- Mifugo

Tumia kilimo cha mzunguko kudhibiti wadudu na magonjwa

Sambaza chapisho hili

Mimi ni msomaji wa jarida la Mkulima Mbunifu, nimekuwa nikivutiwa na makala za uzalishaji wa mazao kwa njia ya asili. Naomba kufahamishwa ni kwa namna gani naweza kudhibiti wadudu na magonjwa kwenye bustani yangu bila kutumia dawa yoyote?

Wadudu na magonjwa visipodhibitiwa, humsababishia mkulima hasara kwa kiasi cha asilimia 20 hadi 80. Kutokana na hali hiyo, ni muhimu kuzuia magonjwa na wadudu kwa kutumia njia mbalimbali kama vile kutoa magugu, kubadili mazao kwa njia ya mzunguko na kutumia madawa ya asili ambayo yanaweza kuwa shambani kwa muda mrefu.

Njia za kuzuia wadudu na magonjwa

Kufanya kilimo cha mzunguko

Kilimo cha mzunguko ni njia ya asili ya kulima mazao kwa kubadili aina ya mazao kila msimu kwenye eneo moja la shamba au kitalu.

Kwa mfano; msimu huu unapanda zao la maharagwe au kunde na msimu unaofuata unalima kabichi, mchicha au matembele. Yaani, unabadilisha aina ya mazao kwa kuangalia zao husika lipo kwenye kundi gani la mazao na kuangalia kama zao unalotaka kulilima linakinzana kitabia na zao lililovunwa.

Kuzuia magonjwa

Kwa kuendelea kuotesha/kupanda zao la aina moja kwa zaidi ya msimu mmoja ni dhahiri kuwa magonjwa mengi huibuka na huwa sugu kuisha na kufanya udhibiti wake kuwa mgumu sana, lakini kwa kufanya kilimo cha mzunguko wa mazao utafanikiwa sana kupunguza/kuondoa kabisa magonjwa hayo.

Kuzuia Wadudu

Wadudu kama minyoo fundo huwa si rahisi sana kufa ama kupote shambani hasa ikiwa unatumia desturi ya kupanda mazao yale yale kwa muda wa zaidi ya msimu mmoja, au kwa kupanda mazao yaliyo kwenye jamii moja hivyo njia ya kudhibiti ni kufanya kilimo cha mzunguko wa mazao.

Nini faida za kilimo cha mzunguko?

  • Kuongeza na kuimarisha virutubisho kwenye udongo hasa pale mazao jamii ya mikunde inapopandwa.
  • Kupunguza na kuondoa wadudu waharibifu.
  • Kupunguza uwezekano wa kuwepo magonjwa shambulizi.
  • Rutuba ya udongo hutumika vyema na mazao yatakayo badilishana.

Njia zingine za kudhibiti wadudu na magonjwa

Mbali na kufanya kilimo cha mzunguko wa mazao, unaweza pia kutumia njia zifuatazo kudhibiti wadudu na magonjwa, pamoja na kuepuka kutumia viuatilifu ambavyo mara nyingi huwa na madhara kwa binadamu, mimea na wanyama, pamoja na kupunguza gharama zisizo za lazima katika kilimo;

Kuweka matandazo

Majani au nyasi kavu huwekwa chini ya mimea karibu na shina au eneo lote la shamba hata pasipo na mimea. Lengo la kuweka matandazo ni pamoja na:

  • Kuzuia wadudu kuzaliana kutokana na magugu
  • Kuhifadhi maji/ unyevunyevu
  • Kuongeza joto kwenye udongo na
  • Kurutubisha udongo
  • Kuzuia magugu kuota

 

 

 

 

 

 

 

  1. Kufahamu mazingira sahihi ya zao husika

Zipo aina za mazao, ambazo hupendelea kustawi katika mazingira fulani fulani. Kwa mfano kuna aina za mboga ambazo huwezi kulima kwenye maeneo ya joto na nyingine huwezi kulima kwenye maeneo ya baridi

  • Sehemu za baridi- Hulimwa mboga kama kabichi, cauliflower, broccoli
  • Sehemu za joto- Hulimwa matango, maboga, matembele, mchicha, matikiti, nyanya, bilinganya, ngogwe, na pilipili
  • Sehemu za uvugu vugu- Hulimwa vitunguu, nyanya, karoti, spinachi, lettuce, sukuma wiki n.k

Muhimu

Ni vyema sana mkulima kuhakikisha kuwa anamshirikisha mtaalamu wa kilimo katika shughuli zake za shambani hasa juu ya kulimo cha mzunguko ili aweze kumuelewesha ni mazao ya jamii gani yanastahili kupandwa kwenye msimu upi na ni mazao ya jamii gani yanastahili kufuata.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *