- Mifugo

Punda anahitaji kutunzwa kama mifugo mingine

Sambaza chapisho hili

Punda ni mnyama anayefugwa na wengi lengo likiwa kutumika kutoa msaada wa nguvu kazi nyumbani hasa kwa kuwa njia nzuri ya kubebea mizigo.

Mnyama huyu ambaye hutumiwa hasa na kina mama na watoto wa jamii ya kimasai na nyinginezo kwa ajili ya kubebea maji, kuni, majani, kupelekea mizigo sokoni na shughuli zote zile za nyumbani amekuwa hana thamani kama waliyonayo wanyama wengine wafugwao kama ng’ombe.

Wafugaji wengi wameshindwa kuwatimizia punda mahitaji yao ya msingi kama vile malazi mazuri pamoja na lishe. Aidha, wamekuwa wakiwabebesha mizigo mara kwa mara bila kuwapumzisha na hata kuwabebesha mizigo mizito kupita uwezo wao. Kwa kufanya hivyo, ni kupoteza haki za msingi za mnyama huyu.

Misingi bora ya utunzaji wa punda.

Ili punda awe na afya na nguvu siku zote, ni lazima apate vitu vifuatavyo:

Chakula bora: Punda anatakiwa kula nyasi au pumba za mahindi, pumba za ngano, mashudu ya pamba au alizeti.

Maji: Ni lazima kuhakikisha punda anakunywa maji ya kutosha muda wote ambao hafanyi kazi.

Banda: Hakikisha punda ana banda safi na bora la kupumzikia akiwa hafanyi kazi na kulala wakati wa usiku. Banda hilo liwe limeezekwa vyema kumkinga na mvua, jua na upepo mkali.

Umri na Kazi: Usimbebeshe mizigo wala kuvuta mkokoteni punda mwenye umri  chini ya miaka mitatu.   Usimfanyishe punda kazi nzito sana na kwa punda mwenye mimba zaidi ya miezi minane au ambaye hajafikisha miezi mitatu toka kuzaa, asifanyishwe kazi yeyote.

Dawa na chanjo: Kama ilivyo kwa mifugo mingine, ni muhimu kuwasiliana na wataalamu ili punda apatiwe chanjo pamoja na kutibiwa kwa usahihi pindi anapokumbwa na magonjwa.

Punda anahitaji matunzo mazuri ili aweze kufaidisha mfugaji

Elimu kutoka MAWO imetufungua akili

“Hatukuwa na elimu ya kutosha juu ya misingi bora ya utunzaji wa punda lakini kwasasa, elimu tuliyoipata kupitia MAWO (Meru Animals Welfare Association) imetufanya tumthaminishe punda na wanyama wengine na kwa kufanya hivyo, tunategemea baada ya muda mfupi tutakuwa wajasiriamali wakubwa.”

Hivyo ndivyo alivyoanza kueleza Bi. Esther Nairowa ambaye ni mwenyekiti wa kikundi cha kinamama kilichopo Simanjiro (EOLS) kinachosimamiwa na chama cha huruma kwa wanyama (MAWO).

EOLS imetokana na maneno ya kimasai “Edamunoto Osikiria Loborsoit Simanjiro” ikiwa na maana ya kumbukumbu ya punda wa (Simanjiro remembering of donkey in Simanjiro).

Mama huyo anaeleza kuwa MAWO walifundishwa namna bora ya kutunza punda ikiwa ni kwa kuwabebesha mizigo kulingana na uwezo wao, kuwapa chakula cha kutosha pamoja na kuwatengenezea matandiko ambazo zitawasaidia kutokuumia wakati wa kubeba mizigo.

Baada ya kupata elimu hiyo, baadhi ya kinamama waliamua kujiunga katika kikundi na kuanza kutengeneza matandiko ambayo wanatumia wao wenyewe na pia wanawafundisha wengine ili waweze kutengeneza kwa ajili ya punda wao. Alieleza”.

Matandiko haya yamekuwa yakipendwa na watu wengi hasa kutokana na kuwa yanamlinda punda kutokuchubuka pindi anapofungiwa mzigo iwe ni wakati wa mvua au kiangazi, hivyo kumuwezesha kuepuka kutokewa na vidonda ambavyo mwisho wake humfanya kudhoofika, hushindwa kufanya kazi na mwishoni hufa.

Mahitaji

Akieleza vitu vinavyohitajika kwa ajili ya kutengeneza matandiko hayo, ni pamoja na magunia na mifuko ya salfeti ambazo wanazinunua, nyasi, blanketi, shuka zilizoisha au nguo zilizochoka, pamoja na manila kwa ajili ya kushonea.

Namna ya kutengeneza matandiko hayo

Esther anaeleza kuwa, ni rahisi sana kutengeneza matandiko hayo kama ukiwa na vifaa alivyovitaja hapo juu. Utengenezaji wake ni kama ifuatavyo;

  • Chukua nyasi kiasi cha kutosha mgongo wa punda kisha weka katikati ya mfuko wa salfeti na gunia.
  • Shonea nyasi ndani ya gunia na salfeti kwa kutumia manila kwa kugawanya manyani ndani ili kupata mchoro wa vipande zaidi ya nne kwenye tandiko. Kushona kwa kugawanya kunasaidia nyasi zisihame wakati wa kubeba mzigo.
  • Chukua blanketi lililochakaa ama nguo zilizochakaa kisha tengenezea kamba zitakazotumika kufungia tandiko na mzigo.
  • Chukua kamba hizo na shonea kwenye pembe za tandiko.
  • Kama utatumia kamba ya katani basi hakikisha unapata mpira wa pipe kwa ajili ya kuvalisha hiyo kamba ili kuzuia kamba isimkate punda ukishamfungia au shonea blanketi kwenye hiyo kamba.

Nini malengo ya kikundi

Mama huyu aneleza kuwa, lengo lao kubwa ni kufundisha watu wengi na hatimaye jamii nzima kujua na kuzingatia kanuni bora za utunzaji wa mnyama huyu pamoja na mbwa.

Aidha, anaeleza kuwa, kulingana na uhitaji wa wengi kutengenezewa matandiko hayo, anategemea baada ya muda wataanza kuuza na itakuwa njia nzuri ya ujasiriamali kwa wanakikundi.

Mafanikio

Ikiwa lengo lao kubwa ni kuielimisha jamii, mama huyo anaeleza kuwa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwaelimisha wengi na hadi kufikia sasa, wafugaji waliopo maeneo hayo wengi wao wanatumia matandiko ya kisasa yanayotokana na elimu wanayotoa MAWO pamoja na kikundi chao cha EOLS.

Changamoto

Bi.Esther anaeleza kuwa, changamoto iliyo kubwa ni upokeaji wa elimu hiyo kwa haraka na uhitaji mdogo wa wanajamii kutaka kuelewa na kufundishwa namna ya kutengeneza. Anasema wengi wa wanajamii wa Simanjiro ni wamasai na wanakuwa wagumu kupokea elimu hiyo kwa wakati, hivyo inawalazimu kutumia muda mwingi kuwasisitiza jambo ambalo wangetumia muda huo katika kuwafundisha namna ya kutengeneza.

Wito

Esther anasema, kwa kuwa mnyama huyu ni wa muhimu kwa watu wote, anawaomba wafugaji na wakulima wazingatie misingi bora ya utunzaji wa punda na watumie matandiko mazuri yanayofaa ili kumlinda dhidi ya matatizo yanayoweza kumkabili na kumdhoofishia afya yake na hatimaye kufa na msaada kwa jamii kufikia kikomo.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

4 maoni juu ya “Punda anahitaji kutunzwa kama mifugo mingine

  1. KWA KWELI NAKERWA SANA NA TABIA HASA YA WATU WA SIKONGE TABORA KWAKUWATUMIKISHA PUNDA NA KUWAPIGA MALUNGU WANYAMA HAO WANAPOKUWA WAMEBEBA MIZIGO,KIBAYA ZAIDI WAMEFUNGA KWAMA AKIVUTA MZIGO MZITO MF TOFALI ZA CHOMA 400_500.PIA AKIPIGWA LUNGU.
    INANIUMA SANA TENA SANA,NAJIULIZA AFISA MIFUGO HAWAONI? AU SHERIA INASEMAJE? KUNA MUDA NATAMANI KUJICHUKULIA SHERIA LKN NAOGOPA.
    NAOMBA NIPATE ELIMU PIA MAMLAKA YAKUSIMAMIA KISHERIA BILA MALIPO YEYOTE.KIKUBWA NIWE NA AMANI NA FURAHA NIKIONA MNYAMA ANATENDEWA HAKI KAMA KUATA CHAKULA,KUTIBIWA NK.HAKIKA NIKIKUTUMIA PICHA KAMA UNACHEMBE YA UTU ITAKUUMIZA KABISA.NAOMBA MAMLAKA IFUATILIWE HILO.

    1. Habari,
      Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuwa na moyo wa kuwajali na kuwathamini wanyama na kuwa miongoni mwa wanaopinga ukatili unaofanywa wa wanyama. Naomba uwasiliane na kaka Ayubu Nnko anayejihusisha na uteteaji wa haki za wanyama kwa namba 0784 290 501

  2. Hata ninyi nawachukia sana Tena sana,nlitumanujumbe wangu nikitegemea support LAKINI hakuna majibu yeyote Wala simu.
    Mimi Sina mamraka ila naona namna punda WA huku wanavyoteswa,hakuna mtetezi Wala anayeliona hili.nimeridi Tena kama tunavyotetea haki za watoto wasioongea sawa na wanyama wasioongea.njooni muone wenyewe jinsi wanavyofanyishw kazi nzito,jua Kali,anapigwa rungu sio fimbo rungu narudia Tena ,Tena anapigwa kwenye mbavu,akiwa na mzigo fimbo na mbio akiwa Hana mzigo mwendonule ule,inauma sana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *