- Kilimo, Kilimo Biashara

Maharagwe machanga hushamirisha uchumi

Sambaza chapisho hili

Hivi karibuni hapa nchini Tanzania, kumekuwa na uanzishaji na uendelezaji wa kilimo cha mazao mapya ambayo hayakuzoeleka hapo awali. Moja ya mazao hayo ni pamoja na maharagwe machanga, maarufu kama Green beans au French beans.

Mbegu Inapendekezwa kutumia chotara aina ya F1. Aina hii ya mbegu imeonekana kuwa na mafanikio makubwa zaidi ikiwa ni pamoja na uwezo wa kumudu magonjwa. Inapendekezwa kupata mbegu kutoka kwa wazalishaji walioidhinishwa.

Aina za mbegu na uwezo wake

  • Boston: Aina hii ya mbegu ina uwezo mkubwa wa uzalishaji. Wakati wa mvua aina hii ya mbegu hushambuliwa zaidi na magonjwa hasa ya ukungu.
  • Serengeti: Aina hii ina uzalishaji wa wastani. Aina hii ina uwezo mkubwa wa kuvumilia magonjwa.
  • Tana: Aina hii uzalishaji wake ni mkubwa na wa muda mrefu. Inashambuliwa na magonjwa kwa wastani. Aina hii huhitaji kiwango kikubwa cha maji hasa wakati wa mavuno.

Maharagwe machanga yamegawanyika katika makundi mawili;

  • Maharagwe mateke kwa wastani (fine beans)
  • Maharagwe mateke zaidi (extra fine beans)

Utayarishaji wa shamba

Lima shamba na kuondoa magugu yote. Hakikisha kuwa umelima kwa kiwango ambacho udongo umelainika vya kutosha. Kabla ya kupanda ni lazima uhakikishe udongo umelainika vizuri na una maji ya kutosha siku mbili kabla ya kupanda. Hii inategemeana na aina ya umwagiliaji, kwenye kilimo cha maharagwe machanga inapendekezwa zaidi kutumia umwagiliaji wa matone.

Kupanda

Inashauriwa kuweka nafasi ya sentimita 30 kati ya mstari na mstari, na kati ya mmea na mmea sentimita 7. Panda mbegu moja kwa kila shimo. Panda kwenye tuta na liwe na upana wa sentimita 70, kati ya tuta na tuta kuwepo nafasi ya sentimita 80.

Ni vizuri kuacha nafasi ya sentimita 15 kutoka pembeni mwa tuta unapopanda mbegu, ili kuepusha athari zinazoweza kutokea na kuathiri mbegu au mmea baada ya kuota, mfano, mafuriko.

Endapo unatumia umwagiliaji wa mifereji inashauriwa kutengeneza makingo yenye kimo cha sentimita 15 na upana wa sentimita 70 kutoka kingo hadi kingo. Hii itasadia mimea kupata unyevu kwa urahisi pamoja na kinga ya magonjwa yanayosababishwa na unyevu uliopitiliza.

Mbolea

Inashauriwa kutumia mbolea hai iliyoiva vizuri kiasi cha … kwa ekari moja. Pia, unaweza kupandia zinazotokana na miamba kama vile DAP. Tumia gramu 5 kwa kila shimo. Hii itasaidia mizizi kuota kwa haraka. Usifukie mbegu kwa zaidi ya inchi 1.5. Mbegu za maharagwe machanga huota baada ya siku saba. Endapo mbegu hazikuota vizuri unaweza kurudishia si zaidi ya siku mbili tangu maharagwe yote.

Umwagiliaji

Hii inategemeana na hali ya hewa/ msimu, kulingana na eneo ulipo. Kwa kawaida maharagwe haya hustawi kwenye udongo usiotuamisha maji, na iwe kwenye ukanda wenye baridi ya wastani.

Utunzaji

Inapendekezwa kuwasiliana na mtaalamu wa kilimo alie karibu nawe baada ya siku 14 ili kufanya ukaguzi shambani kuona kama kuna dalili zozote za wadudu pamoja na magonjwa kama vile mnyauko fuzari, endapo kuna dalili zozote shauriana na mtaalamu.

Mkulima anaweza kutumia mbolea kwa ajili ya kukuzia na kurutubisha majani kulingana na mahitaji. Ni lazima kupanda mahindi kuzunguka shamba la maharagwe ili kuzuia upepo unaoweza kuharibu maharagwe yako na yasiwe na ubora unaotakiwa.

Palizi

Ni muhimu kufanya palizi kuanzia baada ya siku kumi ili kuepusha makazi/maficho ya wadudu waharibifu. Unaweza kunyunyiza dawa ya kuzuia kutu baada ya wiki tatu.

Maharagwe machanga huchukua wiki 9-10 tangu kupanda hadi kuvuna. Hii inategemeana na hali ya hewa pamoja na mbegu. Maharagwe haya huchanua baada ya wiki sita. Wakati huu mkulima anatakiwa kuwa makini sana kutokana na uwezekano wa kuwepo wadudu waharibifu kama vile thiripi. Inapendekezwa kuwasiliana kwa karibu na mtaalamu wa kilimo ili kufanya ukaguzi ili kubaini aina ya wadudu na hatua za kuchukua.

Uvunaji

Maharagwe machanga yanafaa kuvunwa viriba vinapokuwa na urefu wa sentimita 11.5 15, unene wa milimita 6-8. Hii hufanyika katika wiki ya 9-10. Ili kupata soko zuri, pata maelekezo ya namna ya kuvuna kutoka kwa wataalamu walio karibu nawe.

Epuka maharagwe kugusana na maji au tope wakati wa kuvuna kwani inaweza kusababisha ugonjwa wa kuvunda, hivyo kupata hasara. Baada ya kuvuna weka kwenye chombo chenye matundu kwa ajili ya kupitisha hewa. Hii ni wakati wa kuvuna kutoka shambani. Baada ya hapo, maharagwe yawekwe kwenye kreti maalumu na kuwekwa sehemu yenye ubaridi kusubiria uchambuzi na kuwekwa kwenye madaraja pamoja na kufungashwa.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *