- Mifugo

Nguruwe: Mifugo yenye gharama ndogo, tija zaidi

Sambaza chapisho hili

Kwa kawaida nguruwe ni lazima wafugwe ndani ya banda, wasiachwe kuzurura ovyo nje

Ili kuwa na ufugaji wenye tija, na kuweza kuepuka baadhi ya magonjwa yanayoshambulia nguruwe, ni lazima mfugaji azingatie mambo ya msingi katika ufugaji.

Banda

Ni muhimu kuhakikisha kuwa unapohitaji kufuga nguruwe, unakuwa na banda lililotayarishwa vizuri na liwe imara. Utayarishaji mbaya wa banda unaweza kusababisha nguruwe kuugua mara kwa mara na kusababisha hasara.

  • Inashauriwa banda liwe na sakafu ya changarawe
  • Banda liwe na hewa ya kutosha, kusiwe na joto kali
  • Banda liwe na usafi wa hali ya juu ili kuepuka minyoo na ugonjwa wa ukurutu (Mange)
  • Idadi ya nguruwe isiwe kubwa kwenye banda
  • Chakula kiwe na madini yanayotakiwa, mfano; kalishamu, fosiforasi – aina hizi za madini hupatikana zaidi kwenye mifupa, mashudu na pumba
  • Eneo liwe na maji ya kutosha
  • Watoto wa nguruwe wachomwe iron wiki ya kwanza tangu kuzaliwa
  • Nguruwe wapewe dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu. Hii itasaidia kuepusha magonjwa ya minyoo

Lishe

Ulishaji wa nguruwe ni rahisi kwa kuwa wanakula aina mbalimbali za vyakula kulingana na mazingira wanayofugwa. Nguruwe wanaweza kulishwa kwa kutumia aina mbalimbali za majani laini, na pia wanaweza kulishwa kwa kutumia masalia ya nafaka kama vile pumba na mashudu, unaweza pia kuwalisha masalia ya jikoni, mradi tu yawe katika hali ya usafi.

Magonjwa yanayoshambulia nguruwe

Magonjwa ya minyoo: Kwa kiasi kikubwa nguruwe hushambuliwa na magonjwa ua minyoo hasa tegu. Aina hii huathiri ukuaji na afya ya nguruwe kwa kiasi kikubwa sana. Inapotokea minyoo hii ikamwingia binadamu, inaweza kusababisha kifafa.

Udhibiti

  • Njia kubwa ya kudhibiti magonjwa ya nguruwe hasa yanayotokana na minyoo ni usafi.
  • Nguruwe wapewe dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu
  • Kinyesi cha nguruwe kipimwe ili kuweza kutambua kuwa ni aina gani ya minyoo waliyo nayo

Homa ya nguruwe

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na virusi, ambao huenezwa kwa njia ya mgusano. Ugonjwa huu ni hatari kwa kuwa huenea kwa haraka sana, na ni tishio kwa nguruwe. Nchini Tanzania ugonjwa huu umezoeleka kutokea zaidi katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.

Kinga: Bado kinga ya ugonjwa huu haijapatikana, hivyo njia kubwa ya kuudhibiti ni kuweka karantini mara unapotokea. 

Tiba: Hakuna tiba ya ugonjwa huu kwa sababu ni ugonjwa unaosababishwa na           virusi.

Ugonjwa wa ngozi (Ukurutu)

Ugonjwa huu wa ngozi huenezwa na wadudu wadogo sana wajulikanao kitaalamu kama merge mites. Wadudu hawa hujichimbia kwenye ngozi ya nguruwe na kusababisha muwasho. Aina hii ya ugonjwa pia hushambulia aina nyingine za wanyama.

Kuenea: Ugonjwa huu huenea kwa njia ya mgusano.

Muonekano: Nguruwe au mnyama alieathirika na ugonjwa huu hupukutika unga unga. Watoto wa nguruwe huathirika zaidi na ugonjwa huu kwa sababu ya kunyonya.

Dalili: Mnyama alieathiriwa na ugonjwa huu hujikuna mara kwa mara. Mnyama hupukitika unga unga.

Tiba: Ugonjwa huu hutibika kwa kutumia dawa aina ya ivormectin. Dawa hii hutibu minyoo wa ndani na wadudu wa nje.

Ugonjwa wa kimeta (Anthrax)

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria. Ugonjwa huu huenea kwa njia ya hewa. Ugonjwa huu ni tishio sana kwa sababu huua kwa haraka, hata unapompata binadamu pia hufa kwa haraka sana.

Dalili: Mnyama aliepatwa na ugonjwa huu hutokwa na damu kwenye sehemu zote zenye uwazi kwenye mwili wake. Ugonjwa huu husababisha damu kutokuganda, hata baada ya kufa.

Udhibiti: Baada ya mnyama kufa, fukia kwenye shimo lenye urefu zaidi ya mita mbili. Fukia kwa uangalifu na ikiwezekana kazi hiyo ifanyike chini ya usimamizi maalumu wa wataalamu wa mifugo na afya. Choma moto na kuteketeza mzoga kabisa.

Tiba: Ni vigumu sana kutibu ugonjwa huu kwa kuwa hutokea na kuua kwa ghafla.

Kosidiosis

Ugonjwa huu husababishwa na wadudu aina ya coccidia, ambao hushambulia mfumo wa chakula. Ugonjwa huu husababisha nguruwe kuharisha na kusababisha ukuaji kuwa wa shida.

Dalili: Nguruwe hudhoofika

Kinga: Kwa kiasi kikubwa kinga ya ugonjwa huu ni usafi

Tiba: Ugonjwa huu hutibiwa kwa kutumia dawa aina ya Amplorium

Nguruwe kwa njia asili

Kwa kawaida nguruwe wana asili ya kujitafutia, huwa wanafanya vizuri wanapoachwa wakajilisha; kulingana na viwango vya kilimo hai, nguruwe wanahitaji sehemu ya kukimbia na kufanya mazoezi. Nguruwe ambao wanafungwa sehemu moja na yenye msongamano, huwa na msongo na hukosa baadhi ya virutubisho tofauti na wale wanaofugwa sehemu yenye nafasi. Endapo ukiamua kufuga nguruwe kwa kuwaacha  huru, ni lazima uwatengee vizimba vyenye nafasi ya mita 10 kwa 10 kwa nguruwe wawili, na ni lazima kuwe na mzunguko kila baada ya miezi miwili.

Endapo unawaacha nguruwe kujitafutia wenyewe kumbuka kuwa wana asili ya porini na hawapendi mwanga mkali wa jua. Miili yao ina joto, hivyo hupenda kujiviringisha kwenye matope, mtoni kwenye maji na sehemu yenye dimbwi n.k ili kupunguza joto la mwili wakati wa joto. Nguruwe wanaokulia sehemu ambayo hawawezi kupata maji ya kujiloweka huwa wanapata usumbufu kwenye miili yao kirahisi. Hali hii hupunguza uwezo wa miili yao kuwa na kinga.

Tatizo moja la wafugaji wadogo wa nguruwe ni kwamba, huwaruhusu nguruwe kula takataka, na hata zinazotokana na binadamu na makombo ya chakula na mimea iliyooza. Mbali na hatari ya kupata homa ya nguruwe, ni kwamba wanapokutana na wanyama wa mwituni na katika hali hiyo hupata wadudu hatari kama vile tegu, ambao husababisha kifafa wanapoambukizwa kwa binadamu.

Ili kuwalinda walaji wa bidhaa zinazotokana na nguruwe na kuimarisha ubora wake, makampuni yanayonunua nguruwe kutoka kwa wakulima, wana sheria thabiti kwa wafugaji wanaowauzia nguruwe. Moja ya kanuni na sheria hizo ni kwamba, nguruwe ni lazima afugwe kwenye banda safi na lenye nafasi ya kutosha kwa ajili ya kupumzika na kucheza.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Nguruwe: Mifugo yenye gharama ndogo, tija zaidi

  1. napenda sana ufugaji na kilimo na jarida hili limekuwa msaada kwangu kwa kuwa napata vitu vipya na natumaini nitatoka kimaisha kwa kupitia jarida hili hivyo niombe endeleeni kutupa ujuzi kwa faida ya dunia nzima kwa ujumla

    1. Habari,

      Karibu sana Mkulima Mbunifu. Tunafurahi sana kusikia unasoma makala zinazochapishwa katika jarida la Mkulima Mbunifu. Sisi pia hatutaacha kuwapa wakulima wetu elimu kila mara tunapotoa jarida la Mkulima Mbunifu ila tunachosisitiza wakulima na wasomaji wetu watumie elimu wanayopata kwa vitendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *