Viazi vitamu ni moja ya mazao yanayotumika kama kinga ya kukabiliana na uhaba wa chakula kutokana na sifa yake ya kuvumilia ukame kwa muda mrefu. Sehemu kubwa ya zao hili hulimwa kwa matumizi ya nyumbani.
Viazi vitamu ni moja kati ya mazao makuu ya mizizi nchini Tanzania. Zao hili hulimwa kwa ajili ya chakula. Viazi vitamu, asilia yake ni Amerika ya Kati na ya Kusini. Nchini Tanzania, zao hili hulimwa zaidi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Kagera, Arusha, Ruvuma na Singida.
Matumizi
Viazi vitamu hutumika kama chakula kwa kutayarishwa katika njia mbalimbali kama vile kuchemshwa, kukaangwa na kuchomwa. Pia, unga wa viazi vitamu hutumika kutengeneza vyakula kama keki, maandazi, kalimati, tambi na juisi. Majani ya viazi huliwa kama mboga inayojulikana zaidi kama tembele, pia hutumika katika kutayarisha mboji.
Aina
Kuna aina nyingi za viazi vitamu zinazolimwa ulimwenguni. Hapa nchini Tanzania aina zinazolimwa zaidi ni Ukerewe, Simama, Kakamega, Karoti C, Mwananjemu, Ali mtumwa mayai, Mavuno, Pananzala, Kibakuli, Sinia, Vumilia na Polista.
Uzalishaji
Zao hili hustawi maeneo mengi nchini Tanzania. Viazi hustawi vizuri katika maeneo ya tambarare yenye udongo tifutifu, unaoruhusu maji kupenya kwa urahisi. Udongo wa mfinyazi na wenye kokoto nyingi haufai kwani huzuia mizizi kupenya na kupanuka.
Shamba jipya litayarishwe vizuri kwa kufyeka vichaka na kung’oa visiki. Majani yafukiwe wakati wa kutengeneza matuta ili kuongeza rutuba ya udongo.
Kupanda
Viazi vipandwe kwa kutumia marando (machipukizi) yenye urefu wa sentimita 30 kwa mavuno bora. Inashauriwa kutumia sehemu ya juu ya shina ili kuwezesha kupata mavuno zaidi. Wakati wa kupanda mbegu ilazwe mshazari kidogo na sehemu yake kubwa ifunikwe ardhini. Macho ya mbegu lazima yaangalie juu ili yachipue vema. Pia udongo uliopo kando ya shimo lililopandwa mbegu ugandamizwe kidogo.
Nafasi
Marando yapandwe katika umbali wa sentimita 25 hadi 30 kutoka mmea hadi mmea na sentimita 60 hadi 75 kutoka tuta hadi tuta. Viazi pia vinaweza kupandwa kwa kutumia viazi vyenye afya vyenye uzito wa kati ya gramu 20 hadi 30. Hata hivyo, inashauriwa kutumia marando ili kupata mavuno zaidi na kuepuka kuenea kwa magonjwa.
Mvua
Viazi hulimwa katika hali ya joto na mvua kuanzia milimita 450 kwa mwaka na kuendelea.
Kutunza shamba
Ni muhimu kupalilia viazi vitamu katika miezi miwili ya mwanzo ili kuupa mmea nguvu ya kutambaa vizuri. Baada ya muda huo, viazi huweza kufunika ardhi na hivyo huzuia uotaji wa magugu. Ikiwa mimea itachelewa kutunga viazi na majani ni mengi, palilia kwa mara nyingine.
Wadudu
Viazi vitamu hushambuliwa na wadudu mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipepeo, mbawa kavu, fukusi na minyoo fundo.
Magonjwa
Zao la viazi vitamu hushambuliwa na magonjwa yakiwemo magonjwa yanayotokana na virusi kama Sweet Potato Chlorotic Stunt Virus (SPCSV).
Udhibiti
Magonjwa na wadudu yaweza kudhibitiwa kwa kuzingatia usafi wa shamba, na kubadilisha mazao.
Uvunaji
Viazi vitamu huwa tayari kuvunwa miezi mitatu hadi minne tangu kupanda kutegemea hali ya hewa. Viazi vinaweza kuvunwa kidogo kidogo kwa kutumia mikono, vijiti, jembe, au rato kadri vinavyohitajika.
Aidha inashauriwa viazi visiachwe ardhini muda mrefu bila kuvunwa kwani vitakomaa sana na kuwa na nyuzi, na hivyo kuharibu ubora wake. Pia kuacha viazi muda mrefu hukaribisha mashambulizi ya wadudu kama fukusi na kuoza.
Kwa mkulima mwenye eneo kubwa zaidi, inashauriwa kutumia mashine ya kukokotwa na ng’ombe (plau). Uvunaji ufanywe kwa uangalifu ili kuhakikisha viazi havikatwi wala kuchubuliwa wakati wa kuvuna.
Mavuno ya viazi hutofautiana kulingana na aina, hali ya hewa, udongo na matunzo. Mavuno ya viazi yanakadiriwa kufikia tani 20 kwa hekta.
Usindikaji
Viazi vilivyovunwa vizuri humenywa na kusafishwa kwa maji safi, kisha kukatwa vipande vidogo vidogo kwa mkono au mashine ili vikauke upesi vinapoanikwa juani. Viazi vya aina hii ni kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Viazi vilivyokaushwa vema juani huhifadhiwa kwenye mifuko, vihenge na mitungi kwa muda usiopungua mwaka mmoja bila ya kuharibiwa na wadudu.