Ninataka kufuga nyuki wadogo, kwa kuwa nasikia wana faida kubwa sana, lakini sijui namna ya kuwapata na jinsi ya kuwatunza, naombeni msaada-Msomaji MkM
Nchini Tanzania na maeneo mbalimbali barani Afrika, imekuwa ni mazoea kwa wanaotaka kufanya ufugaji wa nyuki kufuga nyuki wakubwa au maarufu kama nyuki wakali.
Aina hii ya nyuki imekuwa ni rahisi kufugwa kwa kuwa uzalishaji wake ni mkubwa zaidi na wanaweza kufugwa kwenye maeneo tofauti tofauti ili mradi kuwe na mahitaji muhimu yanayowawezesha nyuki kuzalisha.
Nyuki wakubwa wanaweza kufugwa katika mapori, shambani, na hata katika nyumba maalumu ambazo hujengwa na kuwekwa mizinga kwa ajili ya uzalishaji wa asali kisasa.
Nyuki wadogo
Tofauti na ilivyo kwa nyuki wakubwa, aina hii ya nyuki ni kundi dogo sana katika jamii ya wadudu wanaozalisha asali.
Nyuki hawa wana umbo dogo sana na rangi nyeusi, na uzalishaji wao huwa ni mdogo ukilinganisha na aina nyinginezo za nyuki.
Aina hii ya nyuki tofauti na ilivyo kwa nyuki wakubwa, majike yote huzaa, huku madume yakifanya kazi kama nyuki wengine, ambapo nyuki jike huleta malighafi na madume hufanya kazi ya kujenga.
Kazi ya kuzalisha asali kwa nyuki hawa wadogo, hufanywa kwa ushirikiano wa wote bila kubaguana.
Asali inayotokana na nyuki hawa, ina aina nyingi zaidi za virutubisho kwa kuwa huweza kupata chavua kutoka katika aina nyingi zaidi za maua kwani huweza kuingia hata kwenye maua madogo zaidi ambayo nyuki wakubwa hawawezi kuingia kwa ajili ya kupata chavua ambayo hutumika kutengeneza asali.
Mahali pa kufugia
Nyuki wakubwa(wanaouma) wanatakiwa kufugwa eneo ambalo liko umbali wa mita 300 kutoka maeneo ambako kunafanyika shughuli za binadamu kwa sababu wakiwa karibu na makazi ya watu wana tabia ya kuwashambulia watu kutokana na kuwa hawapendi usumbufu.
Hii ni tofauti kwa nyuki wadogo, ambao hufugwa katika makazi ya watu bila kuwa na madhara ya aina yoyote.
Mandhari
Ni muhimu kuzingatia kuwa, eneo utakalofugia nyuki wadogo linakuwa na mahitaji muhimu kama vile:
- Kivuli cha kutosha
- Eneo lisiwe na joto kali. Hii ni kwa sababu nyuki hawa wana asili ya milimani ambako kuna baridi.
- Kusiwe na upepo mkali na eneo lisiwe la wazi sana wasipigwe na jua la moja kwa moja.
- Kuwa na maji karibu sana na ulipo mzinga. Hii ni kwa sababu nyuki hawa hawana uwezo wa kwenda mbali kutafuta maji kama ilivyo kwa nyuki wakubwa.
Mzinga
Nyuki wadogo wanaweza kufugwa kwenye mizinga ya kawaida ya asili na hata ya kisasa.
Wafugaji wanashauriwa kutumia mizinga rahisi kulingana na mazingira waliyopo. Ingawa, mizinga ya pembe nne (Square) inafaa zaidi kuliko ile ya bomba (cylinder).
Mizinga ya pembe nne inarahisisha zaidi ugawaji wa makundi. Ili kuwa na kizazi endelevu ni lazima mfugaji azingatie ugawaji wa makundi katika mizinga yake, kwa kuwa nyuki hawa huzaliana taratibu sana.
Ukubwa wa mzinga, uwe kulingana na ukubwa wa kundi la nyuki ulilonalo kwani huzalisha kutokana na ukubwa wa kundi.
Unaweza kutundika mizinga ya nyuki wadogo kwenye paa la nyumba pembezoni mwa ukuta au kwenye miti inayozunguka nyumba (Tazama picha)
Faida za nyuki wadogo
- Asali na mazao mengine ya nyuki
- Husaidia kuchavusha mimea. Baadhi ya mimea kama vile vanilla huchavushwa na nyuki wadogo pekee.
- Huzalisha gundi
Matumizi ya asali ya nyuki wadogo
- Hutumika kama chakula
- Hutumika kama dawa ya kikohozi.
- Dawa ya vidonda.
- Ni chakula muhimu kwa watu waliovunjika kwani husaidia kulainisha mifupa hivyo kufanya uungaji kuwa wa haraka.
- Hutumika kuhifadhia vyakula vinavyoharibika haraka kama vile nyama.
- Hutumika pia kuhifadhi vyakula vya watu wanaosafiri kwa muda mrefu kama vile mabaharia.
- Hutumika kwenye viwanda vya ngozi kwa ajili ya kulainisha ngozi.
Nahamishaje Kundi la Nyuki wadogo waliokatika ukuta wa mlango kwenda kwenye mzinga?