Pamoja na kuwa kuna magonjwa mengi yanayoweza kuathiri mbuzi, pia sumu zinazopatikana katika baadhi ya miti, mimea, dawa au hata wanyama, huweza kusababisha mbuzi kufa mara atakapokula.
Baadhi ya sumu zinazoweza kusababisha mbuzi kufa ni kama zifuatayo;
1. Sumu ya lukina
Mmea huu una sumu iitwayo mimosine, ambayo ikiliwa kwa kiasi kikubwa huleta madhara kwa mbuzi.
Dalili
Mbuzi aliyekula sumu hii ngozi yake hujenga mabaka ya utando ambao baadaye hubanduka.
Jinsi ya kuzuia
Hakikisha mbuzi hali kiwango cha lukina kinachozidi 1/3 ya malisho yote anayolishwa kwa siku.
2. Sumu ya lantana camara
Mmea huu haupendwi na mbuzi, lakini mara nyingi mbuzi wakiwa na njaa kali hula. Hali hii hutokea wakati wa ukame, ambapo malisho huadimika kwa kiasi kikubwa.
Mbuzi akila kiasi kikubwa cha mmea huu hudhurika sehemu za kichwani na masikio.
Dalili
Mwanga wa jua humuumiza mbuzi macho na kumfanya auogope mwanga huo na mara nyingi kukaa kivulini au kuligeuzia jua mgongo.
Sehemu nyeupe au zenye rangi hafifu zinazopigwa na jua hupata vidonda na mbuzi huweza kuharisha sana.
Tiba
Mbuzi atunzwe mahali penye kivuli na vidonda vitibiwe kwa kutumia Sulfanilamide ya unga. Tumia dawa ya kufukuzia inzi kama kutakuwa na haja.
Jinsi ya kuzuia
Mbuzi wasilishwe mimea hii na kama ni lazima walishwe basi wapewe kiwango kidogo sana.
3. Sumu ya mmbono
Sumu iitwayo ricin hupatikana zaidi kwenye mbegu na vilevile kenye majani na shina la mmbono.
Dalili
Mbuzi akila sumu hii hutapika, hupata kiu sana, huharisha na uyeyushaji wa chakula tumboni husimama na hatimaye mbuzi hufa.
Jinsi ya kuzuia
Namna ya kuzuia sumu hii ni moja tu, hakikisha mbuzi hawali mmea huu.
4. Sumu ya ndulele
Sumu ya glycoalkaloids inayopatikana kwenye matunda ya ndulele si nzuri kwa mbuzi japokuwa mbuzi huweza kula kwa nadra sana.
Dalili
Mbuzi aliyekula sumu hii hupata udhaifu na kuanza kutetemeka, kuvimbia au kuharisha na hatimaye kufa.
Jinsi ya kuzuia
Mbuzi wasiachwe bila kupewa malisho kwa muda mrefu na kisha kulishwa malisho yenye mchanganyiko wa mmea huu ili kuepuka kula sumu.
5. Sumu ya dawa za kuogeshea
Mbuzi akimeza sumu hii hutoa machozi na mate, huwa na mshtuko, hutoa jasho na huweza kufa ghafla.
Tiba
Ikigundulika kuwa mbuzi amekula sumu hii, basi atibiwe kwa kudungwa sindano ya atropine sulphate
Jinsi ya kuzuia
Hakikisha dawa hizi zinawekwa mbali na mbuzi, hasa dawa za kuogeshea kama vile organophosphate.
6. Sumu ya nyoka
Mbuzi akiumwa na nyoka akiwa malishoni na kupata sumu ya nyoka humuathiri.
Dalili
Mbuzi huweza kupumua kwa shida, kuwa na mshtuko, kutoa mate na jasho na hata kufa kwa ghafla.
Tiba
Mbuzi apatiwe dawa ya sumu ya nyoka kama ameumwa mguu kwa kufunga kamba upande wa juu wa mguu ili kupunguza kuenea haraka kwa sumu mwilini.
Pia mbuzi anaweza kutibiwa kwa kupatiwa antibaiyotiki na asteroid.
Jinsi ya kuzuia
Epuka kulisha mbuzi kwenye mazingira ambayo yataongeza uwezekano wa mbuzi kuumwa na nyoka.
Matatizo ya vidonda kwa mbuzi
Vidonda huweza kusababishwa na vitu vyenye makali au ncha kali kama vile misumari, seng’enge, mabati, miiba na hata pembe wakati mbuzi wanapocheza au kupigana wenyewe.
Vidonda huchukua muda zaidi kupona ikiwa vitakuwa vinafikiwa kwa urahisi na inzi.
Jeraha la mbuzi huonekana kwa haraka mara baada ya mbuzi kukatwa ua hata kutobolewa.
Tiba
Tibu kidonda cha mbuzi mapema kabla hakijaungua na kuongezeka ukubwa.
Safisha kidonda kwa dawa ya kuangamiza vijidudu kama vile salvon.
Ikiwa ni vigumu kupata dawa hii, chemsha maji safi na kisha yapooze. Maji yakiwa ya uvuguvugu, safisha kidonda kwa kutumia maji hayo na sabuni.
Nyoa manyoya kuzunguka eneo hilo lenye kidonda, kisha angalia kama kidonda hicho kitafungwa au kushonwa.
Ikiwa kidonda kitafungwa, tumia dawa ya antibaiyotiki ya kupaka au iliyo katika hali ya unga kuweka kwenye kidonda na kukifunga.
Kama kikifungwa bandeji kitaweza kubakia katika hali ya ukavu. Funga kwa bandeji, na ikiwa ukifunga bandeji haitabaki katika ukavu basi acha kidonda katika hali ya uwazi.
Baada ya kufanya hayo, paka dawa ya kufukuza inzi kama vile pygrease pembeni mwa kidonda na siyo juu ya kidonda.