Ufugaji ni utunzaji na uzalishaji wa mifugo kwa madhumuni ya kilimo, ikiwa ni pamoja na chakula na bidhaa zingine kutokana na mifugo. Ikifanywa ipasavyo, ni shughuli yenye uwezo mkubwa ya kumkwamua mkulima na kumpa mapato ya kutosheleza mahitaji ya kila siku.
Wengi wa wakulima wadogo huunganisha ufugaji na kuzalisha mazao, ingawa baadhi ya wakulima huzingatia ufugaji pekee, ili kuwawezesha kupata fursa ya kufuga aina moja au mbili kwa ufasaha.
Wafugaji wanatumia rasilimali kama vile nyasi, maji na kadhalika kuwawezesha wanyama kuzalisha. Ufugaji sio tu kuangazia myama bali pia inahusisha mchakato mzima wa kuzalisha rasilimali zinazotumika katika ufugaji.
Bidhaa kutokana na ufugaji kama vile nyama ina uhitaji mkubwa katika soko kwa kuwa na manufaa mengi kiafya. Ni biashara yenye faida kubwa na inaweza pia kuwa na kazi nyingi. Kwa hivyo, ni muhimu kuangalia na kujua chaguo bora kwako ili kuweza kufanya ambayo yatakuletea faida zaidi.
Kwa mfano, hutapata faida nzuri katika hali ambayo unazingatia ufugaji wa nguruwe pekee katika eneo ambapo watu wengi wanapendelea kula kuku au mbuzi. Uelewa wa soko unalolenga unachangia pakubwa katika ufanisi wa biashara ya ufugaji.
Unapofikiria kuingia katika sekta ya ufugaji hapa Tanzania, tunakupa vidokezo vya kuzingatia unapojiandaa kufanya ufugaji wenye mafanikio. Na hapa tunatumia mtazamo wa kibiashara kwa sababu lengo kuu ni mkulima kuinua hali yake kwa kuzalisha zaidi na kuuza zaidi.
Nini Kusudi Lako?
Huwezi kufanikisha ufugaji kama hujui na huelewi lengo lako vizuri. Kujua sababu ya kufanya shughuli za ufugaji ni muhimu sana kwa sababu husaidia kujua nini unataka na jinsi gani unaweza kufikia lengo lako. Ikiwa unapanga kuingia katika ufugaji wa wanyama, wa nyama na bidhaa za maziwa, basi ng’ombe au mbuzi wanaweza kuwa chaguo bora zaidi.
Kuelewa kusudio lako husaidia kuelezea kile unachotaka. Hii ni muhimu sana katika kuanzisha ufugaji kwa sababu unachochagua ndicho kitakachoamua vifaa vinavyohitajika.
Kwa ajili ya kuendesha biashara ya uzalishaji wa maziwa, inahusisha kufuga mifugo hasa kwa ajili ya bidhaa za maziwa, na biashara ya uzalishaji wa nyama inahusisha ufugaji wa mifugo hasa kwa ajili ya matumizi ya nyama. Hivyo, huwezi kuwanunua ng’ombe wa nyama ili kuzalisha maziwa. Hapo, utapoteza au mapato yako yatakuwa ya chini mno.
Tunarudia kwamba, kuna aina nyingi za uzalishaji katika ufugaji. Kwa mfano, unaweza kuwekeza katika ng’ombe kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa na/au kutengeneza na kuuza jibini, mkulima mwingine anaweza kuwekeza kwenye kuku wa nyama au mayai, mwingine kwa nguruwe na kadhalika. Hapa Tanzania, kila mkoa una nguvu na udhaifu wake; mjasiriamali katika nyanja hii ya ufugaji anapaswa kushauriana na idara ya mifugo katika wilaya yake ili kutengeneza mkakati ambao utafanya kazi vyema katika eneo husika.
Tafuta Mahali Unazalisha wapi?
Kupata eneo kunategemea ikiwa unaingia katika biashara kubwa au ndogo; yaani, unatazamia kuwafuga wanyama wengi au wachache. Hii itasaidia kuamua eneo bora kwa biashara yako. Ingawa, unaweza kuanza na eneo dogo na wanyama wachache kisha ukapanua biashara yako kwa utaratibu, hatua kwa hatua kulingana na mapato yako na pia mtaji unaopatikana.
Sambamba na hili, ni muhimu kujua ukubwa wa ardhi unayohitaji kwa uzalishaji wa mifugo yako. Kwa mfano, utahitaji eneo dogo kuzalisha kuku wa mayai kama unanunua chakula cha kuku kutoka madukani. Lakini, kama unapanga kuzalisha malighafi kama vile mahindi, soya, na kadhalika, na kutengeneza chakula nyumbani basi lazima uongeze ukubwa wa shamba kulingana na idadi ya kuku unaowafuga. Vivyo hivyo, kiasi cha ardhi kinachotumika kwa ng’ombe ni tofauti na ile inayotumika kwa ufugaji wa sungura.
Ni muhimu pia kuwa karibu na miundo mbinu muhimu kama vile maji, barabara na umeme. Hakikisha barabara sio mbovu kiasi kwamba italeta shida kubwa kwako kusafirisha mifugo au bidhaa yako kwenda sokoni. Hata anza au fanya ulipo!
Ulishaji sahihi
Kulisha ni muhimu sana katika ufugaji wa mifugo, hivyo kama unajishughulisha na ufugaji wa kondoo, ng’ombe, mbuzi, na mwanyama wengine wanaokula nyasi, inashauriwa kupanda nyasi shambani mwako au karibu na eneo lako kwa sababu itasaidia kupunguza gharama zinazoweza kutokea katika utoaji wa chakula na virutubisho vingine.
Ulishaji unajulikana kuwa moja ya sababu muhimu kwa ufugaji wa mifugo wenye mafanikio kwa sababu wakilishwa vizuri, watazalisha inavyopaswa. Kulisha mifugo vizuri haimaanishi kulisha kupita kiasi, lakini inamaanisha kuwapa chakula kinachofaa na kinachotosheleza mahitaji.
Kulisha mifugo kunahitaji maarifa, ujuzi na uzoefu mwingi ili kuweza kulisha inavyotakiwa. Ni muhimu sana kuelewa aina mbalimbali za vyakula vinavyoweza kulishwa kwa mifugo, na kisha kujifunza jinsi vyakula mbalimbali vinavyoweza kuunganishwa pamoja ili kutengeneza mgao sawia kwa wanyama.
Ukweli ni kwamba, unaponunua mnyama mzuri kisha unashindwa kumlisha hiyo ni hasara ama kazi isiyo na faida.
Hivyo, tuwekeze katika ulishaji, hasa kuelewa ni nini tunawalisha mifugo, wanahitaji virutubisho gani kwa viwango gani, na inagharimu kiasi gani. Hapa ndio inatofautisha yule mkulima atapata faida na yule wa hasara.
Fahamu kuhusu soko
Kufikiria swala la soko mwanzoni, ni muhimu sana, kwa sababu sio tu kuelewa upatikanaji wa soko bali pia soko hili litafikiwa vipi? Kuzingatia tu kuzalisha bidhaa za ubora wa juu haitoshi, lakini ni muhimu kujua utakavyouza bidhaa zako; na wapi unaweza kuuza bidhaa.
Elewa nyakati ambazo soko huwa na bei bora zaidi ili kuendana na mzunguko wa uzalishaji. Utakuwa unatabasamu wakati wengine wananung’unika. Kumbuka, unaanza na kufikiria juu ya soko kwa sababu ndio itaamua unafuga nini na wapi.
Tenga muda
Ufugaji wa mifugo unahitaji kujitolea sana. Wanyama wengi wanahitaji kulishwa na kupewa maji kila siku. Kuchunguza mara kwa mara kiwango cha maji ni muhimu sana, pia ni lazima kama unapanga kuanzisha ufugaji. Ukaguzi wa kila siku wa mifugo wako ni mojawapo ya njia bora za kuzuia majeraha, hivyo, lazima uwe karibu.
Ukitaka kuwa na ufugaji wenye faida na mafanikio unahitaji kuwekeza muda wako ili kuwatunza mifugo ipasavyo. Ikiwa umeajiriwa ama unapanga kuondoka nyumbani kwa muda mrefu, unahitaji kupata mtu ambaye atasaidia katika kuangalia na kuwatunza wanyama wako. Lakini hii itategemea mapato yako na ufugaji wenyewe.