasi. Endapo unafuga, malisho yanahitajika kwa kipindi chote cha mwaka. Chanzo cha malisho ni kuchunga, nyasi, majani jamii ya mikunde, pamoja na miti ya malisho ambayo unaweza kukata na kubeba.
Wakati mifugo wa kienyeji inaweza kuendana vizuri na malisho makavu, ng’ombe wa maziwa na mbuzi wa maziwa wanatakiwa kupatiwa malisho bora na kwa kiasi kinachotosha wakati wote. Inaisistizwa kuhifadhi kiasi cha kutosha cha malisho wakati wa mvua ambapo majani yanakuwa ya kutosha na yanaweza kutumika wakati wa kiangazi.
Malisho yanayolimwa
Nyasi ni chakula kikuu kwa wanyama. Ubora wa malisho unategemea yamevunwa yakiwa na umri gani. Malisho yanakuwa bora zaidi endapo yatavunwa yakiwa katika hatua za mwanzo za ukuaji kabla ya kuchanua, wakati ambao protini na virutubisho
vingine vinakuwepo kwa wingi. Utayarishaji mzuri wa shamba, mbegu bora na mbolea ya kutosha huleta wingi wa mavuno. Inapendekezwa kuweka mbolea ya samadi kila wakati unapomaliza kuvuna. Unaweza kutumia kinyesi kibichi kutoka bandani, na kiwe na kiasi kikubwa cha mkojo wa mifugo.
Mifugo wenye wanaweza kuwa chanzo cha mbolea. Sanya samadi na mabaki ya mimea ili kutengeneza mboji ya kutosha. Hakikisha unaweka mbolea hii shambani kila baada ya kuvuna au kukata nyasi. Kwa kawaida nyasi aina ya Rhodes hufanya vizuri kwani unaweza kuvuna mara kadhaa kabla ya kupanda tena.
Matete
Matete yanapotunzwa vizuri na kukatwa mara kwa mara, yanakuwa na virutubisho vizuri kwa ng’ombe wa maziwa. Utahitajika kuwa na ekari moja ya matete au kilo 25,000 za majani mabichi kwa mwaka kwa ajili ya kulisha ng’ombe anayetoa maziwa kwa wingi, mwenye uzito wa kilo 450.
Panda kwenye tumbukizi
Mbinu hii ya upandaji wa majani unasaidia kupata malisho kwa wingi zaidi, hata wakati wa kiangazi. Hii ni kwa sababu matete yanaweza kuwa katika eneo moja kwa kipindi
cha miaka 3-5. Matete pia yanaweza kupandwa kwenye kontua sehemu zenye mwinuko ili kuzuia mmomonyoko wa ardhi.
Mseto
Inashauriwa kupanda viazi vitamu au aina nyingine ya mimea jamii ya mikunde yenye virutubisho kwa wingi kama vile Desmodium au lusina, kati ya mashimo au mistari ya matete ili kuongeza virutubisho na ubora wa malisho, pamoja na kusaidia kuzuia magugu.
Kuvuna
- Matete yanakuwa tayari kuvunwa katika kipindi cha miezi 3-4 toka yalipopandwa.
- Vuna kila mmea unapokuwa na urefu wa futi 3.
- Vuna majani kwa hatua. Kata kwa kuanzia mwanzo wa mstari na ukate majani ya kutosha kulisha mifugo yako. Wakati mwingine kata mstari unaofuata. Endelea hivyo mpaka utakapofika mwisho wa mstari, kisha uanze mstari mwingine.
- Acha shina urefu wa sentimita 15, kiasi cha kiganja cha mkono, ili kuhakikisha kuwa yanachipua tena.
- Hifadhi majani yaliyozidi kama sileji au hay.
- Shina la matete linapoanza kukomaa linapoteza virutubisho hadi kufikia 0%, hivyo kupunguza uzalishaji wa maziwa.
Palizi
Fanya palizi ya mikono kila unapokata/kuvuna ili kuongeza uzalishaji.
Weka magugu uliyong’oa au kufyeka kwenye shimo.
Utunzaji wakati wa kiangazi
Kupanda kwenye mashimo inasaidia kuhifadhi maji. Kama ukimwagilia ndoo moja ya maji kwenye kila shimo mara moja au mbili kwa wiki, matete yataendelea kukua vizuri zaidi na kutoa malisho hasa wakati wa kiangazi.
Kulisha
- Changanya matete na malisho ya jamii ya mikunde pamoja na virutubisho mvingine kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa. Unapolisha, hakikisha majani ya mikunde isizidi asilimia 35% ya malisho.
- Katakata ili kupunguza upotevu wakati wa ulishaji. Pia, tengeneza chombo cha kulishia ili kupunguza uchafu unaotokana na mifugo kukanyanga au kukojoa na kutia samadi kwenye nyasi.
Malisho jamii ya mikunde na mimea vunde
- Yanaboresha malisho ya wanyama wanaocheua kwa protini na kalishamu ambayo ni muhimu kwa uzalishaji wa maziwa.
- Yanakuwa vizuri wakati wa kiangazi ambapo aina nyingine za malisho zinakuwa hadimu. Lisha 30% (isizidi 35%) kwa kila kipimo.
- Ni lazima yaachwe yanyauke kabla ya kulisha mifugo, na pia yachanganywe na chakula kingine kisichokuwa cha jamii ya mikunde ili kuepuka kuvimbiwa.
Kuna aina nyingine nyingi za malisho kama vile Luserini (Medicago Sativa), fiwi (Lablab), Desmodium, ambayo mfugaji anaweza kutumia kwa ajili ya kuboresha aina nyingine za malisho.