Kila nikihifadhi chakula cha kuku baada ya muda fulani nakuta kimeanza kupata ukungu na wakati mwingine kuwa na harufu kali sana kama ya kuchacha, naombeni msaada wenu. 0654 624229 Dodoma
Chakula cha kuku kinapozalishwa katika hali nzuri na kwa kufuata kanuni sahihi huweza kuhifadhiwa na kutumika kulishia kwa muda mrefu sana bila kuharibika.
Tatizo ambalo mara nyingi huwakuta wafugaji walio wengi, ni kuhifadhi chakula hichi kwa njia asiyosahihi na kupelekea kuharibika kiasi kwamba hata wakati mwingine kuzalisha wadudu.
Chakula cha kuku ni bidhaa muhimu inayohitaji kutunzwa kwa umakini zaidi kwani kisipotunzwa vizuri nab ado kikaendelea kulishia, basi kuku wanaweza kuumwa, kuacha kutaga na hata kupelekea kufa.
Sababu za chakula cha kuku kuharibika
Wanyama wanaoharibu nafaka
Wanyama kama panya, na panya buku ni wajanja na wepesi sana kujua sehemu unayotunzia chakula na wakifika huanza kutoboa mifuko na kuanza kula huku wakiacha chakula kingine ikiendelea kumwagika chini.
Pia, wanyama hawa wanabeba magonjwa ambayo yanaweza yakaathiri chote na kuku watakapokula wanaweza wakapata madhara.
Wadudu waharibifu
Kuku wanapenda kula wadudu lakini siyo wadudu wote ni safi kwa kuku. Wadudu kama nodno na mende wanapenda kula chakula cha kuku na kuishi humo.
Wadudu hawa wanaweza kubeba magonjwa ambayo huathiri chakula cha kuku na pindi utakapotumia kulisha kuku huweza kuumwa na hata kufa.
Fangasi au ukungu
Utunzaji mbaya wa chakula hupelekea chakula kupata fangasi au ukungu na chakula cha kuku kuwa mabonge mabonge.
Fangasi au ukungu inavyosambaa kwenye chakula hupelekea kutengeneza mycotoxin ambayo ni sumu kwenye chakula na inaweza kukipa chakula ladha mbaya na kuku hawatakipenda.
Unyevunyevu
Changamoto kubwa ya kutunza chakula ni unyevunyevu ambao unahamasisha ukuaji wa fangazi au uvundo. Hakikisha sehemu unayotunzia chakula cha kuku ni kukavu na kuna hewa ya kutosha ili kuondoa unyevunyevu.
Chakula kilichooza
Chakula cha kuku kilichochanganywa vitu vya aina mbalimbali hakitaweza kudumu kwa muda mrefu. Mafuta au mashudu yanayotumika katika kutengeneza chakula cha kuku mara baada ya muda huoza na kufanya chakula chote cha kuku kuoza pia.
Chakula hiki kinakuwa na harufu mbaya na kinakuwa na sumu ambayo itapunguza sana ukuaji wa kuku. Pia kuku hawatapenda kula chakula hiki na utaona wakipungua uzito siku hadi siku. Ni muhimu sana kutunza chakula cha kuku kwa usahihi
Chakula cha kuku kitunzwe kwa muda gani
Chakula cha kuku kitakaa kwa muda mrefu kama kitatunzwa kwenye mazingira makavu na yenye hewa ya kutosha kwa muda wa miezi mitatu hadi sita.
Aidha, chakula cha kuku mitaharibika haraka kama kikipata jua, unyevunyevu na kuchezewa na wanyama na wadudu waharibifu.
Chakula cha kuku kitunzwe sehemu gani
Weka chakula cha kuku kilichopakiwa kwenye mifuko sehemu kavu yenye ubaridi, na mifuko hii yenye chakulayawekwe juu ya mbao au miti. Hakikisha chakula hakikai juu ya sakafu kwa hupelekea kuganda na kuweka uvundo.
Muhimu:
Wafanye kuku wako wawe na furaha kwa kuhakikisha chakula chao kinatunzwa sehemu salama, kavu na yenye ubaridi.
Hii itakusaidia kutopata tatizo la chakula kuvunda na kuoza huku kuku wakiwa na safi, kukua haraka na kutaga mayai mengi.