Kuku
- Mifugo

Tumia mihogo kulisha kuku

Sambaza chapisho hili

Kuku

Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa nyuzi za mihogo zinaweza kutumika kwa ajili ya chakula cha kuku wanaotaga.

Sekta ya kuku hapa Tanzania hutegemea nafaka pamoja na jamii ya kunde kwa ajili ya kutengeneza lishe ya kuku. Nafaka kama vile mahindi, mtama, ngano na shayiri ni chanzo kikubwa cha vyakula vya nguvu katika ulishaji wa kuku. Jamii ya kunde kama soya na mazao aina nyingine kama vile alizeti na mbegu za pamba vikiwa ni vyanzo muhimu vya protini.

Hata hivyo, viungo hivi ni ghali na upatikanaji wake ni wa msimu. Aidha, uzalishaji wake mara nyingi huathiriwa na uhaba wa mvua. Jambo hili limepelekea utafutaji wa viungo mbadala kwa ajili ya kutengenezea lishe hapa Tanzania na kwingineko.

Mihogo ni moja ya mazao muhimu ya chakula hapa Tanzania. Zao hili hulimwa na kuzalishwa katika mikoa yote ya Tanzania. Maeneo makuu yanayozalisha zao hili ni pamoja na Mwanza, Mtwara, Lindi, Shinyanga, Tanga, Ruvuma, Mara, Kigoma, mikoa ya Pwani pamoja na baadhi ya mikoa ya Zanzibar. Pamoja na uwepo wake kwa wingi hapa nchini, matumizi yake kwa binadamu ni madogo sana.

Kwa mujibu wa taaarifa ya FAO, inakadiriwa kuwa Afrika inazalisha asilimia 42 ya jumla ya mihogo yote inayozalishwa katika ukanda wa kitropiki duniani. Zao hili lina uwezo wa kukua katika eneo dogo, huku likihitaji pembejeo kidogo sana na ni vumilivu kwa wadudu pamoja na ukame.

Matumizi ya mizizi pamoja na maeneo mengine ya mmea wa muhogo ni pamoja na kutumiwa kama lishe ya wanyama katika jamii nyingi za kiafrika na Asia. Huko Asia, takribani mihogo yote inayozalishwa hutumiwa kwa ajili ya kulishia mifugo pamoja na kuzalishia wanga. Sekta ya wanga huzalisha bidhaa za ziada inayojulikana kama tapioca ambayo hutumiwa kwa ajili ya kulishia ng’ombe pamoja na nguruwe.

Tofauti na Asia, uzalishaji wa mihogo hasa ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu kwa nchi ya Tanzania pamoja na nchi zingine za Afrika Mashariki na Magharibi.

Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa nyuzi za mihogo zinaweza  kutumika kwa ajili ya chakula cha kuku wanaotaga. Pia imegundulika kuwa, badala ya kutumia mahindi, kiasi kidogo cha nyuzi za mihogo zinaweza kutumika katika utengenezaji wa chakula cha kuku wanaotaga bila kuharibu uzalishaji wa mayai pamoja na ubora wake, isipokuwa hubadili kiini cha yai, ambacho hubadilika kutokana na virutubisho vilivyopo katika nyuzi za muhogo.

Faida za mihogo

Tofauti na Asia, uzalishaji wa mihogo hasa ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu kwa nchi ya Tanzania pamoja na nchi zingine za Afrika Mashariki na Magharibi.

Bidhaa nyingi za lishe zinazotokana na mihogo ni pamoja na chipsi na marisawa (pellets), ambazo hukaushwa na kusagwa. Majani ya mihogo pia huweza kutumika kulishia kuku. Majani haya hukaushwa na kusagwa pamoja na mchanganyiko wa chakula na ni chanzo kizuri cha protini kwa kuku. Hata hivyo, huwa na wanga wa kutosha huku mizizi yake ikiwa na kiasi kidogo cha protini.

Hii ina maana kuwa, lishe ya mihogo inatakiwa kuwa na carotene ili kudumisha rangi ya kiini cha yai. Ni vizuri pia kulisha kuku mchanganyiko wenye virutubisho vya asili vya mmeng’enyo. Hii itasaidia kuku kumeng’enya chakula vizuri na kunyonya madini pamoja kudumisha rangi ya kiini cha yai.

Vimeng’enyo (Microbial Enzymes): Viini hivi vinapatikana kwa mawakala wa lishe ya mifugo na baadhi ya maduka ya kilimo yaliyopo Tanzania. Halikadhalika, viungio vya madini ya rangi vinahitajika kuongezwa katika lishe ili kusaidia kudumisha rangi ya njano ya kiini cha yai.

Matumizi ya mihogo badala ya Mahindi

 Wakati wa kutengeneza chakula cha kuku, unaweza kutumia resheni ya mihogo kwa kiasi cha asilimi 20 badala ya mahindi katika mchanganyiko wote. Aina mbili za chakula cha kuku zinaweza kuzalishwa kwa kutumia mihogo.

(a) Resheni inayotumia soya bila kuchanganya dagaa: Mchanganyiko huu huwa na resheni ya: Kilo 40 za mahindi, kilo 10 za mihogo, kilo 26.8 za soya, kilo 23.2 za mchanganyiko wa mashudu ya alizeti na pamba, pumba ya mahindi na ngano.

(b) Resheni inayotumia dagaa bila soya: Mchanganyiko huu huwa na: Kilo 40 za mahindi, kilo 10 za mihogo, kilo 13.4 za dagaa, kilo 36.6 za mashudu ya alizeti na pamba, pumba za mahindi na ngano.

>> Umenufaika kutoka na makala hii? Tushirikishe kwa kuacha maoni yako hapa chini ama kuandika barua pepe kwa info@mkulimambunifu.org

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *