Jarida hili limekuwa mstari wa mbele katika kukudondolea mada mbalimbali zenye tija katika nyanja za ufugaji na kilimo. Mara nyingi mada hizo hujikita katika njia zinazotumika kuzalisha kiasili. Katika toleo hili tutakudondolea moja wapo ya changamoto zinazowakabili wafugaji wa kuku na namna ya kuondokana na changamoto hizo.
Zifuatazo ni sababu au hali inayowakumba kuku na kusababisha kuku kutaga mayai yanayoonekana kuwa ni madogo sana. Hii hali huchangiwa na vitu vingi kama vile;
- 1. Umri wa kuku
Kuku wengi wanapoanza kutaka kutaga huwa wanataga mayai madogo madogo lakini kadri siku zinavyozidi kwenda huongezeka ukubwa. Hii inamaanisha kuwa kama wana umri wa wiki 32 na kuendelea hawawezi kuwa na tatizo hilo isipokuwa sababu zingine zinaweza kuchangia.
- Vinasaba vya kuku
Kuna kuku wengine vinasaba vyao huwafanya kutaga mayai madogo tu na hivyo hata uwafanyeje hawawezi kutaga mayai makubwa, hivyo ndivyowalivyoumbwa n ahata ubadili mazaingira, bado watataga mayao madogo kutokana na vinasaba vyao.
- Msongo
Msongo unaweza kusababishwa na joto kali ndani ya banda, ukosefu wa maji, ukosefu wa hewa ya kutosha pamoja kuzidi kwa mwanga ndani ya banda. Vile vile wakati mwingine msongo huweza kusababishwa na wanyama wakali kuingia bandani.
- Lishe
Mara nyingi kuku wenye wiki zaidi ya 32 wakikosa protini na chumvi ya kutosha husababisha kutaga mayai madogo. Pia inashauriwa kuhakikisha unabadili chakula mapema kutoka hatua moja ya ukuaji kwani nayo inaonekana kuwa ina mchango katika utagaji wa mayai madogo. Pia hakikisha kuku wanapata chakula wanachostahili pamoja na maji kwa siku.
- Ugonjwa
Magonjwa kama vile ya minyoo na “egg dropping syndrome” yanaweza kusababisha kushuka kwa utagaji. Wakati mwingine kutaga mayai madogo madogo. Hakikisha kuku wanapata dawa ya minyoo kila baada ya miezi 3.
Mara nyingi baadhi ya wafugaji wamekuwa wakilalamika kwamba kuku wao wamekuwa hawatagi, na wengi wao hawajui sababu. Hizi ndizo sababu za kuku kupunguza na wakati mwingine kuacha kabisa kutaga;
Kuku hupunguza utagaji na hata kuacha kutaga kabisa iwapo:-
- Kutokupewa chakula bora au cha kutosha.
- Hawapewi maji safi ya kutosha.
- Wamebanana, yaani hawakai kwa raha.
- Vyombo vya maji au chakula havitoshi.
- Mwanga hautoshi.
- Majogoo yamezidi katika chumba(weka jogoo 1 kwa mitetea 10)
- Kuku wanaumwa.
- Wana vidusa vya nje na ndani.
- Wamezeeka (umri zaidi ya miaka miwili na nusu).
- Maumbile ya kuku mwenyewe.
Ni muhimu mfugaji kuhakikisha anazingatia mambo yote ambayo yako kinyume na hayo ili kupata matokeo chanya kama ilivyokusudiwa tangu kuanzishwa mradi wa ufugaji.