Vitoto vya mbuzi na kondoo wanahitaji uangalizi mzuri kwa sababu wao ni mbuzi na kondoo wa kesho. Utunzi mzuri unawafanya kuwa wenye nguvu na afya. Utunzaji wa mbuzi huanza mara tu baada ya kuzaliwa. Mfugaji ahakikishe yafuatayo;
- Kitoto cha mbuzi/kondoo kinapata maziwa ya mwanzo (dang’a) ndani ya masaa 24 tangu kuzaliwa na kwa muda wa siku 3.
- Kama kinanyweshwa maziwa, kipewe lita 0.7- 0.9 kwa siku. Maziwa haya, ni muhimu kwani yana viinilishe na kinga dhidi ya magonjwa.
- Iwapo mama hatoi maziwa au amekufa, inashauriwa kutengeneza dang’a mbadala au kama kuna mbuzi / kondoo mwingine aliyezaa anaweza kusaidia kukinyonyesha kitoto hicho.
- Kitoto cha mbuzi/kondoo kiendelee kunyonya kwa wiki 12 – 16. Wiki 2 baada ya kuzaliwa, pamoja na maziwa, kianze kupewa vyakula vingine kama nyasi laini na chakula cha ziada ili kusaidia kukua kwa tumbo. Aidha, kipewe maji wakati wote.
- Vyombo vinavyotumika kulishia vinakuwa safi muda wote.
- Kitoto cha mbuzi/kondoo kiachishwe kunyonya kikiwa na umri wa miezi 3 hadi 4 kutegemea afya yake.
- Vitoto vipatiwe kinga na tiba ya magonjwa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
Matunzo mengine
Mbuzi huwekewa alama ili atambulike kwa urahisi na kuwezesha utunzaji wa kumbukumbu zake. Shughuli hii hufanyika kwa mbuzi/kondoo akiwa na umri wa siku 3 – 14.
Njia zitumikazo ni pamoja na:
- Kuweka alama sikioni kwa kukata sehemu ndogo ya sikio.
- Kumpa jina kwa wafugaji wenye mbuzi wachache.
- Kumvisha hereni ya chuma au plastiki yenye namba kwenye sikio.
- Kumvalisha mkanda wenye namba shingoni.
- Kuweka namba kwa kuunguza sehemu ya ngozi ya mbuzi. Pale mfugajianapotumia njia hii inashauriwa aweke alama kwenye eneo ambalo halitaathiri ubora wa ngozi.
Kuondoa vishina vya pembe
Mbuzi/kondoo aondolewe vishina vya pembe akiwa na umri kati ya siku 3 hadi 14.
Visipoondelewa hukua na kusababisha kuumizana na kuhitaji nafasi kubwa kwenye banda. Kazi hii ifanywe na mtaalamu wa mifugo.
Kuhasi
Vitoto vya mbuzi/kondoo ambavyo havitatumika kwa ajili ya kuendeleza kizazi vihasiwe kabla ya kufikia umri wa miezi 3. Kazi hii ifanywe na mtaalamu wa mifugo.
Utunzaji wa mbuzi/kondoo wa miezi 4 – 8
Mbuzi wa miezi 4 mpaka 8 ni wale ambao wameacha kunyonya mpaka umri wa kupandishwa kwa mara ya kwanza. Mbuzi wa umri huu wana uwezo wa kula aina mbalimbali za malisho kama nyasi, mikunde, miti ya malisho na mabaki ya mazao wakati kondoo hupendelea zaidi nyasi fupi.
Wakati wa kiangazi huhitaji kupatiwa chakula cha ziada au kupewa pumba za nafaka mbalimbali, mashudu ya alizeti, pamba na dengu, majani ya mikunde yaliyokaushwa, madini na vitamini.
Katika ufugaji huria ni vyema kuzingatia idadi ya mbuzi/kondoo inayoweza kuchungwa katika eneo, aina na hali ya malisho.
Ili mbuzi/kondoo aweze kukua na kufikia uzito wa kuchinjwa/kupevuka mapema, mfugaji anapaswa kufuata kanuni za ufugaji bora zifuatazo:-
- Kumpatia vyakula vya ziada kwa muda wa miezi 2 mfululizo kiasi cha kilo 0.2 – 0.7 kwa siku kuanzia anapoachishwa kunyonya.
- Kumpatia dawa ya kuzuia minyoo kila baada ya miezi 3 na kutoa kinga za magonjwa mengine kama itakavyoshauriwa na mtaalamu wa mifugo.
- Kuchanja na kuogesha ili kuzuia magonjwa mbalimbali.
- Kukata kwato mara zinapokuwa ndefu na kuhasi madume yasiyotumika kuzalisha.
Umri wa kupandisha mbuzi / kondoo
Mbuzi/kondoo wakitunzwa vizuri wanaweza kupandishwa wakiwa na umri wa miezi 8 hadi 12 kwa mbuzi/ kondoo walioboreshwa na miezi 18 hadi 24 kwa mbuzi wa asili kutegemea afya yake. Hata hivyo, inashauriwa wapandishwe wanapofikia uzito wa kilo 12 au zaidi na wasipandishwe mbuzi/kondoo wa ukoo mmoja.
Dalili za joto
Mfugaji anashauriwa asimpandishe jike kabla hajafikisha umri wa kupandwa wa miezi 8 hadi 12 kwa mbuzi/kondoo walioboreshwa na miezi 18 hadi 24 kwa mbuzi wa asili hata kama ataonyesha dalili ya kuhitaji dume. Mbuzi au kondoo aliyezaa anaweza kupandishwa ya siku 30 hadi 60 baada ya kuzaa.
Mbuzi/kondoo aliyeko kwenye joto huonyesha dalili zifuatazo:-
- Hutingisha/huchezesha mkia na hupanda na kukubali kupandwa na wengine.
- Hutoa ute mweupe ukeni na huhangaika mara kwa mara na kupiga kelele.
- Hufuata madume, hamu ya kula hupungua na hukojoa mara kwa mara.
- Uke huvimba na huwa mwekundu kuliko ilivyo kawaida na kwa mbuzi anayekamuliwa hupunguza kiwango cha maziwa.