- Mifugo

Mbinu za asili zinazofaa katika kilimo ikolojia

Sambaza chapisho hili

Ili kutekeleza utunzaji asilia wa mazao ni muhimu sana kuelewa mbinu asilia za kufanikisha kilimo. Kwa hali hiyo matukio na majanga ya kushambuliwa na wadudu waharibifu yanaweza kupunguzwa na utumiaji wa hatua za utunzaji wa mazao.

Miongoni mwa mbini zinazoweza kutumika katika utunzaji wa mazao kwa njia za asili ni pamoja na;

  1. Kuelewa mfumo wa uhusiano wa viumbe na mazingira ya kilimo

Aina za wadudu waharibifu na wadudu na wadudu wenye manufaa katika shamba lililolimwa na katika eneo la jirani.

  • Bayolojia ya wadudu waharibifu, magonjwa na wadudu wenye manufaa. Hii ni pamoja na maumbile, mzunguko wa maisha, tabia ya kuzaliana, tabia za kula, na mengineyo.
  • Utaratibu unaojirudia wa wadudu, katika misimu mbalimbali na kutegemea kwao hali ya mazingira.
  • Aina ya madhara wakati wa mzunguko wa maisha ya wadudu yatakayosaidia katika mbinu zaidi za kuwadhibiti vizuri.
  • Msimu au hatua ya ukuaji wa mmea shambani ambapo ni hatari zaidi kushambuliwa na wadudu.
  • Mimea mingine inayolimwa au mingine ya porini, inayowavutia wadudu maalumu waharibifu.
  • Wadudu marafiki au vimelea wanaoweza kutumiwa kuwala wadudu hao waharibifu.
  1. Kilimo mchanganyiko

Mazao ya aina mbalimbali yanayolimwa sambamba na maua au mimea ya porini yatasababisha yatasababisha mfumo wa aina tofauti utakaosaidia kuwepo kwa maskani na chakula kwa aina mbalimbali za ndege, wadudu na wanyama watambaao(Jamii ya mijusi), ambao pia hupunguza aina Fulani ya wadudu waharibifu wa mazao.

  1. Hali ya ardhi

Maeneo yasiyolimwa kama vile miteremko mikali ya milima, maeneo yasiyofikika au yaliyozungushiwa mimea ni maskani mazuri kwa ndege, wadudu na wanyama watambaao (jamii ya mijusi) wanaowinda wadudu waharibifu.

  1. Kubadilisha na kuchanganya mazao

Madhumuni makubwa ya kubadili mazao ni kutenganisha aina fulaniya wadudu waharibifu wa mazao fulani, ambao kukosekana kwa zao hilo huwafanya wahame au kufa kwa kipindi hicho.

Ni vizuri kubadilisha mazao ambayo si ya jamii moja. Katika msimu unaofuata, yaani mazao yanayoshambuliwa zaidi na wadudu fulani, sharti yabadilishwe na yale ambayo mdudu huyo hayapendelei.

Kwa mfano, ili kuzuia bungu wa mahindi, ni vizuri baada ya kuvuna mahindi msimu unaofuata maharagwe yaoteshwe.  Hali hii huharibu mzunguko wa maisha ya bungua wa mahindi. Ni vizuri pia kuchanganya mazao ili kupunguza mashambulizi ya wadudu.

  1. Matukio asilia yanayojirudia na wakati muafaka wa kupanda

Kuchagua wakati muafaka wa kupanda kunaweza kupunguza mashambulizi. Kufahamu mzunguko wa maisha ya wadudu na mahusiano yake katika mazao yanayoshambuliwa humrahisishia mkulima kuchagua muda wa kupanda. Kutokana na hili, mkulima anaweza kupanda mapema au kuchelewa kupanda, ili kuepuka kipindi ambacho wadudu huzaliana kwa wingi.

Kwa mfano; Nyanya zilizopandwa wakati wa kiangazi, hazipati magonjwa ya ukungu kwani hakuna maji ya kuzidi kiasi yanayolowanisha majani ili kuwezesha vimelea vya ukungu kuota. Mfano; Msimu wa kwanza wa kilimo: Mboga za majani kama mchicha, chainizi, kabichi n.k Msimu wa pili wa kilimo: Mboga za matunda kama nyanya, bamia, bilinganya, n.k Msimu wa tatu wa kilimo: Mazao ya mizizi kama viazi vitamu, viazi mviringo, mihogo n.k Msimu wa nne wa mazao: Jamii ya mikunde, maharagwe, kunde, mbaazi, n.k

  1. Mbolea na afya ya mimea

Mimea yenye afya nzuri zaidi hustahimili athari iletwayo na magonjwa na wadudu waharibifu na kutoa mavuno mengi. Mbolea huwa na wadudu marafiki ambao hurutubisha ardhi.

  1. Ulimaji ardhi

Utifuaji wa ardhi kwa jembe la kukokotwa na ng’ombe au trekta una lengo la kuuairisha funza na hatua nyingine ya kukua kwa wadudu waharibifu waliobaki ardhini au kwenye mabua ya mazao. Kwa kuwachimbua wataunguzwa na jua na kuliwa na wanyama na ndege. Mabaki ya mazao hufukiwa na hivyo kukutana na viumbe wa ardhini au unyevunyevu ambao huyaozesha na kurutubisha ardhi.

  1. Uteuzi wa aina bora ya mbegu

Uteuzi wa aina ya mbegu inayostahimili wadudu au magonjwa, husababisha wadudu waharibifu na magonjwa kushindwa kuzaliana.

  1. Usafi wa shamba

Usafi wa shamba husaidia kuharibu mzunguko wa maisha ya wadudu waharibifu, wadudu waharibifu kukosa maskani.

  1. Kupanda kwa nafasi

Kupunguza kivuli, kupunguza matawi, kuondoa maotea na kushikilia mimea kwa miti ili isilale ardhini. Matendo yote haya husababisha mazingira yasiwe mazuri kwa maendeleo ya vimelea vya magonjwa na wale wadudu waharibifu wapendao kuishi kwenye hali ya kivuli.

  1. Masuala ya kijamii Utunzaji wa mimea ni jukumu la jamii nzima

Mkulima binafsi hawezi kamwe kuchukua hatua zinazofaa kupambana na wadudu waharibifu wanaoenea sehemu kubwa mwenyewe. Hapa ni mahali pazuri pa kufikiria kushirikiana na majirani, ili kuchukua hatua ya pamoja kukabilina na janga la wadudu.

Iwapo hatua za kudhibiti wadudu zitatumiwa baadhi ya mambo ya msingi hayana budi kuzingatiwa:

  • Kuondolewa au kukomeshwa kabisa kwa wadudu waharibifu wa mazao si jambo zuri. Matokeo au athari zake zisizo dhahiri katika mahusiano ya chakula ni mabaya kwa ujumla na hayawezi kamwe kufidiwa na wingi wa mavuno.
  • Kutumiwa mara kwa mara kwa madawa ya sumu yanayoua ovyo aina mbalimbali za viumbe, husababisha uharibifu wa mazingira. Rutuba ya udongo inaweza kupungua kwa ajili ya upungufu wa viumbe hai ardhini na haina budi kurudishwa kwa hali yoyote ile. Uzalishaji wa baadhi ya mimea hauwezekani au hupungua kutokana na kutokuwepo kwa wadudu wanaochavusha.
  • Wanyama wanaokula au kuwinda wadudu waharibifu wa mazao nao wanatoweka.
  • Kutokomezwa kwa wadudu waharibifu na kutumika mara kwa mara madawa ya sumu kunasababisha ongezeko la kukosekana uwiano wa mahusiano ya chakula. Matatizo hayo yanaweza kutokomezwa kwa kutumia gharama kubwa za kununulia aina mpya ya madawa ya kuulia wadudu waharibifu.

Katika hali ya namna hiyo ina maana kwamba wakulima watatengeneza zaidi mashirika na viwanda hatarishi kwa usalama wa afya ya binadamu, mimea na wanyama. Usinyunyize dawa endapo hakuna tatizo.

Baada ya kipindi Fulani, wadudu waharibifu wa mazao wanakuwa sugu kutokana na dawa zinazotumiwa dhidi yao. Iwapo hatua hiyo itafikiwa, wataendelea kuzaliana kwa wingi zaidi kuliko mwanzo.

Ongezeko hili la idadi lina maana kwamba adui asilia wa wadudu waharibifu yaani wanyama au wadudu wanaowashambulia (wadudu rafiki) hawakuzoea sumu ya kuulia wadudu au wote wamekufa.

Inapotokea hali ya namna hiyo, wakulima hawana budi kutafuta aina nyingine ya dawa inayoweza kuua wadudu waharibifu, jambo ambalo ni hatari kwa sababu wakulima hugeuka kuwa wategemezi wakubwa wa sumu za kemikali.

Kwa kawaida mbinu za udhibiti zinazofaa zaidi ni zile za asili ambazo zinaendana na maumbilie na mazingira.

Kila aina ya mmea unaolimwa una idadi fulani ndogo ya wadudu wanaoweza kusababisha uharibifu na kusababisha wasiwasi. Kwa upande wa mkulima anaweza kuwa na kiasi kikubwa cha msaada wa asilia, katika kupambana na wadudu waharibifu. Ni muhimu sana kutokuwaua viumbe rafiki.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *