Mchicha nafaka ni jamii ya mchicha katika kundi la mboga lakini wenye kulimwa kwa ajili ya kupata nafaka. Mimea yake ni tofauti na mimea ya nafaka nyingine kama vile ngano, mahindi au mtama.
Asili ya mchicha nafaka ni huko Mexico, Amerika ya Kusini, na mchicha huu ulikuwa ukitumika kama chakula kikuu cha nchi hiyo ikiwa ni moja ya nafaka.
Makundi ya mchicha
Kuna makundi makuu manne ya mchicha ambayo ni mchicha nafaka (Grain Amaranthus), mchicha majani (Vegetable Amaranthus), Mchicha mapambo (Ornament Amaranthus) na mchicha magugu (Weed Amaranthus).
Namna ya kupanda
Unaweza kupanda kwa kusia mbegu katika mistari yenye umbali wa sentimita 18 kati ya mistari, na kisha baadaye kuendelea kupunguza kwa kung’oa baadhi ya miche.
Baada ya siku 3 hadi 6 kutegemeana na hali ya hewa, mbegu ya mchicha nafaka itakuwa imeota.
Palizi
- Fanya palizi katika wiki ya pili kwa kung’oa magugu yoyote katika shamba.
- Katika wiki ya tatu, punguza mimea kwa kung’oa na kubakiza mimea mitatu katika eneo moja.
- Fanya palizi ya mwisho katika wiki ya 5 hadi 6 huku uking’oa na kubakiza mche mmoja tu katika eneo moja ambao ndio utakaovunwa.
Kumbuka: Mimea inayong’olewa itumike kwa ajili ya chakula yaani mboga.
Faida za kilimo cha zao la mchicha nafaka
- Ni rahisi kuzalisha kwani hulimwa kama nafaka nyingine
- Mchicha nafaka huweza kulimwa katika udongo wa aina yeyote ila wenye pH 4.7 hadi 7.2.
- Mchicha huu unavirutubisho vingi kama Vitamini A, C na E, madini ya chuma, Zinc, nyuzinyuzi na Amino Acid, protini, kalshiamu, magnesiamu, potashiamu na fosiforasi.
- Zao hili linavumilia ukame na linaweza kulimwa katika maeneo yenye mwinuko.
Mchicha nafaka hutumika kuandaa vyakula vya aina mbalimbali kama vile kutengenezea tambi, mikate, maandazi, keki, ugali, uji, na hata bisi.
- Mchicha nafaka hukomaa haraka kuliko nafaka nyingine kama mahindi na mtama kwani huchukua siku 45 hadi 75 (kulingana na hali ya hewa) toka kuoteshwa hadi kuvunwa.
- Zao hili linatoa mavuno kiasi cha kilo 800 hadi 1200 kwa ekari moja na linaweza kustahimili magonjwa.
- Majani yake huweza kutumiwa kama malisho kwaajili ya wanyama na hata kuku.
- Zao hili baada ya kuvuna, huweza kukaa kwa muda mrefu sana bila kuharibika.
Namna ya kusindika mchicha nafaka kupata unga
Kama ilivyo ada kwa mazao mengine kabla ya kupata bidhaa tarajiwa, kuna hatua mbalimbali za kufuata ili kuweza kupata bidhaa iliyo bora.
Mbegu/punje za mchicha nafaka
Vifaa
Katika usindikaji wa bidhaa nafaka, vifaa vinavyohitajika ni pamoja na nyungo, turubai, kisu kikali kisichokuwa na kutu, mifuko isiyotoboka ya kuvunia na kubebea nafaka, mifuko ya kuhifadhia unga.
Malighafi
Malighafi pekee inayohitaji katika usindikaji wa mchicha nafaka ni punje za mchicha huu.
Hatua za usindikaji
- Hakikisha mbegu za mchicha huu zimekomaa na ziko tayari kwa ajili ya kuvunwa. Hii utajua kwa kuangalia majani yake kwani kama iko tayari kuvunwa, majani yake yatakuwa yameanza kulegea.
- Chukua kisu kikali na kata shina lililobeba mbegu zilizokwisha kukomaa kisha weka kwenye mfuko.
- Weka mavuno yako juu ya chandarua kisha chukua mti na piga piga siku hiyo hiyo kutoa mbegu.
- Baada ya kutoa mbegu yote kwenye masuke, chukua ungo na peta kuondoa taka zote.
- Anika kwa muda wa siku 2 hadi 3, kisha baada ya kukauka weka katika chombo safi na hifadhi kwenye mifuko au madumu au peleka mashine moja kwa moja kwa ajili ya kusaga kupata unga.
- Unga ukishapatikana, chukua pakiti au vifuko maalumu vilivyokwisha kuandaliwa tayari kwa kufunga unga wako.
- Weka unga kwenye vifuko kulingana na ujazo wako, tayari kwa kupeleka sokoni.