- Mifugo

Mfugaji mashuhuri wa kuku wa kienyeji Singida

Sambaza chapisho hili

Kama ilivyo ada, Mkulima Mbunifu tumekuwa tukikufikishia taarifa toka kwa wakulima katika mikoa mbalimbali hapa nchini wanaojishughulisha na kilimo ikolojia nia yetu ikiwa ni kuwawezesha wakulima wengine kujionea na kujifunza ni kwa namna gani wakulima wenzao wameweza kufanikiwa katika kilimo ikolojia.

Miongoni mwa wakulima waliopata fursa ya kutembelewa na kuhojiwa na jarida hili ni mfugaji toka mkoani Singida ambaye anajishughulisha na ufugaji wa kuku wa asili kwa misingi ya kilimo ikolojia jambo ambalo anasema laiti angelifahamu mapema angeshafika mbali sana katika ufugaji.

‘’Kwa majina naitwa Madai Njovu, naishi Unyangwe, kata ya Iseke, Ikungi mkoani Singida. Ninajishughulisha na uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa misingi ya kilimo ikolojia pamoja na ufugaji wa kuku wa asili”.

‘’Shughuli za kilimo na ufugaji nimekuwa nikizifanya toka utotoni kwani kilimo ni asili yetu lakini ndani ya miaka kumi iliyopita nimefanikiwa kufanya vizuri katika ufugaji wa kuku wa kienyeji na hii ni baada ya kupata elimu ya kilimo ikolojia toka shirika la Farm Radio Internationala kupitia vipindi vyake vya kiikolojia katika radio ya standard’’.

Hayo ni maneno ya mkulima huyu ambaye amekuwa mfano mzuri kwa wakulima na wafugaji wengine mkoani Singida na ameweza kupiga hatua kubwa katika ufugaji wa kuku wa asili ambapo anasema tofauti na miradi mingine anayofanya ya kilimo ufugaji wa kuku nachukua asilimi 70 ya miradi yote.

Kuhusu kuku wa kienyeji

Bw. Njovu anaeleza kuwa kwa asili alikuwa akifuga kuku wa asili lakini hakuwa akitilia maanani kama kilimobiashara kwani alikua akiona kuku wakifugwa tu kama mtindo wa kawaida wa maisha. Lakini anasemakuwa, toka apate elimu ya kilimo ikolojia kupitia FRI kwa miaka kumi sasa ameweza kupiga hatua kubwa sana na ni mfugaji mkubwa anayezalisha mpaka kuku 300 kwa mwezi na kwa kila mwezi huhakikisha kuwa banda lake lina kuku 200 (hii ni kutokana na kuzalisha vifaranga kila mara).

Anasema kuwa “Baada ya kuona faida iliyoko katika ufugaji wa kuku wa asili kwa misingi ya kiikolojia ikiwa ni pamoja na gharama ndogo za uzalishaji, uleleaji mzuri wa vifaranga, ustahimilivu wa mabadiliko ya hali ya hewa na magonjwa, utagaji mzuri, chanzo cha kipato na uhitaji mkubwa wa bidhaa za nyama na mayai sokoni niliamu kufanya kwa ukubwa zaidi na mpaka sasa najivunia maamuzi yangu”.

Shughuli zingine za uzalishaji

Katika uzalishaji wa mazao, ninajishughulisha na uzalishaji wa mahindi, mtama na uwele ambapo mazao yote nazalisha kwa misingi ya kilimo ikolojia bila kutumia kemikali sumu zozote za viwandani.

Natumia mbegu za asili, mbolea ya asili kama samadi, dawa za asili kupambana na magonjwa, matandazo kulinda rutuba na unyevu ardhini, sikwatui ardhi na nafanya kilimo mesto.

Soko

Bidhaa za kilimo ikolojia zinajiuza zenyewe hivyo soko la bidhaa zangu zote za kilimo na za ufugaji Napata kwa haraka sana kulingana na nini nazalisha na napeleka sokoni au kwa mlaji moja kwa moja bila kupitia kwa madalali. Kwa upande wa kuku, majoo nauza kwa 20,000/= tetea anayetaga 17,000/= tetea anayeeleka kutaga 15,000/= na vifaranga wa miezi 3 elfu 10,000/=

Faida kiuchumi

Nimeweza kusomesha watoto mpaka elimu ya juu, familia yangu inapata kipato cha kutosha kujikimu kula na kuvaa vizuri, lakini pia nazidi kupanua mradi wa ufugaji wa kuku ili niweze kuzalisha kwa wingi zaidi kwani napata wateja karibu mikoa yote.

Changamoto

Changamoto kubwa anayopata Bw. Njovu ni ugonjwa wa kideri ambao mara nyingi ndiyo ugonjwa pekee ambao ukisha kuku unasumbua kidogo, alisema.

 

Ushauri kwa wakulima/ wafugaji

Nawashauri wafugaji wajikite katika ufugaji wa kuku wa asili kwani unalipa sana na soko lake ni kubwa. Aidha wakulima wajikite katika kilimo kwa misingi ya kilimo ikolojia na waachane na kilimo cha kisasa mabcho kinategemea sumu za viwandani kuzalisha na baaye sumu hizo kuleta mdahara kwa binadamu, Wanyama, mime ana mazingira.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *