- Mifugo

Namna bora ya kupambana na maambukizi ya minyoo bapa (Trematodes) kwa mifugo

Sambaza chapisho hili

Aina hii ya minyoo imeripotiwa na wataalamu mbalimbali nchini Tanzania na mahali kwingine duniani kusababisha madhara makubwa kwa mifugo yanayosababisha upotevu mkubwa wa kiuchumi.

Minyoo bapa ni minyoo yenye urefu wa kuanzia midogo milimita moja hadi mirefu ya milimita 7.

Kinachowatambulisha kwa urahisi ni uwepo wa vifyonzeo vya damu viwili, kimoja kikiwa karibu kabisa na mdomo na kingine kikiwa upande wa ubavuni mwa mnyoo.

Minyoo bapa ipo katika kundi kubwa. Iliyopo  nchini ni Tanzania ni pamoja na Fasciola gigantica, Fasciola hepatica, Paramphstomes, Schistosoma bovis na Dicrocoelium hopes.

Tafiti ambazo zimefanyika Tanzania kwa kukusanya sampuli toka kwenye machinjio zinaonyesha kuwa, minyoo bapa ipo kwa wingi ukanda wa nyanda za juu kusini, ukanda wa kaskazini, ukanda wa Ziwa Viktoria na ukanda wa mashariki.

Utafiti uliowahi kufanywa na Nzalawahe toka SUA katika wilaya ya Arumeru, umebaini uwepo wa minyoo bapa kwa ng’ombe.

Utafiti umeonyesha uhusiano wa moja kwa moja wa kilimo cha umwagiliaji na maambukizi ya minyoo bapa kwa ng’ombe wanaofugwa katika maeneo hayo.

Pia katika utafiti huo wa Nzawalahe na wenzake, imebainika uwepo wa minyoo bapa kwenye konokono waliokusanywa toka mifereji ya umwagiliaji na maeneo ya kilimo cha mpunga kwenye vijiji vinavyofanya umwagiliaji.

Kilimo cha umwagiliaji kinatoa mazingira mazuri kwa konokono wanaoishi na minyoo bapa katika hatua ya kati ya ukuaji.

Kiwango kikubwa cha maambukizi kwa konokono hutokea katika kipindi cha mpito kutoka kipindi cha mvua kwenda kipindi cha kiangazi.

Maambukizi kwa mifugo huanza kutokea mwishoni mwa kipindi cha mvua na huwa kwa wingi katika kipindi cha kiangazi. Hii inatokana na uwepo wa malisho mazuri maeneo yenye maji, unyevunyevu, mwingi na mifereji ya umwagiliaji ambako mifugo hupenda kwenda kutafuta malisho.

Kwasababu hiyo, uelewewa mzuri wa wafugaji wa kufahamu namna ya maambukizi ya minyoo bapa kwenye mifugo yao unavyotokeo ungewezesha kwa kiasi kikubwa kuzuia maambukizi ya minyoo bapa.

Wakulima kuacha kilimo cha umwagiliaji kwa kipindi muafaka wakati wa kiangazi hasa punde tu wanapovuna mazao yao kingesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ongezeko la konokono.

Aidha kwa wale wanaofanya ufugaji wa ndani (wa kukatia malisho) wanatakiwa kujua maeneo yasiyo na minyoo bapa kwa kuangalia uwepo wa konokono kama kiashiri cha uwepo wa minyoo bapa.

Njia nzuri ya uhakika ni kulima na kuzalisha malisho yao wenyewe ili kuwa na uhakika wa kupata malisho yasiyo na minyoo bapa.

Mzunguko wa maisha ya minyoo bapa

Minyoo bapa hukua na kuwa minyoo mikubwa kwenye mirija ya nyongo ya mfugo ulio na maambukizi. Mnyoo mkubwa huanza kutoa mayai machanga kupitia kinyesi cha mnyama mwenye maambukizi na sehemu ya maisha inayobaki hutokea kwenye maji yasiyo na chumvi.

Baada ya wiki kadhaa, mayai huanguliwa na kutoa umbo la mwanzo la mnyoo bapa ujulikanao kitaalamu kama Miracidium ambao humwingia konokono.

Yakiwepo mazingira rafiki, mchakato wa ukuaji ndani ya konokono na kuwa umbo jingine lijulikanalo kama Cercaria hutumia ndani ya wiki 5 hadi 7 kisha hutolewa na kuingia ndani ya maji karibu na alipo konokono.

Cercaria hao hupoteza mikia yao wakati wa kubadilisha umbo lao kwenda umbo jingine lijulikanalo kama Metacercaria.

Hili ndilo umbo ambukizi la lava ambao wakiwa ndani ya maji huwa kwenye miti maji na gamba lao la nje ni gumu ukilinganisha na lile la cercaria linalowafanya wawe na uwezo wa kuishi muda mrefu kwenye maeneo yenye unyevu.

Hatua za mzunguko wa maisha ya minyoo bapa

  • Mayai changa ya minyoo bapa hutagwa kwenye mirija ya nyongo na hupatikana kwenye kinyesi.
  • Mayai huwa na kiinitete kikiwa katika hatua za mwanzo ndani ya maji.
  • Mayai hutoa Miracidia.
  • Miracidia humuingia konokono. Miracidia ikiwa ndani ya konokono hupitia pia hatua kadhaa za ukuaji Sporocysts, Rediae na Cercariae.
  • Cercariae hutolewa kutoka kwenye konokono na hujibadilisha na kuwa Metacercariae kwenye mimea maji au sehemu nyingine.
  • Wanyama hupata maambukizi kwa kula mimea (nyasi, majani) yenye Metacercariae. Binadamu pia hupata minyoo bapa kwa kula mimea maji yenye Metacercariae.
  • Baada ya kula mimea yenye Metacercariae, Metacercariae huenda kwenye utumbo mwembamba (duodenum) na hubadili umbo kwa kutoa gamba la nje.
  • Hapo huanza safari yake kwa kupitia kuta za utumbo mwembamba, ndani ya peritonia na kisha kufika kwenye ini na kuingia kwenye mirija ya nyongo ambapo hukua na kuwa mnyoo bapa mkubwa. Hapa ndipo makazi ya kudumu ya mnyoo bapa mkubwa ambapo hutaga mayai pia.

