- Mifugo

Sindika viazi vitamu kuongeza thamani

Sambaza chapisho hili

Ni muhimu kusindika viazi vitamu ili kuongezea thamani, ubora na matumizi yake

Viazi vitamu husindikwa kupata viazi vitamu vilivyokaushwa, unga, wanga na jamu.

Ukaushaji wa viazi vitamu kwa ujumla wake huhitaji au hutumia nishati ya jua ambapo ni lazima mkulima kuzingatia kanuni  kwa ajili ya kukausha mazao yake.

Kanuni muhimu za ukaushaji

Ukaushaji hupunguza maji kwenye zao la viazi vitamu ambayo yakiwepo husaidia ukuaji wa vimelea vya magonjwa na kusababisha kuoza.

Ukaushaji hupunguza maji kwa kiasi kikubwa na kuwezesha hifadhi ya muda mrefu.

Ukaushaji utategemea hali ya unyevu hewani na hufanikiwa vizuri iwapo unyevu kwenye hewa ni mdogo.

Viazi vitamu vina vimeng’enyo ambavyo husababisha upotevu wa rangi, virutubishi na ladha wakati wa kukausha hivyo inashauriwa kuzui hali hiyo kwa njia ya kuchemsha kidogo kabla ya kukausha.

Mambo ya kuzingati katika ukaushaji bora

  • Viazi vikatwe katika vipande vyenye unene, upana na urefu usiozidi sentimita 6. Ukubwa wa vipande ukizidi huo ulioshauriwa ukaushaji huchukua muda mrefu na mara nyingi ubora wa bidhaa hushuka.
  • Tandaza viazi katika kina kinacholingana ili ukaukaji uwe wa pamoja. Usiongeze viazi vibichi juu ya vile ambavyo vimeanza kukauka kwenye kaushio.
  • Acha viazi vipoe baada ya kuvitoa katika kaushio kabla ya kufungasha.

Vifaa

Wakati wa ukaushaji wa viazi vitamu, vifaa vinavyohitajika ni pamoja na kaushio bora, kisu kikali kisichoshika kutu na mabeseni.

Malighafi

Malighafi ni pamoja na viazi vitamu na maji.

Jinsi ya kukausha

  • Chagua viazi vilivyo bora kisha osha vizuri kwa maji safi na salama.
  • Menya kwa kutumia kisu kikali kisichoshika kutu na katakata ili kupata vipande vyenye unene upatao sentimita 6.
  • Tumbukiza vipande kwenye maji yanayochemka kisha chemsha kwa muda wa dakika 3 hadi 5 ili kuzuia vimeng’enyo vinavyoweza kubadili rangi ya viazi.
  • Ipua na acha ipoe kisha anika kwenye kaushio bora kwa kutandaza vizuri ili kila kipande kipate jua sawa.
  • Viazi huweza kukauka kwa saa 6 hadi 7 kutegemeana na nguvu ya jua.
  • Kausha viazi hadi vifikie asilimia 9 ya unyevu na acha vipoe kisha fungasha kwenye mifuko ya plastiki na hifadhi sehemu baridi na kavu.
  • Viazi hivi huweza kuhifadhika kwa muda wa mwaka mmoja au zaidi bila kuharibika.

Matumizi

  • Hukaangwa au kuchemshwa na kuliwa.
  • Huchanganywa na vyakula vya mikunde kupata mlo.
  • Husagwa pia kupata unga.

Kusindika viazi vitamu kupata unga

Vifaa

Kisu kikali kisichoshika kutu, mabeseni, jiko, kaushio bora, mashine ya kusaga na mifuko ya plastiki.

Mahitaji

Viazi vitamu visafi visivyooza pamoja na maji safi na salama.

Jinsi ya kuandaa

  • Osha viazi vizuri kisha menya na katakata vipande vidogovidogo vya milimita 6.
  • Chemsha kwenye maji yenye nyuzi joto 90 za sentigredi kwa muda wa dakika 3 hadi 5 kisha ipua na chuja maji.
  • Kausha kwenye kaushio borakisha saga kwa kutumia mashine kupata unga.
  • Fungasha unga kwenye mifuko ya plastiki na hifadhi mahali safi, pakavu na ubaridi
Unga uliosagwa wa viazi vitamu

Matumizi

Unga huu wa viazi vitamu hutumika kupikia vyakula mbalimbali kama vile mikate, biskuti, keki, vyakula vya watoto na kuongezwa kwenye sosi kama kiongeza uzito.

Kusindika viazi kupata wanga

Vifaa

Mabeseni ya kuoshea, mashine ya kukwangulia viazi, mapipa ya kutulizia wanga, sehemu ya kukaushia na visu vikali vya kumenyea viazi vitamu.

Jinsi ya kutengeneza

  • Menya viazi vitamu kwa kutumia kisu kikali kisichoshika kutu.
  • Osha viazi kwa kutumia maji safi kisha kata vipande vidogo.
  • Saga au parua kwa kutumia mashine ili kupata rojo kisha ongeza maji kwenye rojo.
  • Acha yatulie kisha mwaga maji na ongeza tena maji na kuacha yatulie kisha kumwaga tena.
  • Fanya hivyo hadi uone rangi yote inatoka na maji yamekuwa meupe kabisa.
  • Mimina wanga kwenye kitambaa safi cheupe kisha kamua maji.
  • Anika wanga kwenye kaushio bora katika sehemu safi.
  • Saga wanga kwa mikono kulainisha mabonge yake.
  • Chekecha kwenye chekeche laini kisha fungasha kwenye mifuko ya plastiki.
  • Hifadhi sehemu safi, kavu, na isiyokuwa na mwanga mkali.

Matumizi

Wanga huu hutumika kuongeza uzito kwenye mchuzi, sosi na kuwekwa kwenye nguo viwandani.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *