Ng'ombe mwenye dalili ya joto ya kusimama
- Mifugo

Uzoefu husaidia kutambua mnyama anapokuwa kwenye joto

Sambaza chapisho hili

Uzalishaji wenye faida kwa ng’ombe wa maziwa huhitaji uangalizi wa karibu, unaowezesha kutambua ni wakati gani ng’ombe ana joto, hivyo kufanya uhamilishaji kwa wakati unaotakiwa.

Ng'ombe mwenye dalili ya joto ya kusimama
Dalili muhimu ambayo mfugaji anaweza kutambua mara moja ng’ombe anapokuwa kwenye joto ni pamoja na kupanda ng’ombe wengine. Huo ni muda muafaka wa uhamilishaji. © Picha – vetstudentresearch

Kushindwa kutambua joto ni chanzo kikubwa cha urutubishaji hafifu. Mbali na Tanzania, kulingana na utafiti uliofanywa na chuo cha PennState huko Marekani, takriban nusu ya joto hushindwa kutambulika katika uzalishaji wa maziwa nchini humo.

Hata hivyo, kutokana na utafiti juu ya kiwango cha homoni kilichopo kwenye maziwa, inaonekana kuwa takribani asilimia 15 ya ng’ombe waliotakiwa kufanyiwa uhamilishaji hawakuwa katika joto sahihi. Kutokana na hali hiyo, husababisha hasara kiuchumi kutokana na kuongezeka kwa vipindi tofauti vya kuzaa pamoja na kuongezeka kwa gharama za ziada za uhamilishaji.

Ni muhimu kuweka kumbukumbu ya taarifa zote za joto kuonesha kama ng’ombe anafaa kuhimilishwa au hapana. Utambuzi wa joto husaidia kujua kama kuna matarajio ya kuwepo kwa joto linalostahili hapo baadaye. Hata hivyo, mzunguko mrefu usio wa kawaida pamoja na vipindi virefu kutoka kuzaa kwa mara ya kwanza vyaweza kufuatiliwa.

Kwa kawaida, ng’ombe huwa katika joto mara moja kila baada ya siku 17 adi 25. Ng’ombe huonyesha ishara ya kwanza ya joto ndani ya wiki 3 hadi 4 baada ya kuzaa.

Wakati muafaka wa kumshughulikia ng’ombe ni kati ya siku 45 hadi 90 baada ya kuzaa. Uhamilishaji wa aina yoyote utakaofanyika kabla ya siku 45 baada ya kuzaa hutoa mwanya finyu wa ng’ombe kushika mimba.

Dalili za mwanzo za joto

Kusimama: Ng’ombe kusimama anapopandwa na wenzake au dume ni dalili tosha kuwa yupo katika wakati muafaka na joto linalostahili kufanyiwa uhamilishaji.

Ng’ombe wanahitaji nafasi ya kutosha ili kuchangamana. Hili halitawezekana kwa ng’ombe anaefugwa ndani, na endapo ni ng’ombe mmoja tu anafugwa. Muda wa wastani wa joto la kusimama ni kati ya saa 15 hadi 18, lakini pia huweza kutofautiana kutoka saa 8 hadi 30.

Dalili zinazofuata

Dalili hizi huweza kutokea kabla, wakati au baada ya joto la kusimama. Mfugaji anatakiwa kumchunguza ng’ombe husika kwa ukaribu zaidi hasa katika kipindi cha awali cha dalili za joto.

Kupanda ng’ombe wengine: Ng’ombe anayeonesha tabia hii huweza kuwa katika joto au kukaribia joto.

Kutokwa ute: Hii ni dalili isiyofungamana moja kwa moja na joto la kusimama. Ute huzalishwa kutoka katika mfuko wa uzazi na hujilimbikiza pamoja na majimaji mengine katika uke kabla na muda mfupi baada ya kipindi cha joto kupita.

Kuvimba na wekundu katika uke: Wakati wa joto vulva huvimba, huwa na unyevu na wekundu kwa ndani. Kwa ujumla dalili hizi huonekana kabla ya joto na hubaki kwa muda mfupi baada ya joto.

Kutokutulia: Ng’ombe anapokuwa katika hali hii huwa hatulii, huhangaika, hukosa kupumzika na hata hula kidogo sana kuliko wengine.

Kunusa: Ng’ombe anapokuwa kwenye joto hunusa na kulamba uke wa ng’ombe wengine mara kwa mara.

Mambo yanayoathiri uhitaji wa ng’ombe kupandwa

Mambo mbalimbali yanayohusiana na mazingira, afya ya ng’ombe na lishe yanaweza kuathiri uhitaji wa ng’ombe kupandwa.

Banda: Mpangilio wa banda linaloruhusu ng’ombe kuingiliana au kuwa pamoja wakati wote hutoa mwanya kwa ng’ombe kupandwa na tabia ya kusimama hudhihirika kwa urahisi.

Sakafu: Tendo la kupanda hufanyika mara nyingi zaidi ikiwa ng’ombe wapo katika eneo la udongo au kwenye nyasi badala ya sakafu ya saruji. Hali ya utelezi, tope pamoja na kukosekana kwa nafasi ya kutosha huzuia kupandana.

Matatizo ya miguu: Ng’ombe mwenye matatizo au kidonda miguuni huwa na kiwango cha chini cha kupandisha kutokana na sababu kuwa  ushindwa kuonyesha ushirikiano kwani hukwepa zaidi kupata maumivu.

Joto: Ng’ombe huonyesha zaidi kuhitaji kupandwa hasa katika kipindi cha baridi kuliko kipindi cha joto.

Muda wa kupandisha: Kupandisha mara nyingi hufanyika wakati wa asubuhi au mapema wakati wa jioni. Ng’ombe akionekana kuwa kwenye joto kabla ya 12:00 asubuhi ni lazima apandishwe siku hiyo hiyo, wakati ng’ombe aliyeonekana kwenye joto baada ya mchana ni lazima kupandishwa mapema siku ya pili.

……………………………………

Umenufaika kutoka na makala hii? Tushirikishe kwa kuacha maoni yako hapa chini ama kuandika barua pepe kwa info@mkulimambunifu.org

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

4 maoni juu ya “Uzoefu husaidia kutambua mnyama anapokuwa kwenye joto

  1. Ng’ombe wangu alipanda vizuri ,lakini baada ya siku 21alianza kulia akiwa hatulii kabisa ,Nlimpeleka Kwa ndume ndume Wala hakupanda alimunusa tu kwenye uke na kuondoka ,,Kuna uwekano kua ana mimba au?

    1. Habari, Karibu Mkulima Mbunifu.Tunakushauri upime mimba mara baada ya miezi miwili au mitatu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *