Afya ya mifugo ni tatizo kubwa linalowakabili wafugaji walio wengi katika sehemu mbalimbali za nchi. Wapo wataalamu mbalimbali katika maeneo na mikoa yote ya nchi wanaotoa huduma ya mifugo lakini, bado kuna changamoto nyingi zinazowakumba wafugaji.
Katika sehemu ambazo mawasiliano na miundo mbinu ni duni, wafugaji wamekuwa wakipoteza mifugo kutokana na sababu kuwa mara ugonjwa unapoikumba inakuwa si rahisi kufikiwa na mtaalamu kwa wakati hivyo kusababisha mifugo kufa.
Huduma za kisasa za kitabibu pia kuonekana ni aghali katika maeneo machache hivyo wafugaji wengi kutozitegemea kwa asilimia 100 na kuendelea kupoteza mifugo yao.
Mnyama mwenye matatizo ya kiafya
Mnyama mwenye shida ya kiafya hukosa hamu ya kula na kunywa maji, mwili kunyong’onyea na kuonekana mchovu na hutembea pole pole na kwa taabu na mara nyingi hujitenga na wenzake.
Pia, pua zake na midomo huonekana kukauka na kupunguka kwa kiwango cha uzalishaji kama vile maziwa. Kwa madume huzubaa na kuinamisha shingo chini na kukosa hamu ya kuwapanda majike wanaokuwa kwenye joto.
Mnyama mwenye afya nzuri
Mara nyingi mnyama mwenye afya nzuri huwa mchangamfu wakati wote, macho mang’avu huku mkia na masikio vikimsaidia kufukuza inzi na pia hula na kucheua, kunywa maji vizuri kila siku.
Mnyama huonyesha ushirikiano na kutembea pamoja kwenye kundi huku akitembea vizuri, anashtuka na kukimbia anaposhtuliwa na mnyama hatari anapomkaribia.
Mwili wa mnyama mweye afya nzuri una uwezo mkubwa wa kukibadili chakula anachokula, kutoa mazao ya kutosha kama vile maziwa na anaonekana mwenye nguvu na kwa wale wanaoendelea kukua wanaongezeka uzito kwa muda mfupi.
Kwa mnyama anayekamuliwa mara kwa mara kupiga kelele za kumtafuta mtoto wake, kiwele huwa kimejaa maziwa, chuchu huwa wakati mwingine zimetanuka upande kwa ajili ya kujaa maziwa.
Aidha, ngozi ya mnyama husisimka mara kwa mara wadudu wapomtambaa, ngozi kuwa na ulaini unaotakiwa na manyoya hung’aa na pua na midomo huwa na unyevu unyevu wakati wote.
Kwa madume, huwa wana hamu ya kuwapanda majike wanaoingia kwenye joto, miili yao hujengeka vizuri.
Kwa kawaida unapo mkaribia mnyama mweye afya njema na asiye na tatizo lolote la viungo endapo atakuwa amekaa chini ni lazima atanyanyuka na ikiwa amesimama ataanza kusogea sogea kuangalia unataka kufanya nini.
Nini husababisha magonjwa kwa mifugo
Magonjwa mengi ya mifugo husambazwa na vijidudu ambao huingia kwenye mfumo wa damu na kusababisha homa na baadae madhara makubwa.
Mangonjwa mengi ya mifugo husababishwa na vyanzo kutoka nje ya mwili wa mnyama mfano mazingira machafu anayoishi mnyama, vitu vinavyosababisha vidonda na ambazo vimelea vinaweza kukaa.
Pia mnyama anaweza kupata ugonjwa kutokana na hali za ndani ya mwili kama upungufu wa lishe, mfano; madini, na na magonjwa ya kurithi.
Upungufu wa viinilishe katika chakula cha mifugo husababisha madhara katika mwili.
Madhara hayo ni kama vile majike kutopata joto mapema, ndama kuzaliwa na viungo visivyo komaa, upungufu wa uzalishaji maziwa na kiwango cha uzalishaji kushuka
Kutokuzingatia usafi kwenye banda la ng’ombe, pamoja na kusafisha kiwele vizuri kabla na baada ya kukamua, mkamuaji mwenye kucha ndefu na ambaye hajasafisha mikono vizuri kabla ya kumkamua ng’ombe pia ni chanzo kikubwa cha kueneza magonjwa.
Nini cha kufanya
Pamoja na changamoto hizi, magonjwa yaliyo mengi huweza kutibiwa kwa kutumia njia za kienyeji na dawa za kienyeji ambapo pia ni vyema wataalamu kuwafundisha wafugaji ili kujua njia hizi na kutumia kwa ufasaha, hivyo kusaidia kupunguza gharama za ufugaji/matibabu kwa wafugaji na jamii kwa ujumla.
Wafugaji walio wengi wana ujuzi wa miti shamba, ambao umewafaa wengi wao kwa miaka kadhaa ambao umeanza kupotea kwa kiasi kikubwa na kusababisha njia za kisasa kutumika zaidi.
Aidha, jambo hili linahitaji wafugaji na wakulima kulirejelea tena kwani zina msaada sana hasa katika maeneo ambayo huduma za kisasa haziwezi kupatikana kwa urahisi lakini pia njia za kienyeji ni bora zaidi kiafya na kiuchumi.