- Mifugo

Matatizo katika ufugaji wa kuku wakienyeji

Sambaza chapisho hili

Tija katika ufugaji wa kuku wa asili ni ndogo kwa sababu ya matatizo mengi wanayokumbana nayo.

Katika mazingira ya kujitafutia chakula kuku hawa hukumbana na vimelea mbalimbali vya magonjwa. Kwa ujumla kuku hawawezi kuongezeka kwa idadi kubwa mahali pasipo na vyakula vya kuwatosheleza hata kama magonjwa hatari yatadhibitiwa kwakuwa mwishowe watakufa kwa kukosa chakula.

 

Magonjwa yanayoathiri kuku wa kienyeji
Ugonjwa wa Mdondo/Kideri
Ugonjwa huu ambao husababishwa na virusi huathiri kuku wa rika zote wasiochanjwa, na kusababisha vifo hata kumaliza kundi lote la kuku.

Hutokea zaidi wakati wa kiangazi hasa miezi ya Mei hadi Septemba japo waweza kutokea wakati wowote wa mwaka.

Udhibiti
Ugonjwa huu unazuilika kwa chanjo. mf. I-2 na Lasota. Chanjo ya I-2 inafaa kutumika katika mazingira ya vijijini kwa kuwa inavumilia joto la kati ya 14-29◦C kwa siku 14. Chanjo hutolewa kila baada ya miezi 3 au minne 4 kwa njia ya tone katika jicho moja tu la kuku. Vifaranga wanaototolewa kabla ya muda wa chanjo hutakiwa kuchanjwa wafikapo umri wa siku 14 na kisha kuingizwa katika ratiba ya uchanjaji wa kundi la wakubwa. Chanjo ya I-2 kama ilivyo chanjo zingine hutolewa kwa kuku waliowazima.

Upungufu wa Vitamini A
Huathiri vifaranga na kuku wanaokua.

Vifaranga wadogo hufa ghafla chini ya wiki tatu tangu kutotolewa na wale wanaovuka muda huo huvimba macho, hushindwa kula na hatimaye hufa. Jicho lililovimba hutoa uchafu mithili ya kipande cha sabuni kilicholowekwa. Wengine hufa kwa kushindwa kula kutokana na kutoona.Ugonjwa hujitokeza wakati wa kiangazi kutokana na kukosekana kwa majani mabichi na wadudu hivyo kusababisha kuku kutaga mayai yenye upungufu mkubwa wa vitamini A. Vifaranga wanaototolewa hukumbwa na ukosefu wa vitamini na kadri wakuavyo mahitaji huongezeka zaidi na kusababisha macho kuathirika.

Udhibiti
Tumia vitamini mchanganyiko za madukani ambazo zina kiwango kikubwa cha Vitamini A kwa kuwapa kuku wanaotarajia kutaga na pia vifaranga baada ya kutotolewa. Kuwapa kuku majani na mchicha kutoka bustani ni wakati wa kiangazi pia husaidia.

Ndui ya kuku
Huathiri kuku wa rika zote japo wadogo huathirika zaidi na kufa zaidi. Kuku huonesha vipele katika maeneo yasiyo na manyoya na kisha hutoa maji na kuacha vidonda ambavyo hatimaye hujenga kovu kwa baadhi ya kuku wanaopona. Ugonjwa hujitokeza zaidi wakati wa kiangazi na mwanzoni mwa msimu wa mvua. Husababishwa na virusi vijulikanvyo kama fowl pox virusi ambavyo huingia kupitia kwenye ngozi dhaifu.

Udhibiti
Huzuiwa kwa chanjo inayochomwa kwa sindano maalum katika mabawa ya kuku. Kuku wanaopewa kiwango kizuri cha vitamini A, matukio ya ndui huwa ni machache kutokana na kuwa na ngozi imara. Ni vyema kuwalisha kuku vyanzo mbalimbali vya vitamini A ili kuzuia ugonjwa wa ndui na magonjwa mengine.

Minyoo ya kuku
Kuku huathiriwa na minyoo mviringo pamoja na minyoo bapa. Minyoo hatari kiuchumi kwa kuwa inanyonya chakula cha kuku kwa wingi na hatimaye kusababisha vifo vya kuku wadogo, na hata wakubwa. Minyoo hupunguza uzalishaji wa kuku kuanzia kutaga mayai na kushindwa kutotoa.

Udhibiti
Dawa aina ya Piperazine inapatikana katika maduka ya dawa za mifugo na huuwa minyoo ya duara ambayo huu wa zaidi kuku kuliko minyoo mingine ya kuku. Ni vema kuku wa asili kupewa dawa za minyoo mara moja kila baada ya miezi mitatu na wiki moja kabla ya chanjo ya I-2. Maelekezo ya kuchanganya dawa na maji yatatolewa kwa mtaalam katika duka la dawa za mifugo kwa kuwa mchanyiko wa maji na dawa hutegemea ukali wa dawa ilivyotengenezwa.

Wadudu wa nje wa kuku
Wadudu wa nje wa kuku huhusisha viroboto, chawa na utitiri, ambao hunyonya damu kwa kuku, husababisha usumbufu kwa kuku wanaotaga na wanaoatamia na husababisha vifo vya vifaranga.

Udhibiti
Wadudu wa nje hudhibitiwa kwa kutumia njia za asili kama vile kumwaga majivu na majani ya miti katika banda na viota vya kutagia.

Pia kwa kutumia dawa za madukani za kuua wadudu kama vile Akheri powder® au Sevin dust®. Kwa kuua viroboto wang’ang’aniao dawa hizi huchanganywa na mafuta mgando ili iweze kushika vizuri. Ujenzi wa mabanda ya chaga za juu na kuta zinazopitisha hewa ya kutosha na kuzingatia usafi wa banda pia husaidia kudhibiti wadudu.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *