Umoja ni nguvu na wakulima wanapoungana pamoja, mambo mazuri hufanyika. Wanatiana nguvu, kuleta rasilimali pamoja na kuanzisha miradi ambayo ni ngumu kwa mkulima mmoja kuanzisha.
Kikundi cha Shangushangu kilichopo kijiji cha Narunyu, kata ya Tandangongoro, mkoani Lindi lina wanachama 16 (wanawake 8 na wanaume 8) na kilianzishwa mwezi wa saba mwaka 2023 likiwa na lengo la kujifunza kilimo na ufugaji kwa mbinu bora za kilimo hai.
Wanachama wote wa kikundi hiki wanatoka katika kijiji cha Narunyu, na walipata hamasa ya kuunda kikundi baada ya kupata uelewa wa kilimo hai kutoka Mkulima Mbunifu, hasa kuhusu kubadilisha mkondo na kupunguza na kuzalisha bidhaa za kilimo na mifugo zisizokuwa na viambata sumu ili kuimarisha afya ya walaji. Pia, wanachama waliona urahisi wa utekelezaji wa aina hii ya kilimo kwa kuwa kwa asilimia kubwa kinatumia malighafi zinazopatikana shambani na zinazomzunguka, na kwa kufanya hivi mkulima anapunguza gharama za uzalishaji. Hii inamaanisha kwamba mkulima anazalisha chakula salama kwa gharama ya chini na kujiongezea kipato.
Shughuli za kikundi
Kikundi hiki kinajihusisha na ufugaji wa kuku na kilimo cha mazao ya msimu kama mahindi, mbaazi, ufuta, alizeti na mikunde. Kuku wanafugwa katika banda la kikundi lililojengwa kwa nguvu zao wenyewe na walianza na kuku 100. Kuku hawa walipokomaa, waliuzwa na fedha zilizopatikana ziliweza kutumika kununua kuku wengine, wakiongeza idadi na kufikia kuku 200.
Misingi ya kilimo hai
Mfumo wa ulishaji unaotumika ni kulisha vyakula maalumu kwa muda wa wiki nne kisha kutengeneza mchanganyiko kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika mazingira ya wafugaji kama vile mbaazi, kunde, mashudu ya alizeti, mahindi na kadhalika.
Kwa upande wa magonjwa, wanatumia dawa za asili kama vile kitunguu saumu, tangawizi, majani ya mpapai, mlonge, na chanjo kwa magonjwa hatari kama vile kideri.
Malengo ya kikundi
- Kufikisha kuku 500 ifikapo Disemba 2025.
- Kila mwanakikundi kumiliki mradi wa ufugaji wa kuku 100 kufikia mwaka 2027.
- Kuanzisha kilimo cha bustani kitakachosaidia uchumi wa kikundi pamoja na uhakika wa upatikanaji wa mboga mboga kwa kuku na matumizi ya nyumbani.
Dawa za asili kwa kuku
- Urahisi wa upatikanaji kwa kuwa dawa zinazotumika zipo katika mazingira ya wafugaji.
- Urahisi katika maandalizi na usalama kwa kuwa si hatarishi kwa afya ya kuku na binadamu.
- Mbali na kutumika kama tiba, hutumika kama sehemu ya lishe. Mfano, tangawizi hutumika kama tiba dhidi ya mafua ya kuku na ni chanzo cha Vitamin C ambayo ni muhimu kwa kuhimarisha kinga ya mwili ya kuku. Majani ya mpapai ni chanzo cha Vitamin muhimu hasa nyakati za kiangazi ambapo asilimia kubwa ya nyasi huwa zimekauka.
Faida kutokana na Mkulima Mbunifu
- Jamii imepata hamasa na uelewa kuwa kuku wanaweza kufugwa kwa njia za asili na kupata matokeo chanya.
- Kikundi kimetengeneza ajira kwa jamii, mfano, huwa wananunua malighafi mbalimbali za kutengeneza chakula cha kuku. Wananunua makaa kwa ajili ya kupasha joto vifaranga. Pia, kuna wanunuzi wa kuku ambao wanaenda kukaanga na kuuza vipande kwa wateja wao. Kwa kufanya hivyo, wanaunda nafasi za biashara na kwa wanajamii wanaojipatia kipato.
- Mradi umekuwa ni chanzo cha kupata mbolea ya uhakika isiyokuwa na viambata sumu kwa wakulima wa bustani. Baada ya kumaliza mzunguko wa uzalishaji (baada ya kuuza kuku), matandazo huondolewa na kutumika kama mbolea shambani.
- Kupitia mradi huu lishe kwa wanajamii imeimarika kwa kuwa kuku na mayai ni chanzo kizuri cha protini inayohitajika kwa ukuaji bora wa mwili.
Faida kiuchumi
Kupitia mradi huu, kikundi kimepata fedha kwani mwezi wa Mei mwaka huu walifainikiwa kuuza jumla ya kuku 99 na hela TShs 1,323,000, faida ikiwa TShs 500,000. Hii ni baada ya kuondoa gharama zote za uzalishaji. Faida hiyo imewawezesha kuongeza idadi ya kuku na kuendelea kupanua mradi.
Kwa mawasiliano na kikundi hiki cha Shangushangu kupitia John Cosmas Ng’habi kwa simu 0689081581 au barua Pepe: johncosmasnghabi@ gmail.