- mbuzi, Mifugo, Ng'ombe

Matatizo yanayoweza kumpata ng’ombe baada ya kuzaa

Sambaza chapisho hili

Mara nyingine ng’ombe anapozaa, huweza kupatwa na matatizo machache kama vile kizazi kutoka nje, kondo la nyuma kushindwa kutoka na hata wakati mwingine kupooza miguu na kushindwa kusimama.

Kushindwa kutoka kwa kondo la nyuma

Kwa kawaida mara baada ya kuzaa, kondo la nyuma pamoja na majimaji yaliyobakia kwenye tumbo la uzazi hutolewa nje kutokana na msukumo wa misuli ya tumbo. Kondo la nyuma linaweza kutoka baada ya muda mfupi tu tangu ng’ombe azae na likishatoka inategemewa kuwa hali ya ng’ombe itaendelea kuwa vizuri.

Nini cha kufanya

Ikiwa kondo litabakia kwenye tumbo la uzazi au likatoka kiasi na kuning’inia, msaada wa kuliondoa kabisa unaweza kuhitajika. Ikiwa kondo la nyuma litaning’inia hadi kwenye sakafu, funga sehemu ile inayoning’inia kuanzia kwenye goti la ng’ombe ili kondo hilo lisiwe linaburuzwa ovyo kwenye sakafu.

Usilifungie tofali au kipande cha mti kwasababu ukifanya hivyo, vitu hivyo ulivyofungia vinaweza kujishika mahali na kusababisha kondo kukatika mahali pasipotakiwa na tena kukiwa bado mapema mno.

Ikiwa kuna matatizo ya namna hiyo kwenye utoaji wa kondo la nyuma, basi mtaalamu wa mifugo anahitajika kuitwa ili aweze kuliondoa kondo hilo kwa muda mfupi baada ya ng’ombe kuzaa.

Lisipotoka kwa muda wa siku tatu kuna tatizo?

Hata hivyo, kondo la nyuma linaweza kubakia na kuendelea kuning’inia kwa muda wa siku mpaka tatu kabla halijatoka lenyewe, kwa maana hiyo ng’ombe anaweza kukaa nalo kwa muda wa siku tatu bila kupata msaada wowote wa mtaalamu na likatoka.

Kwa kipindi hicho cha siku tatu, ng’ombe hataweza kupata madhara makubwa kutokana na kubakia kwa kondo hilo. Muda wa siku tatu unapotimia bila kondo la nyuma kutoka, ni muhimu sana mtaalamu wa mifugo akataarifiwa ili atoe msaada wa kulitoa kondo hilo.

Kwa kawaida mtaalamu wa mifugo atajaribu kulitoa kondo lote kwa utaratibu na kisha kuweka kidonge kilichotengenezwa maalumu kwa matumizi hayo (pessary) ili kuzuia ambukizo lolote la ugonjwa linaloweza kutokea.

Tahadhari

Kamwe mfugaji mwenyewe asijaribu kulitoa kondo la nyuma kwani hana utaalamu wowote wa kufanya hivyo, mtaalamu pekee ndiye anayetakiwa kufanya kazi hiyo.

Nifanyaje endapo kizazi kitatoka nje?

Mara nyingine baada ya kuzaa kwa shida, baadhi ya ng’ombe huendelea kusukuma wakitarajia kukitoa nje chochote kilichopo kwenye kizazi.

Kwa bahati mbaya kutokana na kusukuma huko kupita kiasi, sehemu au njia yote ya uzazi huweza kutoka nje.

Hali hii hutokea zaidi kwa ng’ombe ambao wakati walipokuwa wakizaa walilala kwenye sakafu isiyokuwa na usawa unaolingana, yaani upande mmoja kunyanyuka kuliko mwingine. Pamoja na hayo, baadhi ya ng’ombe hukumbwa na matatizo hayo zaidi kuliko wengine.

Iwapo kizazi kilichotoka nje ya mwili wa ng’ombe hakitarudishwa ndani mapema kikiwa katika hali ya usafi, maisha ya ng’ombe yatakuwa hatarini kwani anaweza kufa katika kipindi cha masaa machache kutokana na mshtuko.

Nini cha kufanya

Ikiwa kizazi kimetoka nje, mtaalamu aitwe ili asaidie kukirudisha ndani kwa utaratibu unaofaa. Mtaalamu asafishe kizazi kilichotoka nje kwa maji mengi yaliyo safi na baridi, na ikiwa kizazi hicho kimevimba uvimbe huo unaweza kupunguzwa haraka kwa kukitumbukiza kwenye maji yaliyotiwa sukari na kukorogwa vizuri.

Baada ya kufanya hivyo, kwa uangalifu huku akichukua tahadhari kisikatike ama kisumie, atakisukuma kizazi ndani kidogokidogo mpaka kitakapoingia chote.

Kama kutakuwa na sehemu ya kondo la nyuma ambazo bado zimejishika kwenye kizazi hicho, basi ataweza kuziondoa kwanza ili zisirudi tena ndani ya tumbo.

Baada ya kukirudisha kizazi ndani, ng’ombe atibiwe kwa antibiotic ili kuzuia uwezekano wa kuugua kwasababu ugonjwa wa aina fulani unaweza ukawa umeingizwa mwilini wakati wa zoezi la kukirudisha kizazi ndani.

Ikiwa urudishaji ndani wa kizazi utafanywa mapema, ni wazi kizazi hicho kitakuwa bado hakijavimba na kazi ya kukirudisha ndani itakuwa rahisi zaidi.

Nini kifanyike iwapo ataendelea kukisukuma kizazi nje?

  • Iwapo ng’ombe ataendelea kukisukuma, jambo ambalo mara nyingi hutokea, jaribu kumsimamisha au kumfanya aelekeze kichwa chake upande wa bondeni.
  • Jambo lingine   unaloweza kulifanya ni kumfunga kamba zaidi ya moja kuanzia shingoni kupitia chini ya miguu na halafu ulikoanzia na kisha kuzivuta hadi kwenye shingo na kufunga mafundo mengi kwenye sehemu ya nje ya uke. Kwa kufanya hivyo utasaidia kumzuia ng’ombe asisukume tena.
  • Mbinu nyingine inayoweza kutumika ili kumfanya ng’ombe asiendelee kusukuma ni kushona sehemu ya nje ya uke, na kazi hii ataifanya mtaalamu wa mifugo mwenyewe.

Utazuia vipi kutokea kwa tatizo hili?

  • Ili kuzuia kutokea kwa tatizo la namna hii, wakati wa kuzaa, ng’ombe awekwe kwenye sakafu iliyo na usawa uliolingana.
  • Ng’ombe akishazaa ndama na ukawa na uhakika kwamba hakuna ndama mwingine zaidi anayetegemewa kuzaliwa, mara tu baada ya ng’ombe kuzaa msimamishe.

Mbinu ya kumsimamisha ng’ombe mara tu baada ya kuzaa husaidia ng’ombe kutokumbwa na tatizo la kupooza kwa miguu ya nyuma kunakotokana na kuumia wakati wa kuzaa na hivyo kushindwa kabisa kusimama.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *