Uoteshaji na usiaji wa mbegu katika viriba ni teknologia inayokua siku hadi siku. Zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika katika kutibu udongo unaotumika kwenye viriba ili usiwe chanzo cha kusambaza vimelea vya magonjwa.
Udongo
Mchanganyiko wa udongo unaotumika katika viriba unatakiwa uwe na sifa zifuatazo;
- Uwe na rutuba ya kutosha.
- Usiwe wenye kutuamisha maji, lakini uweze kuhifadhi unyevu wa kutosha.
- Unaoruhusu hewa katika udongo (air circulation).
- Wenye uwezo wa kushikamana na mizizi ya miche.
- Usiwe na vimelea vya magonjwa hatari ya mimea (soil pathogens)
- Usiwe na mbegu za magugu hatari mfano ndago (nut grass)
- Usiwe na wadudu hatari wa mimea mfano minyoo fundo na wadudu wengineo.
Ongezeko la uoteshaji wa mbegu katika viriba
Outeshwaji wa mbegu katika viriba hufanywa na:-
- Taasisi za serikali.
- Taasisi zisizo za kiserikali.
- Watu binafsi.
- Vikundi vya wakulima na mazingira.
- Mashirika mbalimbali.
Malengo ya uoteshaji
- Matumizi binafsi.
- Kiuchumi, kuongeza kipato kwa kuuza miche.
- Mafunzo na shughuli za kiutafiti.
Uoteshaji wa mbegu katika viriba uende sambamba na jinsi ya kutibu udongo (soil treatment).
Zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika katika kutibu udongo unaotumika kwenye viriba ili usiwe chanzo cha kusambaza vimelea vya magonjwa (soil borne pathogens), mbegu za magugu (weed seeds), minyoo hatari kwa miche na wadudu mbalimbali hatarishi.
Njia kuu tano zinazo tumika katika kutibu udongo.
- Kutumia mvuke (steam sterilization)
- Kukaanga
- Kutumia mwanga wa jua (solarization)
- Kutumia viumbe hai wengine (biological control)
Kutibu udongo kwa kutumia mvuke
Kutibu udongo kwa kutumia mvuke ni njia ambayo hutumika kwenye kilimo cha ndani na cha nje ili kuondoa na kuua masalia ya magugu, bakteria na fangasi.
Hivi karibuni njia ya kutibu udongo kwa mvuke imeonekana kuwa ni njia bora na fanisi kwa kutibu udogo.
Vifaa vinavyo tumika
- Pipa la chuma lililofunikwa na kuchomelewa bomba fupi la chuma.
- Bomba la mpira.
- Kuni
- Maji
- Udongo
- Karatasi nyeusi ya nailoni.
- Kasha boksi la mbao la kuweka udongo.
Hatua za kutibu udongo kwa mvuke
- Andaa mahitaji yote kwa ajili ya mchanganyiko wa udongo kama vile mboji au udongo wa msituni, udongo tifutifu na mchanga.
- Pima kila moja kwa kuzingatia uwiano wa 2:2:1 vipimo viwili vya udongo mwitu, vipimo viwili vya mboji na kipimo 1 cha mchanga.
- Changanya barabara mchanganyiko huo na kisha lowanisha kuwa maji mchanganyiko kwa kupindua saa 1 ili kuwachangamsha wadudu na kisha weka kwenye kasha la kuweka udongo.
- Funika udongo ulioloweka kwenye kasha kwa kutumia karatasi nyeusi ya nailoni kuzuia mvuke kutoka nje.
- Weka pipa la kuchemsha maji mafigani na washa moto tayari kwa kuchemsha maji hayo ili kupata mvuke 100% hakikisha pipa limefunikwa.
- Unganisha bomba la mpira kutoka kwenye pipa la maji yaliyo chemshwa kwenda kwenye udongo uliokuwa kwenye kasha ili kuruhusu mvuke kutoka kwenye maji kwenda kwenye udongo kwa muda wa saa moja ili kuuwa bacteria, kuvu, fangasi na mbegu za magugu.
- Uache udongo upoe tayari kwa matumizi.
Angalizo.
- Hakikisha maji yanachemka na kuzalisha mvuke kabla ya kuelekeza kwenye udongo.
- Hakikisha udongo umefunikwa vizuri ili kuzuia mvuke kupotea.
- Zingatia muda ili mvuke uweze kupita katika eneo lote la udongo.
Faida ya kutibu udongo kwa mvuke.
- Kuuwa vimelea vya magonjwa kwenye udongo.
- Kuua mbegu za magugu kwenye udongo mfano baktreria, fangasi na kuvu
- Ni njia mbadala ya kemikali.
- Inarahisisha upatikanaji wa virutubisho vya mimea kutoka kwenye udongo.
- Inaongeza ukuaji wa miche iliyo bora.
Hii ni njia rahisi ya kutibu udongo ambayo mkulima mdogo na mkubwa wanaweza kutumia, pia ni njia salama ya kutibu udongo badala ya kutumia kemikali ambazo huleta madhara kwenye udongo.
Kutibu udongo kwa kutumia mionzi ya jua (solarization)
Matumizi ya mionzi ya jua ni njia rafiki kwa mazingira inayotumika kudhibiti vijidudu, bakteria na magugu kwenye udongo. Mbinu hii inahusisha ufunikaji wa ardhi kwa kutumia mtego. Mara nyingi huwa ni nailoni angavu ambayo hutumika kuruhusu au kusharabu mwanga wa jua.
Jua huunguza udongo katika joto ambalo huua bakteria, wadudu, minyoo fundo, magugu na mbegu za magugu.
Hatua za kutibu udongo kwa kutumia mionzi ya jua.
- Amua wakati wa kufanya, inashauriwa kutibu udongo wako kipindi cha kiangazi ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati ya jua kwa kipindi kisicho pungua miezi miwili.
- Chagua eneo unalotaka kutibu udongo wako.
- Safisha eneo ulilochagua kutibu udongo wako kwa kuondoa masalia ya mazao na aina yoyote ya mimea.
- Lima na tifua udongo wako, hakikisha unakuwa laini kwa kutumia jembe na chepeo (beleshi).
- Sawazisha udongo wako uwe katika usawa kwa kutumia reki.
- Mwagilia udongo wako mpaka uwe na unyevu na usiwe tope.
- Funika udongo wako kwa karatasi ya nailoni angavu na nyembamba. Hakikisha karatasi yako inagusa udongo, bana karatasi yako pembezoni kwa kufunikia na udongo.
Angalizo
- Hairuhusiwi kutumia karatasi za nailoni zenye rangi kwa sababu haziruhusu mionzi ya jua kufika kwenye udongo.
- Acha nailoni yako kwenye udongo kwa muda wa mwezi mmoja ikiwa ni kipindi cha joto kali (kiangazi) na muda wa wiki sita hadi nane kwa kipindi cha joto la kawaida.
- Joto linalo hitajika ni 50 hadi 60 sentigredi chini ya karatasi ya nailoni ambalo linaweza kuuwa bakteria, minyoo fundo na mbegu za magugu sumbufu.
- Angalia joto ridi la udongo kwa kila baada ya wiki kadhaa kwa kutumia kipima joto.
- Ondoa nailoni juu ya udongo baada ya kupata joto ridi linalohitajika, unaruhusiwa kuondoa karatasi hiyo ya nailoni juu ya udongo wako baada ya miezi miwili. Na tayari utakuwa umeweza kutibu udongo wako.
Faida.
- Huua wadudu wote waharibifu katika udongo.
- Huwapa nafasi wadudu rafiki wa mazingira kuendelea kuishi katika udongo.
- Njia hii ni rafiki kwa mazingira na afya ya binadamu
- Ni njia rahisi kutibu udongo ukilinganisha na njia nyingine za kutibu udongo
TAHADHARI: Njia ya kutibu udongo kwa kutumia mionzi ya jua huua wadudu wote wafaao na waharibifu. Hivyo basi wakulima wanashauriwa kuweka mboji ili kufanya vijidudu vifaavyo kuendelea kuishi.
Kwa maelezo zaidi, unaweza kuwasiliana na Suleiman Mpingama wa Horti-Tengeru. Barua Pepe: mpingama@yahoo.com Simu:+255 685 460 300