Miti ya malisho ni chanzo rahisi cha protini kwa ng’ombe wa maziwa. Miti hii hutoa chakula chenye protini ya kutosha katika msimu wote wa mwaka. Wafugaji wanaweza kuokoa pesa endapo watapanda miti ya malisho jamii ya mikunde kama vile desmodium na lusina. Miti ya malisho pia husaidia kuboresha udongo kwa kutoa matandazo ya kijani au kuongeza nitrojeni kutoka hewani.
Kaliandra: Hustawi vizuri zaidi kwenye ukanda wa juu na wenye mvua nyingi (700-2000mm).
Lusina: Lusina hustawi vizuri kwenye ukanda wa juu wenye mvua kiwango cha kati na cha juu. Aina hii huvumilia ukame kwa kiwango kikubwa lakini ni rahisi kushambuliwa na wadudu na magonjwa. Huchipua vizuri baada ya kukatwa na kuvunwa.
Sesbania: Hustawi vizuri zaidi kwenye ukanda wenye mvua nyingi, na huwa na ufanisi kuliko aina nyinginezo kwenye ukanda wa juu na wenye baridi. Kwenye hatua za mwanzo hukua kwa haraka zaidi kuliko kaliandra au lusina, lakini haikui tena baada ya kuvunwa.