Ni muhimu kwa wafugaji kutumia makingo katika kuzalisha malisho aina ya nyasi na mikunde ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa malisho bora na ya kutosha.
Makingo hutengenezwa kwa kuchimba mitaro na kupanda majani kwenye mistari ya kontua. Makingo pia huweza kutengenezwa kwa kutumia mawe, takataka au mabaki ya shambani baada ya mavuno.
Umuhimu wa makingo
Makingo yanahitajika sana kwenye mashamba yaliyo kwenye miteremko au hata ya kawaida ili kulinda rutuba ya udongo na kuzuia mmomonyoko wa ardhi ambao njia za kawaida za matayarisho ya shamba haziwezi kuzuia mmomonyoko huo.
Wakati unaofaa kutengeneza makingo
Wakati wote wa kiangazi unafaa kwa shughuli za upimaji na uchimbaji wa makingo. Aidha, wakati mzuri zaidi ni mara tu baada ya mavuno kuondolewa shambani kwasababu kutakuwa na nafasi ya kutosha kufanya upimaji, ili shughuli za kuchimba ziendelee shambani na utayarishaji wa shamba.
Jinsi ya kupanda nyazi za malisho kwenye makingo
Panda nyasi za malisho kama vile majani ya tembo, Guatemala na setaria katika ardhi iliyotayarishwa vizuri juu ya making. Pia, waweza kupanda malisho jamii ya mikunde kama vile fundofundo pamoja na nyasi ili kuweza kurutubisha udongo na kusaidia mifugo kupata mchanganyiko maalumu wa wanga na protini wakati wa kulisha.
Njia ya kupanda
- Kupanda nyasi kwa kutumia shina la mizizi
Mara baada ya kukata majani kwa ajili ya kulishia mifugo, ng’oa mashina ya majani na gawanya mashina hayo katika vipande vidogovidogo vyenye mizizi.
Chimba vishimo vyenye kina cha sentimita 10 juu ya makingo na kisha panda vipande hivyo.
Nafasi kati ya simo na shimo iwe ni kati ya sentimita 30 au futi moja tu kupanda vipande hivyo vya mashina.
- Kupanda nyasi kwa kutumia pingili za shina
Kata mashina ya majani yaliyokomaa katika vipande vidogovidogo na hakikisha kila kipande kina vifundo vitatu au vinne kisha vipande kwa nafasi ya sentimita 30 au futi moja toka shina na shina.
Vipande hivyo visukumwe kwenye udongo vikiwa vimeinama ili kifundo kimoja au viwili vibakie juu ya udongo na vifundo vingine viwili viwe chini ya udongo.
Ili kufanya making yajae mapema nay awe mapana ni vizuri kupanda mistari miwili au mitatukatika kila tuta.
- Kupanda mbegu za nyasi
Nyasi zinazoweza kustawishwa kwa njia ya mbegu ni pamoja na Chloris gayana (Rhodes grass), makarikari, molasses grass na Africana foxtail.
Shamba liandaliwe vizuri na mbegu iliyokwisha kutayarishwa ipandwe kwa kutawanyishwa ardhini au kupandwa katika mistari kwa umbali wa sentimita 10 kati ya mstari mmoja na mwingine.
Baada ya mbegu kupandwa zifunikwe kwa udongo wenye kina kisichozidi sentimita moja ili zisishindwe kuota ama zikakaa ardhini kwa muda mrefu na kusababisha kuoza.
- Kupanda nyasi pamoja na mikunde
Ni vyema kupanda mikunde kama vile desmodiuma au fundofundo, siratro, glycine na clitoria ternatea kwenye makingo yaliyostawisha nyasi ili kurutubisha ardhi na kuvuna malisho yenye mchanganyiko wa wanga na protini. Njia mbalimbali za upandaji zilizoelezwa hapo juu zinaweza kutumika kutumika kwenye uoteshaji wa mikunde pamoja na nyasi kufuatana na aina ya malisho yanayostawishwa.
Palizi
Hakikisha unapalilia mapema malisho ili kuondoa magugu shambani yasisonge nyasi na fanya hivyo kila wakati mara tu unapoona magugu yanaanza kuota.
Mbolea
Wakati wa kuotesha, tumia mbolea ya samadi, mboji au mbolea ya chumvichumvi kulingana na ushauri wa Afisa kilimo na pia waweza kuweka mbolea ya kukuzia.
Uvunaji
Kata nyazi zikiwa na urefu wa mita moja, na acha shina lenye urefu wa sentimita kumi wakati wa masika, na sentimita kumi na tano wakati wa kiangazi ili nyasi ziweze kuchipua kirahisi. Pia, wakati huo majani huwa mengi na yenye virutubisho vya kutosha.
Ulishaji
Baada ya kuvuna, wataalamu wanashauri kutakata malisho katika vipande vidogovidogo vyenye urefu usiozidi sentimita 10 ili mifugo iweze kuyala kwa urahisis zaidi. Vilevile unaweza kuyafunga malisho kwa kamba kwenye mti au ukutani ili mbuzi wasiweze kuyavuta chini kwa urahisi na kuyakanyaga kwa wingi.
Mbuzi hupenda kula majani yakiwa yamefungwa juu lakini yakishaanguka chini huyaacha na kuyakanyagakanyaga. Kutokana na hali hiyo, mbuzi huweza kuepukana na hayo kwa kutumia mbinu yeyote itakayozuia uwezekano wa malisho ya mbuzi kuanguka chini na kukanyagwa. Kwa kufanya hivyo, utaweza kudumisha afya ya mbuzi, kuzuia mbuzi kupata minyoo, pamoja na kuzuia uharibifu wa malisho.