- Mifugo

Baadhi ya lishe ya vyakula kwa ng’ombe wa maziwa

Sambaza chapisho hili

Ng’ombe wa maziwa anahitajika kulishwa aina ya vyakula vinavyoweza kuupatia mwili wake viinilishe vinavyohitajika kwa ajili ya ukuaji, nguvu, uzazi, pamoja na hifadhi ya viinilishe kama mafuta, protini, madini na majimaji.

Ng’ombe huhitaji viinilishe kwa ajili ya kutosheleza mambo yafuatayo;

  • Kuufanya mwili udumu katika hali yake ya kawaida, na kuweza kumudu mambo kadhaa muhimu kufanyika kwa ajili ya kudumisha uhai wake ambayo ni pamoja na mapigo ya moyo, kupumua, kutunza joto la mwili, uyeyushaji wa chakula, utoaji wa uchafu mwilini, mzunguko wa damu mwilini. Ili mnyama aweze kuendelea kuishi ni sharti mambo hayo yote yafanyike mwilini mwake hata kama atakuwa amepumzika.
  • Kukua, kujengeka kwa mifupa, nyama, mafuta na vitu vingine muhimu mwilini mwake.
  • Viinilishe pia huwezesha utengenezaji wa maziwa kwa ng’ombe anayekamuliwa.
  • Pia, husaidia katika ukuaji wa ndama tumboni na kuzaa salama kwa ng’ombe mwenye mimba.

Zifuatazo ni baadhi ya viinilishe anavyotakiwa kupatiwa ng’ombe wa maziwa;

Chakula cha Ng’ombe wa maziwa

Dairy meal ni chakula maalumu cha kusindika cha ng’ombe wa maziwa ambayo hutengenezwa kutokana na mchanganyiko wa vyakula vinavyoweza kuwekwa katika makundi makuu matatu ambayo ni;

  • Vyakula vyenye uwezo mkubwa wa kutia mwili nguvu na joto kama vile pumba za nafaka aina ya mahindi, ngano, na mpunga (asilimia 60% hadi 70%).
  • Vyakula vyenye uwezo wa kujenga mwili kama vile mashudu ya mbegu za mimea inayotoa mafuta kama vile pamba, alizeti, ufuta, maharagwe (asilimia 25% hadi 35%.
  • Vyakula vyenye mchanganyiko wa madini pamoja na chumvi (asilimia 4% hadi 5%).

Madini na chumvi

Kutegemeana na ukubwa wa mnyama na aina ya chakula kinacholishwa kwa siku, mnyama anaweza kuhitaji kiasi cha gramu 10 hadi 50 za madini kwa siku ili kutosheleza mahitaji yake ya mwili.

Baadhi ya vyakula huwa na kiasi kikubwa cha madini kuliko vingine huku lita 10 za maziwa zikiwa na gramu zipatazo 100 za madini. Iwapo ng’ombe atashindwa kupata kiasi cha gramu 100 za madini kutoka katika chakula alicholishwa kwa siku, atalazimika kutumia madini ya ziada kutoka mwilini mwake ili kutengeneza maziwa.

Baadhi ya wafugaji hulisha mifugo yao mchanganyiko wa madini ulioko katika hali ya unga pamoja na chumvi na wanyama huruhusiwa kujipatia mchanganyiko huo kwa kadri wanavyotaka na siyo kawaida kwa mnyama kutumia madini mengi zaidi kuliko mwili wake unavyohitaji.

Namna ya kutengeneza mchanganyiko wa madini

Ikiwa unaweza kupata chumvi ya kawaida, madini yaliyoko katika hali ya unga kama vile chokaa, basi unaweza kujitengenezea mwenyewe mchanganyiko wa madini kwa ajili ya mifugo.

Mchanganyiko huo wa madini utakuwa na gharama nafuu zaidi na utaweza kulisha kati ya gramu 20 hadi 100 kwa siku kwa ng’ombe wa umri wowote.

Pili, kama huwezi kupata mchanganyiko huo, basi unaweza ukatafuta fosifeti na kuichanganya na mifupa iliyosagwa vizuri pamoja na chumvi (ikiwezekana upate chumvi yenye iodine).

Tatu, ikiwa njia zote mbili hapo juu utazishindwa basi unaweza kuchanganya chumvi na mifupa iliyosagwa pekee na kulisha ng’ombe kila siku.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *