Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vijulikanavyo kisayansi kwa jina la Phlebovirus vya kabila la Bunyaviridae. Virusi hivi huenezwa na wadudu waumao hasa mbu wa aina ya Aedes, Anopheles, Culex, Mansonia nk. Ugonjwa huu huwapata ng’ombe, mbuzi, ngamia, kondoo na pia binadamu. Ugonjwa huu pia huwapata wanyamapori kama vile; swala, nyati na nyumbu.
Njia ya maambukizi
Ugonjwa huu huambukizwa kwa kuumwa na mbu au wadudu wengine wanaponyonya damu ya wanyama walioambukizwa virusi vya Homa ya Bonde la Ufa.
Dalili za ugonjwa kwa mifugo
- Homa kali ambayo inaweza kuzidi nyuzi joto sentigredi 41
- Mnyama kuzubaa
- Manyoya kusimama
- Kutupa mimba
- Vifo vingi vya ndama na vitoto vya mbuzi na kondoo. Takribani asilimia 70% ya ndama katika kundi wanaweza kufa na kwa upande wa vitoto vya mbuzi na kondoo ni asilimia 95% hadi 100%.
Ni muhimu sana kwa mfugaji kutoa taarifa kwa watoa huduma za afya ya mifugo mara uonapo moja ya dalili za ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa.
Njia za kuzui maambukizi kwa mifugo
- Kuogesha au kunyunyiza mifugo dawa za kuogeshea mifugo
- Chanja mifugo ambao hawajaambukizwa
- Kuzika kwa tahadhari wanyama waliokufa
Usalama kwa walaji wa nyama
- Kitoweo cha nyama iliyopikwa na kuiva vizuri ni salama
- Tuzingatie tahadhari wakati wa kuchinja na kuandaa kitoweo
- Mishikaki isiyoiva vizuri inaweza kuwa chanzo cha uambukizo
- Ni muhimu kutumia machinjio yaliyo rasmi
- Hakikisha mifugo inakaguliwa kabla na baada ya kuchinja
Muhimu
Ugonjwa huu wa Homa ya Bonde la Ufa hauna tiba. Njia pekee ya kuudhibiti ugonjwa huu ni kila mfugaji kuhakikisha kwamba ng’ombe, mbuzi na kondoo wake wanapata chanjo dhidi ya ugonjwa huu mara moja kila mwaka.
Njia za maambukizo kwa binadamu
- Kuumwa na mbu wanaoeneza ugonjwa huu
- Kugusa damu au majimaji ya mnyama au binadamu aliyeambukizwa
- Kula nyama isiyoiva vizuri
- Kunywa maziwa ambayo hayajachemshwa
- Kuchinja au kula nyama ya mnyama mgonjwa au mnyama aliyekufa
Dalili za ugonjwa kwa binadamu
- Homa kali, kuumwa kichwa, maumivu ya mwili na kizunguzungu
- Kichefuchefu, kutapika na kuharisha damu
- Kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni na kwenye ngozi
- Kupofuka macho na
- Kupoteza fahamu
Jinsi ya kuzuia kuambukizwa
- Kutumia chandarua chenye viuatilifu
- Kuvaa vifaa vya kukinga; glovu, koti na buti wakati wa kuchinja na kuchuna mnyama
- Kuepuka kula nyama ya mnyama mgonjwa au mnyama aliyekufa
- Kuepuka kula nyama isiyoiva vizuri na maziwa yasiyochemshwa
- Kusafisha kwa maji na sabuni visu na vyombo vinavyotumika kuandaa nyama
- Kunawa mikono kwa maji na sabuni kabla na baada ya kuandaa nyama