Mboga ya asili
- Kutuhusu

Kwa nini tunafanya kilimo?

Sambaza chapisho hili

Kilimo kimekuwepo tangu kale za mababu zetu. Binadamu wa kwanza walipata chakula chao kwenye mazingira yanayowazunguka na kwa juhudi kama uwindaji kabla ya kuanza kulima ardhi, kupanda mazao na kufuga mifugo kama vyanzo vya lishe. Hii ni pamoja na nafaka, mazao ya mizizi, karanga, matunda, nyama, maziwa, na hata mayai. Kilimo kimebadilisha maisha na maisha pia yamebadilisha muundo wa kilimo.

Kwa sasa, kilimo ni muhimu sana na umuhimu huu hauwezi kupungua katika miaka ya karibuni. Maadamu watu wanaishi, ni lazima wakule na wakulima wataendelea kulima!

Nini kinafanya kilimo kuonekana muhimu zaidi? Nini hufanya wakulima kutumia muda wao mwingi mashambani; kwenye jua kali, wakivuta vumbi toka kwenye ardhi iliyokauka wakati wa maandalizi ya msimu wa mvua, kuloa wakati wa mvua za rasharasha wakijaribu kupata thamani zaidi?

Watu wengi hawajawahi kufikiri kwa nini kilimo ni muhimu sana, hata wakulima wenyewe hawajiulizi hili. Tunafanya kilimo kama desturi tu, na tukijaribu kueleza kwa nini tunafanya tunachofanya, tunashindwa kujieleza au tunaeleza bila kuwa na uhakika.

Chakula na lishe

Mboga ya asili

Upatikanaji wa chakula na lishe ni haki ya msingi ya binadamu. Tuangalie takwimu zinazofuata.

  • Takribani watu bilioni 7.7 duniani utegemea wakulima ambao utumia muda wao hata wa ziada kufanya kilimo kwa ajili ya kulisha watu hawa kuishi.

Hii inasisitizwa na malengo ya maendeleo duniani (MDGs) inayoipa kipau mbele lengo la kukabiliana na njaa.

  • Watu milioni 815 (ambayo ni 10% ya watu ulimwenguni) wanapata mlo mdogo, na hii ni aibu kubwa kwa ulimwengu katika karne ya 21.

Watu wengi wanaokabiliwa na njaa duniani wanaishi katika nchi zinazoendelea za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia ya Kusini.

Hapa nyumbani Tanzania;

  • Zaidi ya asilimia arobaini na tisa (49%) ya idadi ya watu nchini wanaishi chini ya TSh 4,612 (Dola 2) kwa siku.
  • Kiwango cha utapia mlo nchini kimezidi kuwa juu sana.
  • Asilimia 34 ya watoto chini ya miaka mitano wamedumaa,
  • Takribani asilimia 45 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa wana upungufu wa damu.
  • Sehemu kubwa ya idadi ya watu nchini bado wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula na lishe; wengi wao wanaishi maeneo kame vijijini, maeneo yenye watu wengi na ardhi ndogo, maeone yanayopakana na miji mikubwa na miji midogo zinazokua.

Haya ni maswala mazito sana katika usalama wa chakula na lishe, na kuna umuhimu wa kuhakikisha kuwa watu katika maeneo haya wanapata chakula na lishe bora.

Suala la chakula na lishe ni suala la usalama wa taifa. Nchi inayoshindwa kulisha watu wake iko katika hatari ya kuhadaiwa, kuchokozwa na kufanyiwa ujanja na nchi za nje. Hii ni mazingira ngumu ya kufanya kazi na kuzalisha mali.

Lishe bora hujenga kinga thabiti ya mwili na kufukuza magonjwa. Watu wenye afya bora ni nguvu kazi imara kwa taifa. Kwa mantiki hii, wakulima ni lazima watambue kuwa hawapo tu kwa ajili ya kulima bali wana jukumu kubwa ya kufanya katika taifa.

Mbali na lishe, chakula bora huburudisha

Nyama na ugali

Hebu fikiria ni wakati wa chakula cha mchana, na unaelekea nyumbani. Ghafla, ukiwa getini kwako unakutana na mnuzo wa harufu nzuri ya pilau. Katika siku yako ya mapumziko ya wiki, upo na marafiki zako mmekaa kijiweni mlikozoea, upo na kinywaji chako. Ghafla mlango wa jikoni unafunguliwa kwa bahati mbaya na unakutana na harufu nzuri ya nyama ya kukaanga. Kwa hakika unapataka hamasa moja kwa moja; hamu kubwa ya kumega, kutafuta, kumeza chakula kile na utamu wake wote. Hivyo ndivyo, chakula bora kutoka kilimo bora kinavyoridhisha na kufurahisha.

Uchumi na ajira

Kilimo ni moja ya sekta ya uzalishaji inayosaidia kukuza uchumi wa nchi. Inatoa ajira moja kwa moja kwa asilimia 75 ya nguvu kazi na huchangia moja ya tatu (30%) ya pato la ndani la taifa (GDP). Sekta ya kilimo iliyo thabiti hupimwa kwa uchumi imara, usioyumba na usiokuwa na mfumuko wa bei.

Sekta ya kilimo inaonyesha mafanikio kwa haraka na moja kwa moja inapopokea mtaji ili kuchochea uzalishaji wa mali. Hii inaonekana kupitia ukuaji wa uchumi, kuongezeka kwa nafasi za ajira na mapato kwa vijana; wengi ambao hawajasoma, hawana ustadi au wana ujuzi na uzoefu mdogo wa kufanya kazi.

Umri wa wastani wa wakulima wadogo wadogo Tanzania ni zaidi ya miaka 60. Hata hivyo, watu wapya wanaoingia katika kilimo wanaleta mbinu mpya za kuimarisha na kubadilisha jinsi ya kufanya kilimo nchini Tanzania.

Kwa namna hiyo, vijana wengi wanaaingia katika kilimo; uzalishaji wa maziwa, kuku, kilimo cha mboga-mboga, uzalishaji wa majani ya malisho na kadhalika, wanaweka jitihada katika teknolojia ili kuboresha mchakato wa uzalishaji. Hii inawaletea faida kubwa huku wanaongeza nafasi za ajira kwa vijana wenzao.

Aidha, wanatumia mtandao na mitandao ya kijamii kuwafikia wateja moja kwa moja bila kupitia kwa madalali. Hivyo, wanasaidia mkulima kuteka dhamani yote na kupata faida yake moja kwa moja kutoka kwa mlaji bila kutumia mnyororo wa watu wengi.

Mazingira

Tunaishi katika kipindi ambacho uharibifu wa mazingira unaendelea kuongezeka na kupelekea madhara yayosababisha kupungua kwa umri wa kuishi. Uchafuzi wa vyanzo vya maji, hewa chafu kutoka viwandani, ukataji wa miti kiholela ni shughuli zinasodumaza badala ya kudumisha maisha mazuri. Aidha, matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi yamebadili mfumo wa mvua ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Kilimo bora huchangia uhifadhi mkubwa wa mazingira na mkulima mzuri anajali mazingira, na wakati wa kuzalisha chakula anatunza pia mazingira kwa lengo la kuzalisha chakula salama na kulinda afya za walaji.

Moja ya vitendo vinavyoanza kukita mizizi kwa utaratibu nchini Tanzania ni upimaji wa udongo ili kujua virutubisho vilivyopo na vinakosekana. Hii inamwezesha wakulima mkulima kuongeza virutubisho sahihi katika udongo, kupunguza asidi (kuunguza) kwenye udongo hasa katika maeneo yanayolimwa mazao kama vile mtama, mchele, pamba na miwa.

Jambo la msingi ni kama hatutatunza ardhi tunayotumia, tutaiharibu. Hivyo, tunahitaji wakulima kutunza ardhi kwa kufanya kilimo sahihi.

Kilimo chetu kinatimiza utoaji wa chakula na lishe, kukuza uchumi na lengo kubwa la uhifahi wa mazingira. Bila kilimo kizazi kijacho kimanyimwa na kitaumia. Vijana wa kisasa wanakaribishwa kuingia na kuchuma hela kwenye kilimo.

Ni nini falsafa yako ya kilimo? Tushirikishe kwa kuacha maoni yako hapa chini ama kuandika barua pepe kwa info@mkulimambunifu.org

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *