Mahindi ni zao muhimu na tegemezi kwa jamii nyingi barani Afrika. Nchini Tanzania zao hili hulimwa mikoa yote kwani ni zao tegemezi kwa chakula. Hata hivyo, zao hili lina changamoto, kwani hushambuliwa na visumbufu mbalimbali vya mimea ikiwamo viwavijeshi vamizi (Fall armyworm).
Viwavi hawa hula sehemu zote za mmea majani, bua, mbegu, gunzi; pia hula aina nyingine za mimea. Umakini mkubwa unahitajika katika kuwadhibiti sababu huingia ndani ya bua na gunzi la mhindi.
Mdudu huyu amekuwa tatizo kubwa katika Nchi za Kusini Mashariki ya Asia, uangamizwaji umekuwa changamoto. Wakulima wengi wamepata hasara kutokana na uvamizi wa mdudu huyu, kwani si wote wanaweza kumudu gharama za kununua dawa kumuangamiza mdudu huyu.
Hatua za ukuaji na uharibifu
Mdudu huyu huanzia hatua ya mayai na ni vyema kuanza kupambana nae katika umri wa lava kama ufunguo wa kudhibiti mashambulizi yao shambani.
Mdudu huyu hukua na kugeuka Nondo (kipepeo), ambae hutaga mayai na muda wake wa kuishi ni siku 30 huku akiwa kama buu kwa siku 6.
Jike la Nondo hutaga mayai 200 hadi 250 kwa mara moja katika jani la mmea wa hindi. Katika maisha yake yote hutaga mayai yasiyo pungua 1,000 – 1,500.
Ndani ya siku 5 baada ya mayai kutagwa huanguliwa viwavi na kuanza kushambulia mahindi machanga. Viwavi hawa huwa wadogo na wenye rangi ya Kijani na huning’inia kwa utando wa nyuzi kama buibui ambao huwa na vichwa vyeusi na badae vichwa hivyo hubadilika na kuwa vya rangi ya chungwa (Orange) na mara ya tatu hugeuka na kuwa rangi ya kahawia. Katika hatua hii huanza kula katika sehemu ya chini ya mmea wakati.
Hatua inayofuata huanza kula sehemu ya juu ya mmea hasa katikati ya mmea na katika hatua hii huweza kutambulika kwa madoa manne meusi kwa nyuma, na umbile la ‘Y’ usoni iliyogeuka chini juu.
Baada ya muda mdudu huyu huanguka chini udongoni na kujizika mwenyewe katika udongo na huingia kiasi cha urefu wa sentimita 2.8 udongoni na huwa anageuka na kuwa pupa.
Baada ya siku saba (7) – kumi (10) hubadilika na kuwa Nondo na hii ndio hatua ya mwisho katika kukomaa.
Mdudu huyu hushambulia zaidi ya aina za mimea 80. Lakini hupendelea sana kula Mahindi, Mtama, Majani aina ya Bermuda, Solighum n.k.
Dalili za uharibifu wa mdudu huyu kwenye mahindi
Ishara za uharibifu wa mdudu huyu ni majani kuwa na madirisha madirisha – kwa kuwa lava mdogo huwa na urefu wa mm 1. Huanzia uharibifu wake katika kuyakwangua majani akiyala na kuacha utando mithili ya nailoni nyeupe ndipo anapoelekea sehemu ya kati ya mmea linapoanzia jani kuota yaani katikati ya jani changa na jipya.
Hivyo mara baada ya kubaini uvamizi wa mdudu yafaa kuwa makini haraka, tembelea shamba kwa mtindo wa ‘W’ ili kubaini mashambulizi kila mara.