- Mifugo

JAGEF wanaonesha njia katika usindikaji wa vyakula

Sambaza chapisho hili

“Kukaa mwenyewe na kufanya shughuli za ujasiriamali ni rahisi sana kuanguka, kutokutambuliwa au kuweza kupiga hatu, lakini mkiwa kwenye kikundi, mnapiga hatua kwa haraka sana na wepesi zaidi”

Ndivyo alivyoanza kueleza mama Ester Moshi, mwenyekiti wa kikundi cha wasindikaji cha JAGEF katika kijiji cha Kikarara Old Moshi mkoani Kilimanjaro alipokuwa akielezea shughuli za kikundi hicho.

JAGEF kilianza mwaka 2010 kikiwa kama kikundi cha wakulima wa zao la rosella kikiwa na wanachama 10 ingawa kwa sasa wapo 9, wakiwa wanazalisha rosella na kuuza ikiwa kavu kwenye maduka ya vyakula na wasindikaji wa bidhaa za rosella.

Baadaye mwaka 2010 walipata mafunzo kutoka SIDO na Halmashauri ya Moshi vijijini juu ya lishe na usindikaji wa vyakula na ndipo walipoamua rasmi kuingia kwenye shughuli za usindikaji, na kusajiliwa rasmi na wakala wa usajili wa mashirika BRELA kwa namba 191128

Mwenyekiti wa kikundi cha JAGEF akionyesha moja ya bidhaa wanayozalisha katika kikundi chake

Shughuli wanazofanya

JAGEF wanajishughulisha na usindikaji wa vyakula vya aina mbalimbali kama vile unga wa lishe, ndizi, matunda na mbogamboga.  Halikadhalika hutengeneza jamu, achari. Pia wanazalisha mvinyo wa ndizi, rosella, zabibu na mtama.

Pamoja na uzalishaji wa bidhaa za aina mbalimbali, Ester anaeleza kuwa wamejikita zaidi katika usindikaji wa unga kwa kuwa uhitaji wake ni mkubwa, hivyo unatoa mwanywa kwa wao kupata faida ya haraka na kuweza kuendeleza miradi mingine.

Kwa nini waliunda kikundi?

Kikundi hicho kiliundwa ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na umaskini, pamoja na kuokoa mazao ya wakilima ambayo mara nyingi yanaharibika kwa kukosa soko wakati wa msimu, na baadaye wakulima hao hao kutaabika kwa ukosefu wa aina hiyo ya mazao kama vile matunda.

Mafanikio

Ester anaelez kuwa moja ya mafanikio makubwa ambayo JAGEF wamepata ni pamoja na kujipatia ajira, ambayo imewawezesha kupata pato la kuendeshea maisha ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto wao na kukuza miradi ya kilimo, huku wakiondokana na hali ya kuwa tegemezi.

JAGEF wamefanikiwa kupata udhibitisho wa ubora wa bidhaa zao wanazozalisha kutoka TBS na kuwafanya kuwa na hatua zaidi katika soko

Pia wameweza kujifunza mambo mbalimbali na kufahamiana na watu wa kada tofauti tofauti.

Malengo

  • Kikundi cha JAGEF kina malengo ya kuwa na kiwanda kikubwa chenye mashine za kisasa kwa ajili ya usindikaji wa bidhaa za mazao ya kilimo wanazozalisha, ili kutoa fursa kwa wakulima nchini Tanzania kuwa na soko la uhakika la mazao yao.
  • Kutoa ajira kwa kina mama na vijana
  • Utunzaji wa mazingira kwa hali ya juu
  • Kutoa ajira ya kudumu kwa wanakikundi na watu wengine muhimu watakaoajiriwa na kikundi hicho

Changamoto

Penye mafannikio siku zote hapakosi kuwa na changamoto. JAGEF pia wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile

  • Ushindani kwenye soko kutoka kwa wazalishaji wengine
  • Vifungashio kwa ajili ya bidhaa wanazozalisha
  • Soko: Bado bidhaa zao hazijafahamika vizuri kwenye soko, na gharama za kujitangaza ni kubwa sana.
  • Kodi: Kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye bidhaa zao ni kubwa sana, huku kukiwa na bidhaa nyingine zinazofanana kwenye soko ambazo hazilipiwi kodi, hivyo kuumiza wao kama walipa kodi.
  • Upatikanaji wa mtaji wa kutosha pamoja na vifaa vya kisasa bado ni tatizo

Wito

Ester anatoa wito kwa watu wote na serikali kufanya mambo yafuatayo:

  • Kuhimiza watu wote kuwa na uthubutu wa kufanya mambo tofauti kwa lengo la kuboresha maisha
  • Kina mama waepuke makundi yanayokatisha tamaa na badala yake wabuni na kuibua miradi itakayowasaidia
  • Wajasiriamali wawe wadadisi, wabunifu na washirikishane ujuzi
  • Serikali isaidie wajasiriamali kupata vifungashio vya kisasa na kwa bei nzuri vitakavyosaidia kutoa ushindani katika soko
  • Serikali isaidie wajasiria mali kupata vitendea kazi vya kisasa, vitakavyosaidia kufanya kazi kwa muda mfupi zaidi
  • Kuwepo na utaratibu wa serikali wa kuwapatia wasindikaji ruzuku au mitaji kukuza shughuli zao
  • Serikali iwe na utaratibu wa kutembelea viwanda vidogo vidogo ili kujionea maendeleo yao na kuwapa motisha pale inapostahili
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *