Mbuzi wa maziwa ni aina ya mbuzi ambao hufugwa kwa lengo kubwa la kupata maziwa. Mbuzi hawa wapo wa aina mbalimbali kama vile, Saanen (Switzerland), Norwegian (Norway), Toggenburg (Switzerland), Anglonubian (Chotara kutoka Misri, Sudan, India na Switzerland), Alpine (Ufaransa na Switzerland) na wote hawa wanapatikana Tanzania.
Ulishaji sahihi wa mbuzi wa maziwa ni lazima uzingatie mambo makuu yafuatayo;
- Lishe bora
Lishe bora ni muhimu kwa mbuzi wa maziwa kwani humfanya aweze kuishi, kukua na kutoa maziwa mengi na yenye ubora. Maziwa hutengenezwa na viinilishe vitokanavyo na vyakula anavyokula mbuzi pamoja na maji safi na ya kutosha anayokunywa.
Ukosefu wa lishe bora husababisha mbuzi kudhoofika, ukuaji wake kuathirika, utoaji wa maziwa kupungua, kutoshika mimba, kuugua mara kwa mara na hata wakati mwingine kufa.
Kukua vizuri, kutoa maziwa mengi, kutokuugua mara kwa mara na uzazi mzuri ni mambo yanayohitaji lishe ya hali ya juu na ya kutosha. Lishe bora ni lazima iwe na viinilishe vifuatavyo;
- Wanga na sukari kwa ajili ya kutia nguvu mwilini.
- Protini ya kutosha.
- Madini na Vitamini.
- Maji safi naya kutosha.
- Mahitaji ya mbuzi wa maziwa
Mahitaji ya chakula kwa mbuzi wa maziwa hutegemea mambo yafuatayo;
Umri au uzito wake, kiasi cha maziwa anachotoa mbuzi kwa siku, hali yake (yaani ana mimba au la/anakua au hakui tena) na mbuzi wazazi yaani wanapokaribia kupandwa/kupanda na wakati wanapokaribia kuzaa.
Umri au uzito
Chakula halisi cha mbuzi mdogo ni maziwa. Lakini ili tumbo lake liweze kukua vizuri ili hapo baadaye awe na uwezo mkubwa wa kula majani.
Lishe sahihi kwa mbuzi wa maziwa ni lazima apewe majani mazuri na laini katika umri mdogo. Mbuzi wenye uzito mkubwa wanahitaji chakula kingi kuliko mbuzi wenye uzito mdogo hata kama ubora wa lishe wa chakula hicho ni sawa.
Kiasi cha maziwa
Maziwa mengi hutokana na lishe bora na ya kutosha hivyo ni lazima mbuzi mwenye uwezo wa kutoa maziwa mengi apewe chakula kingi na bora zaidi kuliko mbuzi mwenye uwezo mdogo.
Hali yake
Mbuzi mwenye mimba huhitaji nyongeza kidogo ya malisho ukilinganisha na mbuzi asiye na mimba hasa kama hakamuliwi. Baadhi ya mbuzi hushika mimba wakiwa bado wadogo na hivyo huendelea kukua hata wakati ule wanapokuwa na mimba. Mara nyingi hali hii hutokea kwa wale mbuzi wanashika mimba kwa mara ya kwanza tangu kuzaliwa.
Kutokana na ukweli huu, ni sharti mbuzi mwenye mimba alishwe chakula kizuri zaidi kwani kinahitajika kwa ajili ya ukuaji wake yeye mwenyewe na vilevile kwa ajili ya ukuaji wa mimba.
Mbuzi wazazi
Wakati wa uzalishaji, mbuzi jike au dume anastahili kupewa chakula zaidi ilia pate viinilishe vya kumwezesha kupata mimba au kutoa mbegu hai kwa wakati unaostahili. Pia mbuzi anapokaribia kuzaa apewe chakula cha ziada ili kumwandaa kutoa maziwa mengi na kumlisha mtoto anayekua tumboni.
- Vyakula vya mbuzi wa maziwa
- Malisho
Malisho yawe yametokana na nyasi au mikunde kwani ndicho chakula cha asili na rahisi cha mbuzi. Ili kupata matokeo mazuri, hakikisha malisho yamo kwenye hori la mbuzi wakati wote na pia mbuzi wa maziwa anaweza kuchungwa kwenye eneo lenye malisho mazuri.
Nyasi
Ziko nyasi za asili na za kigeni na nyasi nyingi hupatikana kila mahali ingawaje hutofautiana kwa ubora na uwingi. Nyasi za asili ni pamoja na panicum, brachiaria, nyasi za molasi, cenchrus na makengera. Nyasi za kigeni ambazo hupandwa nchini ni pamoja na guatemala, maji ya tembo, setaria, rhodes grass, edible canna, canna lilies na kikuyu grass.
Mikunde
Malisho ya jamii ya mikundeHuboresha lishe ya mbuzi na hupatikana sehemu nyingi hapa nchini. Mikunde ya asili ni pamoja na fundofundo, kudzu, siratro, desmodium, stylo, na centrosema.
Mikunde ya kigeni ni pamoja na alfalfa (lusina), blue pea, clover, desmodium, velvet bean (ngwala kubwa) na lablab (fiwi).
Miti ya malisho
Miti ya malisho hupendwa sana na mbuzi kuliko hata nyasi na mikunde.
Thamani ya miti lishe haipungui hata kama ni wakati wa kiangazi. Baadhi ya miti huendelea kustawi na kutoa malisho mazuri wakati wa kiangazi.
Ipo miti ya kawaida ya malisho kama vile lantana na ipo miti ya malisho ya jamii ya mikunde kama vile lukina na sesbania. Miti ya malisho ya asili ni pamoja na sesbania, lantana, acacia, na jamii nyingi za lukina. Miti ya malisho ya kigeni ni pamoja gliricidia, caliandra, flemingia, miparachichi, mifenesi na jamii kadhaa ya lukina.
Mabaki ya mazao
Mabaki ya mazao kama vile mabua ya mahindi, makapi ya maharagwe, majani ya mpunga au ngano yanafaa na yanatumika sana kulishia mbuzi hasa wakati wa kiangazi. Kwa wakati huo majani hukosekana kabisa na kama yakiwepo basi kuna uwezekano mkubwa wa kuwa haba au hafifu.
Kwa bahati mbaya malisho haya sio mazuri sana ukilinganisha na nyasi, mikunde au miti ya malisho hivyo huhitaji kuboreshwa.
Jinsi ya kuboresha mabaki ya mazao
Ziko njia nyingi za kuboresha mabaki ya mazao kabla ya kuyatumia kama
malisho ya mifugo ikiwa ni pamoja na kusindika mabua kwa kutumia urea.
Aidha, njia rahisi zaidi inayoweza kwa kila mfugaji ni pamoja na kuchukua mabaki ya mazao kama yalivyo bila kukatakata kisha kunyunyizia maji yenye magadi au chumvi kisha kumpa mbuzi ale kwa wingi atakavyoweza.
Kwa kawaida mbuzi anapokula huchagua sehemu zile zilizo laini na nzuri zaidi kama majani. Na kwa kutumia maji, sehemu kavu za mabaki ya mazao kama vile mabua hulainika huku chumvi au magadi vikiongeza utamu wa mabaki hayo na kumfanya mbuzi kula kwa wingi zaidi.
Halikadahalika, baada ya mbuzi kula, mabaki hayo yanaweza kutumika kulishia wanyama wengine kama vile ng’ombe wasiokamuliwa, maksai na punda au kutumika kutengenezea mboji.
Wakati wa mavuno inashauriwa kuyatoa mabaki ya mazao shambani
mapema kabla ya kuwa makavu sana.
Mabaki hayo yakitolewa mapema kiasi hicho na kuhifadhiwa, yataweza kuliwa na mbuzi kwa urahisi na kwa wingi zaidi.
- Ulishaji bora wa malisho
Malisho ya aina yoyote yawe ni nyasi, mikunde, miti ya malisho au mabaki ya mazao ni muhimu yalishwe ya kutosha ili mfugaji aone matokeo mazuri ya kufuga mbuzi wa maziwa.
Ili mbuzi ale malisho kwa wingi, changanya nyasi na mikunde, au mabaki ya mazao na mikunde kama fundofundo na lukina.
Mikunde isilishwe peke yake kwani ikilishwa kwa wingi bila kuchanganywa na malisho mengine huweza kuleta madhara.
Inashauriwa kwamba ili mbuzi wa maziwa awe amekula chakula cha kutosha ni lazima apate malisho kati ya asilimia 4 hadi 5 ya uzito wake.
Ili uweze kukaribia kipimo hicho, usimpe mbuzi majani mara tu baada ya kuyakata kwa vile yatakuwa na kiasi kikubwa cha maji. Hivyo jaribu kuyanyausha kidogo ili maji yaliyopo yapungue kabla ya kumlisha mbuzi.
Nawezaje kunenepesaha mbuzi wa nyama
Habari, Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa swali lako.
Ndiyo, unaweza kunenepesha na watafanya vizuri sana