Watu wanaoishi kwa kutegemea vyakula vya kwenye maji huishi kwa muda mrefu na huwa na kumbukumbu nzuri na uwezo mkubwa wa kufikiri.
Katika matoleo kadha wa kadha ya jarida la MkM, tumekuwa tukieleza kwa ufasaha kabisa namna ya ufugaji bora wa samaki, na faida zake kiuchumi kwa mfugaji na jamii kwa ujumla.
Katika toleo hili, tumeona ni vyema kuwa na makala hii ambayo itaeleza kwa undani faida za kiafya zinazotokana na lishe ya samaki kwa wafugaji na jamii kwa ujumla.
Samaki ni nini?
Samaki ni wanyama wenye damu baridi wanaoishi kwenye maji ya mito, mabwawa, maziwa au bahari. Ni moja ya chakula ambacho katika ulaji wa kila siku tumekuwa tukitumia kama mboga, pia kama sehemu ya mchanganyiko katika kuandaa vyakula vya aina nyingine.
Kwanini muhimu kula samaki?
Siyo watu wengi wanaofahamu umuhimu wa kula samaki mara kwa mara na jinsi kitoweo hiki kilivyo na umuhimu wa kipekee katika afya ya binadamu.
Kitoweo hiki kinaelezwa kuwa na mafuta yenye kiambata aina ya Omega 3 yanayomfanya binadamu kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, kutunza kumbukumbu na kuishi kwa muda mrefu.
Vyakula vyote vinavyozalishwa majini huwa na kiambata aina ya Omega 3 yenye mafuta yanayotakiwa kwa mwili wa binadamu yatokanayo na samaki.
Mafuta hayo yana mbegu maalumu zinazomsaidia binadamu katika ukuaji ambazo pia ni maalumu kwa faida ya mfumo wa ubongo na neva.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa watu wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito mikubwa wamekuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, akili nyingi na wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu kutokana na kutokuzeeka mapema.
Umuhimu kwa wajawazito
Kina mama wajawazito wamekuwa wakipewa ushauri kutumia kitoweo hicho wawapo wajawazito na kuepuka nyama nyekundu ambayo hata hivyo ni muhimu kwa mama mjamzito kutumia ili kuongeza damu haraka.
Wajawazito wanapaswa kula samaki kwa wingi ili kukuza ubongo wa mtoto. Pia ni lazima wale nyama nyekundu ili kuongeza damu kwa uharaka mwilini ila tunawashauri isizidi nusu kilo kwa siku saba.
Samaki wana umuhimu katika afya ya mama na mtoto na iwapo mama hatapata Omega 3 ya kutosha anaongeza hatari ya kupata postpartum depression, mtoto mwenye uzito mdogo, uchungu wa mapema mtoto kuzaliwa kabla ya muda, au kulazimika kuzaa kwa upasuaji.Omega 3 inahitajika kwa kila binadamu ili kuendelea kuutunza ubongo na kujiepusha na magonjwa yanayotokana na kukosa madini haya.
Ni nini umuhimu wa Omega 3 kwa mtoto?
Omega 3 humsaidia mtoto kukuza ubongo, kutengeneza retina kwenye mboni ya macho na kutengeneza mfumo wa neva.
Pia humsaidia mama kuzuia matatizo kama kifafa cha mimba na sonona baada ya kujifungua. Njia kuu ya mtoto kupata Omega 3 ni kutokana na vyakula anavyokula mama yake.
Watoto ambao wamepata Omega 3 ya kutosha wameonesha kuwa na umakini mkubwa na upeo mzuri kuliko watoto wengine.
Pia, hukua kwa haraka zaidi kuliko yule ambaye hakupata kiambata hicho na huwa mtunzaji mzuri wa kumbukumbu.
Hupunguza matatizo ya kitabia, na kwa watu wazima hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na saratani nyinginezo.
Je, ni wakati gani tunahitaji kupata Omega 3?
Ni vizuri kupata Omega 3 ya kutosha kupitia mlo wa kila siku.
Wakati wa ujauzito mwanamke anashauriwa kupata angalau gramu 250 kila siku na katika kipindi cha mwisho (miezi mitatu ya mwisho) kwa sababu katika kipindi hiki mtoto hutumia asilimia 70 ya Omega 3 kujenga ubongo wake na mfumo wake wa neva.
Nini chanzo cha madini hayo?
Wataalamu wanaelezea vyanzo vinavyoleta madini hayo kuwa vinapatikana katika samaki na mafuta ya samaki, hasa samaki wenye mafuta mengi kama vibua, sato, salmon, sangara, dagaa, herring na jodari.
Aina ya vyakula vingine vyenye Omega 3
Vyanzo mbalimbali vya habari duniani vimewahi kuripoti kuwa wapo samaki ambao si wazuri sana kuwatumia, kwani wana sumu aina ya mercury kwa sababu ya machafuko ya kimazingira.
Kutokana na hilo unaweza pia ukapata Omega 3 kutoka kwenye mayai, mkate, juisi, mboga za majani, canola, alizeti, mafuta ya samaki na vyakula jamii ya mbegu.
Tahadhari: Kama utapenda kumeza vidonge vya Omega 3 uhakikishe kwamba havijatengenezwa na maini ya samaki kwani hizi zina asilimia kubwa ya retinol Vitamin A, ambayo imegundulika kusababisha madhara kwa watoto.
Omega 3 iliyotengenezwa kutoka kwa nyama ya samaki na siyo maini ni bora zaidi.
Kama huna uhakika ni bora kununua vidonge maalumu vya Omega 3 vilivyotengenezwa kwa ajili ya wajawazito.
Inaelezwa na wataalamu kuwa mafuta ya samaki yanaweza kuchanganywa katika vyakula vya mboga mboga ikiwemo za majani na hata katika kachumbari.
Ni muhimu kujumuisha mlo wa samaki au mafuta yake kwenye mlo wa kila siku endapo hauna aina nyingine ya chanzo cha Omega 3, na virutubisho vingine. Hii itasaidia kuujenga mwili na kupata faida kadha wa kadha kama ilivyoelezwa hapo awali.