Ng’ombe ni mifugo ambayo hutegemewa sana na wananchi walio wengi hapa nchini.
Kuna aina tatu za ng’ombe wafugwao hapa nchini, nao ni ng’ombe wa kisasa, kienyeji na machotara.
Faida za ufugaji wa ng’ombe
- Kupata chakula kama vile maziwa na nyama.
- Kupata ngozi ambayo hutumika kama malighafi kwa ajili ya kutengeneza viatu, mikanda, mikoba, nguo na vitanda.
- Kujipatia pesa na pia ni akiba.
- Ufahari na huongeza heshima kwa baadhi ya makabila.
- Kupata mapambo, pembe.
- Udhibiti madhubuti wa magonjwa mbalimbali.
- Ng’ombe pia hutupatia mbolea ya samadi ambayo ni muhimu sana katika kilimo hai.
Ili ng’ombe akue vizuri, atoe maziwa mengi na awe na afya nzuri zingatia haya;
- Hakikisha unafanya uchaguzi mzuri wa ng’ombe wa kufuga.
- Apate malisho mazuri tangia akiwa ndama na banda liwe zuri na bora.
Chakula
Chakula ni kitu muhimu sana kwa mifugo yote. Ulishaji wa ng’ombe wa maziwa na wengine huanzia toka anapozaliwa (ndama) na ndipo atakapokuwa na mafanikio mazuri katika uzalishaji.
Ndama anapozaliwa tu anahitaji kupata maziwa ya kwanza (colostrum) kwa muda usiopungua siku tatu mfululizo. Maziwa haya humsaidia kujikinga na magonjwa na pia humpatia ndama virutubisho vya kutosha. Baada ya hapo ndama aendelee kunywa maziwa ya mama mpaka atakapofikia mwezi mmoja, aanze kupatiwa chakula cha ziada (pumba ya mahindi iliyochanganywa na mashudu pamoja na majani mabichi yaliyokatwa katwa vipande vidogo vidogo).
Ndama akifikia umri kati ya miezi miwili na sita unaweza kumuachisha kunyonya, na anatakiwa apatiwe chakula chenye virutubisho sawa na maziwa ya mama.
Kwa mfano apatiwe pumba za mahindi zilizochanganywa na mashudu na majani mabichi (apatiwe wakati wote).
Ngombe jike wa kisasa hufikia umri wa kupandwa akiwa na mwaka mmoja na nusu. Ng’ombe atakapokuwa na mimba ya miezi 7 kama alikuwa anakamuliwa anatakiwa kukaushwa na kupatiwa chakula chenye virutubisho zaidi.
Banda
Nyumba ni muhimu katika ufugaji wa ng’ombe. Tunashauriwa kuwahifadhi ng’ombe katika banda lenye hewa ya kutosha, lisilo na joto kali, lisilopitisha maji ya mvua na liwe lenye nafasi ya kutosha.
Pia banda la ng’ombe liwe na sakafu yenye mteremko kidogo kurahisisha usafi wa banda na kuzuia kutuama kwa maji na mkojo.
Nyumba ya ng’ombe inatakiwa iwe safi wakati wowote ili kuzuia magonjwa mbalimbali.