Madhara ya minyoo bapa

Minyoo bapa wakiwa kwenye ini huharibu ini na kusababisha maini mengi kukataliwa na wataalamu wa mifugo kwenye machinjio.

Lakini pia minyoo bapa husababisha upungufu wa uzito kwa mifugo na kufanya bei kuwa chini.

Kupambana na maambukizi ya minyoo bapa

Upambanaji wa maambukizi ya minyoo bapa hufanyika kwa kiasi kikubwa kwa kutumia madawa (flukicides) kwa lengo la kutibu au kuzuia maambukizi.

Tafiti zinaonesha kuwa uzuiaji wa kuenea kwa konokono haufanyiki na hivyo kufanya kazi ya kupambana na minyoo bapa kuwa ngumu na isiyo na ufanisi.

Inashauriwa kuwa ili upambanaji huu uwe na tija tiba ya minyoo bapa na uzuiaji wa maambukizi kwa kutumia dawa halisi uendane sambamba na utokomezaji wa konokono.

Mifugo ipewe dawa nzuri ya kuua minyoo bapa mwishoni mwa mvua (mwezi wanne na wa tano) ikifuatiwa na matibabu katikati ya kiangazi (mwezi wa tisa au wa kumi), na matibabu ya mwisho yafanyike mwanzoni mwa mvua (Disemba au Januari).

Uzuiaji wa minyoo

Minyoo ya ndani ya mwili, hasa ile inayoishi kwenye maini pamoja na ile ya mviringo huathiri sana afya za wanyama wa dogo kama ndama. Kwa ujumla husababisha udhaifu wa mwili, ukosefu wa nguvu, ukuaji duni na hatimaye vifo vya maelfu ya mifugo ya wafugaji wadogowadogo kila mwaka.

Hali hii ni ya kusikitisha kwasababu mifugo hiyo ingeweza kuokolewa kwa kutumia njia rahisi zinazoeleweka kama matibabu ya mara kwa mara kwa ajili ya kutokomeza minyoo hiyo kwa kutumia dawa za minyoo zinazofaa kufuatana na eneo la mfugaji.

Ni muhimu sana kulisha mifugo malisho yaliyo safi kwenye mahori safi ambapo ndama au wanyama wengine watashindwa kuyakanyaga na kuyachafua.

Kwa kuzingatia swala hili kila siku kutasadia kuzuia maambukizi ya minyoo kwa mifugo.

Iwapo mifugo inatunzwa kwa kuchungwa, ni vyema kugawa eneo la kuchungia katika sehemu ndogondogo na kuichunga mifugo hiyo kwa mzunguko.

Wanyama wataruhusiwa kuingia kwa kujilisha katika sehemu moja tu ya eneo hilo kwa kipindi cha muda fulani na malisho yatakapopungua katika sehemu hiyo ndipo watakapohamishiwa katika sehemu inayofuata ya malisho katika eneo hilo.

Kila sehemu ya eneo hilo la malisho lililotengwa linafaa kupumzishwa kwa kipindi cha angalau wiki 6 kabla ya kuruhusu tena wanyama kuingia na kujilisha. Kwa kufanya hivyo utaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa mifugo yako kuambukizwa minyoo kwa urahisi kutokana na malisho kuwa safi kwa kiasi kikubwa.

Wanyama pia waletewe maji nyumbani kuliko kuwapeleka kunywa maji lamboni kutokana na sababu kuwa maeneo wanakopelekwa kunywa maji yanaweza kuwa na minyoo hasa ile kwenye maini au mayai yake na hivyo mifugo hiyo kuambukizwa.

Nji ya pekee na nzuri zaidi ya kutosha kupambana na minyoo ni kuwapa mifugo dawa za minyoo mara kwa mara.

Baadhi ya dawa hizo hutolewa kwa njia ya sindano, nyingine zikiwa na uwezo wa kuangamiza minyoo ya aina nyingi na nyingine zikiwa ni maalumu kwa ajili ya aina fulani tu za minyoo.

Muhimu

Ili kukinga wanyama kuambukizwa magonjwa mbalimbali ni muhimu kwa mfugaji kuzingatia yafuatayo;

  • Kuwa na banda safi lililojengwa kwa mpango mzuri pamoja na mazingira yaliyo safi.
  • Kutunza ndama kwa usahihi tangu akiwa mdogo mpaka anapokuwa amefikisha umri mkubwa wa kupanda.
  • Kuchukua tahadhari stahiki kabla, wakati na baada ya kuzaa na kuzingatia mbinu sahihi za ukamuaji.
  • Kulisha mifugo lishe bora na ya kutosha kila wakati na kupandisha kwa njia ya chupa au mrija.
  • Kuwa karibu na wanyama wakati wote na kuwachunguza ili kutambua dalili ama tatizo la magonjwa.

Makala hii ni sehemu ya utafiti uliofanywa na watafiti kutoka SUA. Kwa mawasiliano zaidi, unaweza kuwasiliana na mtaalamu wa mifugo Augustino Chengula kutoka SUA kwa simu namba +255767605098

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *