Kilimo kitabaki kuwa msingi wa ukuaji wa uchumi kupunguza umaskini na kudumisha mazingira iwapo kitafayika kwa utaratibu. Hata hivyo ni muhimu mkulima kuzingatia kilimo biashara ili kukuza kipato.
Kilimo biashara ni fursa muhimu ambayo mkulima anapaswa kufanya kwa kuzingatia utaratibu maalumu. Hii ni pamoja na kufanya tathmini ya biashara ili kuhakikisha kufaulu kwake.
Katika makala hii tutaangazia kuhusu kilimo biashara na jinsi kilivyo fanikiwa kwa wanakikundi wa KIBIU Meru, Arusha.
Mambo ya kuzingatia unapotaka kufanya kilimo biashara, inawezekana umejifunza au kusoma kuhusu kilimo biashara. Makala mbalimbali za Mkulima Mbunifu zilishaandika kuhusu kilimo biashara. Makala hii itakurejeza kwa ufupi mambo muhimu ya kuzingatia kama ifuatavyo;
- Utambuzi na ufafanuzi wa fursa ya biashara
Mkulima lazima atambue fursa ya biashara na aweze kuonyesha namna atakavyoweza kutumia nafasi hiyo ili kupata faida. Hii ni pamoja na kuangaza soko la bidhaa bila kusahau hatari zinazoweza kutokea.
- Upangaji wa biashara
Mpango wa biashara humwezesha mfanyabiashara kuandika utendakazi wa biashara kwenye karatasi, ili kutathmini namna biashara ikakavyokuwa kabla ya kuwekeza pesa.
3. Utekelezaji
Utekelezaji una maana ya kuweka vitendo kwenye mpango wa biashara. Wakati wa utekelezaji, weka kipaumbele kwa mambo muhimu. Tumia taarifa kutoka kwenye soko ili kufanya maamuzi kuhusu bidhaa.
Hata hivyo utekelezaji wa mpango huo lazima uanzie kwenye hatua ya uzalishaji. Jambo la pili litakuwa ni kutekeleza mpango wa uuzaji. Kumbuka kuwa utekelezaji wa michakato hii yote huhitaji fedha. Fedha za kutosha lazima zipatikane ili kupanga uzalishaji na uuzaji au shughuli yoyote ile inayohusika katika mchakato wa kuhakikisha kuwa bidhaa zinamfikia mtumiaji.
- Mfumo
Mfumo unahusisha uratibu wa vipengele vyote vya biashara ambavyo ni muhimu kwa kufanikiwa kwake. Hii itajumuisha mfumo wa uzalishaji na uuzaji kupitia kwa uongozi bora. Hakikisha kuwa wafanyakazi wanaohusika wanapatikana na wanafanya kazi yao vizuri.
- Tathmini
Angazia upya maendeleo ya utekelezaji ili kuhakikisha kwamba kila sehemu inaendelea vyema. Kufutilia kwa maendeleo inafaa kufanyika mfululizo. Kila shughuli katika kila kiwango lazima ifanyiwe tathmini ili kuangalia kama inachangia lengo kuu.
Kikundi cha KIBIU (Kilimo, Bihashara, Ufugaji)
Mkulima Mbunifu ilitembelea kikundi cha wakulima KIBIU (KILIMO BIASHARA na UFUGAJI) kwa lengo la kunukuu mafanikio ya kilimo biashara. Ni kweli, “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu”.
Mkulima Mbunifu imebaini mafanikio ya kilimo biashara kwa njia ya kikundi. Kikundi cha KIBIU kilianza kikiwa na wakulima Ishirini (20) ambao walijikita katika kufanya kilimo biashara kwa kuangazia masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi. Malengo makuu ilikua ni kujifunza kwa pamoja, kuzalisha mazao ya kilimo ili kupata kipato kwaajili ya kuboresha lishe ya familia na makazi.
Hata hivyo, kikundi hiki kimefanikiwa kwani wamepata soko la kuuza mazao nje ya nchi kwa njia ya mkataba. Utaratibu, kanuni na sharia za kikundi hiki ikiwamo uongozi mzuri umesaidia mafanikio ya mkulima mmoja mmoja.
Kupitia kikundi wakulima shiriki wamenufaika kulima na kuuza mazao ya mkataba yanayohitajika na kampuni kwa muda husika. Hata hivyo, kila mkulima anafanya kilimo chake katika eneo lake akizingatia kanuni na sharia walizojiwekea. Mkulima hulipwa kulinganana na alichozalisha. Hii imewatia motisha wakulima wengine kujiunga na kikundi hiki na mpaka sasa kufikia wanakikundi 237.
Wakulima ni vema kujiunga katika vikundi kwani kupitia vikundi nirahisi kujifunza na kupashana habari mbalimbali kuhusu kilimo na masoko.
Kwa mawasiliano zaidi kuhusu kilimo biashara wasiliana na mwenyekiti Bw. Jeremia Ayo, kwa simu namba 0754 664 882.