- Mifugo

Udhibiti wa magonjwa ya ng’ombe wa maziwa

Sambaza chapisho hili

Ugonjwa ni hali ambayo inamzuia ng’ombe kuzalisha kwa kiwango kikubwa kulingana na uwezo wake. Hii inajumuisha upatikanaji wa lishe bora na ambayo ni chanzo kikuu cha aina nyingi za yanayosumbua mifugo. Wafugaji wanafaa kuwapa mifugo wao chakula cha kutosha ili kujenga afya na kinga ya mwili na kuepukana na maradhi mengi.

Ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ni shughuli muhimu kwa wakulima wadogo, kwani hutoa maziwa kwa matumizi ya nyumbani na mapato kwa mfugaji. Hata hivyo, ng’ombe wa maziwa wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali yanayoweza kupunguza uzalishaji wa maziwa, kusababisha hasara kubwa ya kifedha, na hata kusababisha vifo ikiwa hayatatibiwa mapema.

Kwa wafugaji wadogo, utambuzi wa mapema wa magonjwa na usimamizi mzuri inadumisha mifugo wenye afya na wanaoleta tija. Tuangazie magonjwa ya kawaida ya ng’ombe wa maziwa, jinsi ya kuyatambua, na mbinu bora za kuyadhibiti.

Visababishi vya magonjwa

Magonjwa ya ng’ombe wa maziwa husababishwa na mambo mbalimbali;

  • Bakteria: Husababisha magonjwa kama wa kiwele/matiti (mastitis), kifua kikuu na kadhalika.
  • Virusi: Husababisha magonjwa kama ugonjwa wa midomo na miguu (Foot-and-Mouth DiseaseFMD).
  • Vimelea; mfano, kupe ambao husababisha homa ya ndigana kali (East Coast Fever – ECF), na nzi wa mbung’o wanaosababisha ugonjwa wa Nagana.
  • Kuvu (fangasi); husababisha maambukizi ya ngozi na matatizo ya lishe kutokana na chakula chenye ukungu.
  • Upungufu wa lishe na madini ya kutosha huweza kusababisha magonjwa kama homa ya maziwa (Milk Fever). 

Jinsi magonjwa yanavyoenea

Magonjwa ya ng’ombe huenea kupitia;

  • Kutangamana na mifugo kugusana moja kwa moja na ng’ombe wagonjwa huleta uwezekano mkubwa wa kuambukizana magonjwa.
  • Chakula na maji machafu, yanayoweza kuwa na bakteria au vimelea hasa wakati ambapo mifugo wanakula chakula kichafu au kutumia vyombo vichafu na hata kunywa maji chafu.
  • Kufuga kwenye mazingira yenye kupe, mbung’o, mbu na wadudu wengine wanaosambaza magonjwa.
  • Usafi duni bandani na malishoni, husababisha maambukizi kama ugonjwa wa kiwele/matiti.
  • Usimamizi mbaya, mfano, kutembeza au ng’ombe kiholela huongeza uwezekano wa mifugo kupata na kusambaza magonjwa.

Kuzuia magonjwa

  • Kuzuia magonjwa ni vyema kuliko kutibu kwani mfugaji anaweza kupunguza uwezekano wa mifugo wake kuambukizwa na pia kuondokana na gharama kubwa ya kuwatibu ng’ombe wagonjwa. Baadhi ya njia za kuzauia magonjwa ni;
  • Kudumisha usafi wa mabanda na vifaa vya kulishia na kukamulia maziwa.
  • Kufuatilia ratiba za chanjo ili kuwapa mifugo uwezo wa kupata magonjwa na pia kustahimili maambukizi.
  • Kutoa lishe bora na safi kwa mifugo. Ni muhimu mifugo kupewa lishe ya hali ya juu yenye virutubisho na madini ya kutosha, hasa vya kujenga mwili, kuipa mwili guvu nay a kujenga kinga dhidi ya magonjwa, madini na maji ya kutosha.
  • Kudhibiti wadudu kama vile kupe na nzi (hasa mbung’o). Waogeshe ama wanyunyize mifugo mara kwa mara (ikiwezekana kila wiki) ukitumia dawa viuadudu. Pia, hakikisha mifugo hawatembei ovyo-ovyo hasa barabarani na kwenye malisho ama nyasi ndefu.
  • Tenga na kuwatibu wanyama wagonjwa ili kuepuka magonjwa kuenea.

Baadhi ya magonjwa muhimu

Ugonjwa wa kiwele (mastitis)

Ugonjwa huu huambukiza kiwele na matiti na mara nyingi husababishwa na bakteria ambayo hupatikana sana sana katika mazingira chafu, matumizi ya vyombo chafu ya kukamulia na vyombo ambayo vimetumika kukamulia ng’ombe mwenye maambukizi.

Dalili zake ni;

  • Kiwele kuvimba na kuwa na maumivu. Ng’ombe anakataa kukamuliwa au anarusha mateke mara sehemu ya kiwele au matiti yanapoguzwa.
  • Ugonjwa unasababisha ng’ombe kupunguza uzalishaji wa maziwa, na anapokamuliza, maziwa huwa na madonge, usaha, au damu.
  • Ikiwa ng’ombe hatatibiwa kwa haraka, anaweza kuwa na joto na homa kali.

Ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa kupitia;

  • Usafi wakati wa kukamua. Nawa mikono ukitumia maji safi, kisha safisha kiwele na matiti kabla na baada ya kukamua.
  • Mbali na usafi, hakikisha hautumii nguvu nyingi, kufinya matiti au kuvuta kupita kiasi.
  • Ili kutibu, tumia viuavijasumu (antibiotics) kulingana na maelekezo, naushauri wa daktari wa mifugo.
  • Tenga na kukamua mwisho ng’ombe walioambukizwa ili kuepuka maambukizi zaidi.

Ndigana kali (East Coast Fever – ECF)

Ugonjwa huu ni hatari na unasababishwa na kupe, na unaweza kusababisha hasar kubwa kwa mfugaji.

Dalili zake ni;

  • Joto na homa kali.
  • Tezi za ng’ombe kuvimba, hasa zile zinazopatikana shingoni.
  • Ugumu wa kupumua au ng’ombe kuonekana anatumia nguvu nyingi kupumua kiasi kwamba mwili wake inatingika.

Ng’ombe anakosa nguvu, hamu ya chakula, na kufa ikiwa hatatibiwa mapema.

Ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa kupitia;

  • Kupulizia au kuzamisha ng’ombe kwenye dawa ya kuua kupe mara kwa mara. Hakikisha unatumia kiwango kichachofaa cha dawa ili kuzuia wadudu kuwa na uwezo wa kustahimili makali ya dawa baada ya muda. Pia, usipitishe kiwango kwani unaweza kuwadhuru mifugo wako.
  • Chanja mifugo dhidi ya ECF. CHanjo hii inapatika, ila shauriana na afisa wa mifugo katika eneo lako.
  • Matibabu ya mapema itawasaidia ng’ombe wa walioathirika. Pia, pata ushauri kutoka kwa afisa wa mifugo kabla ya kutumia tiba yoyote.

Ugonjwa wa midomo na miguu (Foot-and-Mouth Disease – FMD)

Ugonjwa huu wa virusi huenea haraka sana kupitia mgusano wa moja kwa moja au vifaa vilivyochafuliwa.

Dalili ni pamoja na;

  • Vidonda kwenye midomo, fizi, kwato, na kiwele.
  • Ulemavu kwa sababu ya maumivu kwenye kwato.
  • Kutokwa na mate mengi na kushindwa kula
  • Kushuka kwa uzalishaji wa maziwa

Ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa kupitia;

  • Kuwatenga mifugo wagonjwa. Tenga eneo maalum ili kuwashughulikia bila kuwaambukiza wengine.
  • Wape chanjo mifugo wako mara kwa mara.
  • Dhibiti uingiaji wa watu, magari na vifaa vingine kwenye shamba unapowafugia ngombe.
  • Tibu mifugo kulingana na dalili ili kupunguza maumivu. Pia, wape ng’ombe walioathirika chakula laini.
  • Kudumisha afya ya ng’ombe wa maziwa ni muhimu kwa uzalishaji wa maziwa wenye faida. Wakulima wanapaswa kuwa waangalifu katika kutambua magonjwa mapema, kuchukua hatua za kinga, na kupata usaidizi wa wataalamu wa mifugo mara magonjwa yanapotokea.
  • Tutaendelea kuangazia magonjwa mengine ya ng’ombe wa maziwa katika matoleo yajayo ya jarida hili.
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *