Kwa miaka iliyopita, Mkulima Mbunifu iliweza kufanya mafunzo mbalimbali, kwa waandishi wa habari, maafisa kilimo na mifugo, lengo likiwa ni kuongeza uelewa pamoja na kufundisha mbinu mbalimbali za kuandika makala zinazohusu kilimo endelevu, na namna ya kutumia vyombo vya habari katika kufundisha juu ya kilimo endelevu.
Washiriki katika semina mbalimbali zilizofanyika, walitoka mikoa mbalimbali ya Tanzania ikiwepo Tabora, Iringa, Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Mbeya.
Aidha, warsha hizo zilizoongozwa na jopo la Mkulima Mbunifu, zliweza kutoa fursa kwa maafisa ugani, wakulima pamoja na waandishi kubadilishana uzoefu wao juu ya kilimo na matumizi ya mbinu rafiki za kilimo.
Washiriki waliweza kufundishwa nini maana ya kilimo hai, mbinu rafiki za kilimo pamoja na kilimo endelevu. Ilibainika kuwa, hivi sasa kuna matumizi makubwa ya pembejeo za viwandani, ambazo huwa na madhara makubwa katika udongo, pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira nchini kote. Aidha, ilionekana kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kwa wakulima juu ya njia mbalimbali za kupunguza athari hizo katika mazingira.
Ingawa kuna ongezeko kubwa la wakulima kuzalisha vyakula kwa ajili ya soko lakini kuna umuhimu wa kuzalisha kwa kuangalia ubora wa chakula, na kulinda afya za walaji pamoja na mazingira yao.
Ufugaji wa Kuku umekuwa nguzo kuu ya biashara kwa wafugaji na wakulima wengi nchini Tanzania, na Mkulima Mbunifu limetilia mkazo katika hili kwa kuandika mara kwa mara mada mbalimbali zinazohusu ufugaji wa kuku lengo likiwa ni kuwafundisha wafugaji kuzalisha katika misingi sahihi, kuzalisha kwa malengo na kujipatia kipato kwa wingi huku wakizilinda afya zao.
Ikiwa ni njia mojawapo ya kufundisha umuhimu wa kilimo endelevu na faida zake, washiriki waliweza kupata nafasi ya kutembelea wakulima na wafugaji mbalimbali akiwepo kijana anayejishughulisha na ufugaji wa kuku mkoani Arusha na kuweza kujionea ni kwa namna gani amekuwa akifanya ufugaji huo na kujipatia kipato.
Aidha, waandishi waliweza kujionea mambo mengi kuhusu ufugaji wa kuku huku wakiuliza maswali mbalimbali ambayo walidhani huenda yakawasaidia kuzifanya makala zao kuwa nzuri, za kuvutia na za kueleimisha.
Washiriki hawakuishia hapo, walipendekeza mambo mbalimbali yanayoweza kufanyika ili kuboresha maudhui ya jarida la Mkulima Mbunifu.
Walisema kuwa, wakulima walio wengi huamini yale wanayoyapata kupitia kwenye jarida la Mkulima Mbunifu na hutumia kwa vitendo katika kufanya kilimo, hivyo basi ni muhimu sana kuliongezea jarida hili thamani hasa kwa kujumuisha gharama za uendeshaji kwa ajili ya mafunzo ya kilimo kwa vitendo na utekelezaji wa kilimo biashara.
Lengo la mafunzo yanayotolewa na Mkulima Mbunifu ni kuboresh ubora wa habari na usambazaji wa elimu kupitia vyombo vya habari nchini Tanzania, huku tumaini kubwa likiwa ni washiriki hao kuwa mabalozi wakubwa wa kilimo endelevu.