- Mifugo

Funza walisha kuku: Ubunifu mpya wa asili kwa wafugaji

Sambaza chapisho hili

Funza ni nini?

Funza ni aina ya wadudu ambao wanapatikana kwenye mbolea ya samadi inayotokana na mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe.

Funza wanazalishwa kutokana na nini

Wadudu hawa wanaweza kuzalishwa kutokana na kinyesi cha wanyama kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo, na nguruwe kwa kuchanganywa na tope chujio linalotokana na mtambo wa biyogesi (biogas).

Sehemu ya kuzalishia wadudu

Wadudu hawa hupendelea sehemu isiyokuwa na joto kali wala baridi sana, hivyo ni muhimu kuandaa sehemu yenye kivuli kwa ajili ya uzalishaji wa funza.

Sehemu itakayoandaliwa kwa ajili ya uzalishaji wa wadudu hao, inaweza kutumika kwa muda wa miezi sita.

Muda

Wadudu hawa huchukua muda wa siku 3 kufaa kulishia kuku, tangu mbegu yake kupandikizwa kwenye sehemu ya uzalishaji.

Namna ya kuzalisha

•Andaa sehemu yenye kivuli

•Hakikisha udongo hauna magadi. Endapo uko sehemu ambayo udongo una magadi, unaweza kuchukua udongo kutoka sehemu nyingine na kuutanguliza chini kabla ya mbolea

•Tandaza udongo huo kiasi cha hatua ishirini

•Mwaga tope chujio kutoka katika mtambo wa biyogesi juu ya udongo ulioandaa kiasi cha kufunika

•Weka mbolea uliyoandaa ya ng’ombe na mbuzi juu ya tope chujio (unaweza kutumia mbolea ya ng’ombe pekee)

•Weka mbegu ya funza kisha funika kwa kutumia nyasi au majani mengine kuweka joto la wastani

•Nyeshea maji kiasi cha kulowana kila siku ili kuweka unyevu unyevu

•Funika na baada ya siku tatu, utakuwa tayari kuruhusu kuku kujilisha

Ufanisi

Kutokana na ulishaji wa kuku kwa kutumia funza, wameweza kubaini kuwa kuku wanaongeza uzito kwa haraka na kwa kiasi kikubwa, tofauti na ulishaji wa kawaida.

Ni muda gani kuku walishwe

Kwa kawaida kuku hulishwa pumba asubuhi mpaka saa saba mchana, muda ambao kuku hao huwa wameshamaliza kutaga, hivyo hufunguliwa katika eneo lao la wazi ambalo kunakuwa na matuta ambayo wadudu hao wamezalishwa, na kufunguliwa tuta moja baada ya jingine.

Kuku huweza kuwa huru kujilisha kwa kutumia funza hadi jioni, na baada ya hapo kurudi katika mabanda yao bila kulishwa aina nyingine yoyote ya chakula.

Kuku mia mbili (200) wanaweza kulishwa kwa kutumia matuta mawili hadi matatu yenye ukubwa wa mita 20 kwa siku.

Je hakuna madhara yoyote yanayotokana na wadudu hawa kwa kuku!

Wagunduzi wa njia hii mpya ya ulishaji kuku wa kienyeji wanasema kuwa, kwa kipindi cha miaka mitatu ambayo wamekuwa wakilisha kuku kwa kutumia funza, hakuna madhara yoyote yaliyoyojitokeza, sana sana kinga ya magonjwa imeongezeka kwa kuwa kuna baadhi ya magonjwa ambayo yalikuwa yakiwashambulia kuku hapo kabla, lakini kwa kipindi cha miaka miwili hawajapata tatizo lolote.

Je kuna mafanikio?

Mafanikio ni makubwa, moja wapo ni kupungua kwa gharama za utunzaji kwa upande wa chakula.

Pia ongezeko la kipato kinachotokana na ongezeko la bei kulingana na uzito wa kuku, ambao inaaminika unatokana na aina hiyo mpya ya ulishaji wa kuku kutokana na funza.

Funza pia hulisha samaki

Ulishaji wa kuku kwa kutumia funza ni upande mmoja, lakini upande wa pili hutumika pia kulisha samaki kwenye mabwawa.

Tofauti na ilivyo kwa kuku, funza kwa ajili ya kulisha samaki, huachwa kwa muda mrefu zaidi takribani wiki mbili, ili wawe wakubwa. Katika kipindi cha wiki moja na kuendelea funza wanakuwa wakubwa kuweza kulisha kuku.

Kama ilivyo kwa kuku, imebainika pia kuwa samaki wanapolishwa funza ukuaji na uzito huongezeka kwa haraka, ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za kulisha pia.

Je mbolea hiyo inafaa tena kwa matumizi mengine

Mbolea iliyotumika kwa ajili ya kuzalisha funza inafaa kabisa kuendelea kutumika shambani na kwenye bustani za mboga kama kawaida. Hakuna uharibifu wala madhara yoyote yanayotokana na mbolea iliyotumika kuzalisha funza. Na hii ndiyo maana halisi ya kilimo hai, kwani mzunguko wa asili unakamilika bila tatizo lolote.

Wito na ushauri

Wafugaji na wazalishaji wa kuku wa kienyeji na chotara wanashauriwa kutumia mazingira yao ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kutumia mbolea inayotokana na mifugo mingine kama vile ng’ombe, mbuzi na nguruwe kuzalisha aina hii mbadala ya chakula cha kuku na kupunguza gharama.

Halikadhalika kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yao kwa ajili ya kujiongezea uzalishaji na kuboresha maisha.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na Maria Kaheta kwa simu +255 767 683 824

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

4 maoni juu ya “Funza walisha kuku: Ubunifu mpya wa asili kwa wafugaji

  1. Kwanza natanguliza shukurani kwa kwa makala nzuri yenye taaluma muhimu na faida nyingi hususan kwa wafugaji. kwa upande wangu naomba ufafanuzi katika maeneo yafuatayo:
    1. Funza wanaozalishwa hapo ni wa aina gani?
    2. Iwapo mfugaji ataamua kuchanganya funza na pumba katika lishe ya kuku, anatakiwa kutumia ratio gani?
    3. Jee funza hao wanaweza kutumika katika lishe ya ng’ombe? kama ndio ni kwa ratio gani?

    1. Habari,
      Kama unavyoona kwenye picha hao funza ni weupe na wanatokana na kinyesia ma mbolea ya mifugo.
      Lisha kwanza pumba asubuhi kisha waachie kuku wajilishe funza hao kwa kiasi watakacho wao, soma makala vizuri tumeeleza kwa undani namna ya kulisha kuku kwa kutumia funza hawa.
      Funza hawa wanatumika kulisha kuku na samaki pekee kuhusu ng’ombe hapana.

  2. Niko na changamoto la mbuzi wakifikisha miezi mitatu wanaishiwa nguvu mpaka na kufa ukichinja wana kuwa awana damu naomba ushauli nifanyeje au nitumie dawa gani

    1. Habari,
      Karibu Mkulima Munifu na pole sana kwachangamoto unazokumbana nazo. Tafadhali wasiliana na mtaalamu wa mifugo aliye karibu na wewe mara tu unapokutana na changamoto kama hizi kwani hizi zinahitaji vipimo na kujua shida ni nini?

      Karibu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *