Nyuki wadogo huitwa kwa jina maarufu la nyuki wasiouma. Nyuki hawa wana umbo dogo kulinganisha na nyuki wanaouma lakini pia kila kabila katika Tanzania huwa na majina yake kama nyori, mbuyaa, mpunze, n.k.
Mzinga uliotegeshwa katika tundu wanaoingilia nyuki wadogo ardhini kwa lengo la kuwaokoa toka ardhini kuingia kwenye mzinga huo.
Nyuki hawa pia hutofautiana kulingana na meneo wanayopatikana. Wapo wanaopatikana maeneo ya vichuguu, wapo wanopatiakana maeneo ya pembezoni mwa barabarara, wapo wanaopatikana katika magogo, wapo wanaopatikana katika kuta za nyumba
Aina za nyuki wadogo
Kuna aina nyingi za nyuki wadogo wanaopatikana Tanzania. Nyuki hawa wamegawanyika katika makundi takribani kumi na moja, mengine bado hayajatambuliwa au tafiti hazijajitosheleza.
Makundi yaliyopatikana
Meliponula feruginea: Nyuki hawa wameonekana maeneo ya Siha, Sanya juu na Ngarenanyuki. Nyuki hawa ni weusi kwa rangi, huweza kuweka asali kutokana na ukubwa wao. Pia huweza kupata chavua kwa wingi na ni nyuki rahisi kugawanywa.
Hypotrigona ruspulii: Nyuki hawa wamepatikana maeneo ya kusini mwa Tanzania Iringa, Mafinga hupendelea misitu yenye baridi na hukaa juu zaidi ya miti mikubwa yenye matundu. Nyuki hawa hutengenza vyungu vingi vya asali na huwa na akiba ya muda mrefu zaidi ya chakula kuliko nyuki wadogo wengine.
Plebeina hildebrant: Hawa wanapatikana Arusha maeneo ya Njiro, Muriet na Eengutoto katika maeneo ya vichuguu. Nyuki hawa wana umbo dogo zaidi hutengeneza vyungu vya asali karibu na nyumba yao na vyungu vyao (masega) huwa vidogo sana lakini wana asali tamu zaidi
Meliponula ogounesis: Nyuki hawa wamepatikana maeneo ya Buger, Marang na Ayalalio Karatu. Nyuki hawa ni wakubwa, huweza kutengeza asali nyingi na vyungu vyao vya asali huwa vikubwa zaidi
Kwanini tuokoe makundi ya nyuki
- Hatari ya kupotea kwa baadhi ya aina ya nyuki wadogo kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo zile zinazochangiwa na binadamu kama kilimo kinachotumia kemikali za viwandani ambazo hasa huathiri majani ya nyuki pale ambapo nyuki wafanyakazi huenda kutafuta chavua katika maua yaliyopuliziwa kemikali.
- Urinaji wa asali unaofanywa kiholela na kuacha makundi ya nyuki yakiwa hayana makazi wala chakula.
- Uchomaji moto wa misitu unaochangia kupoteza makundi haya ya nyuki.
- Faida itakayopatikana kutokana na nyuki hawa endapo wataokolewa, kuwekwa kwenye mizinga na kuanza kufugwa kwa mazingira safi na salama.
Unawezaje kuokoa kundi la nyuki wadogo wa chini?
Mara nyingi watu wamekuwa wakijiuliza, ni kwa namna gani nyuki wadogo wa chini wanaweza kuokolewa na kufugwa kama nyuki wa kwenye magogo.
Vifaa
- Brashi la rangi, jipya na la saizi ya kati
- Beleshi
- Jembe
- Waya wa kukunjika
Namna ya kufanya
- Tafuta mlango au mdomo ambapo nyuki wanatokea. Mara nyingi huwa na mnato fulani wa gundi asili ambayo wao huiweka kuwakinga na maji na wadudu maadui.
- Tumia waya unaokunjika kuweka katika mdomo wa shimo .
- Anza kuchimba na jembe kufuata waya kwa taratibu huku ukiangalia mikunjo ya njia inayokupeleka katika nyumba ya nyuki.
- Tumia beleshi kutoa udongo taratibu bila kuugusa waya.
ANGALIZO: Usitumie nguvu kubwa kuchimba usije ukagusa nyumba ya nyuki na kuharibu seli za mayai na majana.
- Mara baada ya kufikia sehemu yenye nyumba ya nyuki wadogo, chukua nyumba yote na weka kwenye mzinga tayari kwa ajili ya ufugaji.
KUMBUKA: Nyumba ya nyuki wadogo wa chini haipaswi kuvunjwa wakati wa kuwekwa kwenye mzinga kwani lazima waendelee kuzoea hali ya mzinga mpya wakiwa katika nyumba yao ya zamani.
Faida za ufugaji, uhifadhi na uendelezaji wa makundi ya nyuki zinazolengwa na mradi huu
- Kuongeza idadi ya nyuki na kuwagawanya kila wanapokuwa wameongezeka. Hii itapelekea kuwa na nyuki wengi ambao wanasaidia katika shughuli za uchavushaji na kuhakikisha usalama na uhakika wa chakula.
- Uvunaji wa bidhaa za nyuki kama asali, gundi na chavua.
- Kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na nyuki ikiwa ni pamoja na sabuni zitokanazo na nta na asali, mishumaa itaokanayo na nta, pamoja na mafuta ya kupakaa ambayo yanatokana na nta
- Uuzaji wa mizinga na mbegu za nyuki wadodgo Kuwepo kwa wageni wanaohitaji kujifunza juu ya nyuki na tabia zake na aina zake
Wito kwa wadau na serikali
- Kufanyike tafiti nyingi zaidi kuhusu ufugaji wa nyuki hasa wadogo na kujaribu kulinganisha njia za jadi za kuendeleza makundi ya nyuki na kuziboresha.
- Kufanyike mafunzo zaidi juu ya bidhaa zitokanazo na nyuki na uchakataji wake kwa kukidhi viwango vya ndani na nje ya nchi
Kwa maelezo Zaidi kuhusu Makala hii wasiliana na Daudi Ngosengwa Manongi, Mtaalamu wa nyuki na kilimo ekolojia, Simu namba 0769861063
Mm naishi mafinga nimesoma kwamba mafinga nyuki wasiouma wanapatikana juu ya mapango ya miti.Lakini Mimi nimeaanza kufuga hao nyuki na nimewapata kwenye vichuguu hapa mafinga je hao Nia sina gani?
Mm naishi mafinga nimesoma kwamba mafinga nyuki wasiouma wanapatikana juu ya mapango ya miti.Lakini Mimi nimeaanza kufuga hao nyuki na nimewapata kwenye vichuguu hapa mafinga je hao Ni aina gani? Pili nikitaka kwenda kuwa fuga dar watastahimili na kunipa asali
Habrai, karibu sana Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za Mkulima Mbunifu.
Hongera kwa kuanza ufugaji wa nyuki. Hao ni nyuki wasiouma ambao wanapatikana pia kwenye vichuguu siyo kwenye miti pekee. Unaweza kwenda kufuga lakini kikubwa ni lazima kuangalia eneo lenye uwezekano wa kuwapatia chakula kwa ajili ya uchavushaji wa asali.