Umuhimu wa kufahamu vyanzo vya magonjwa ya mifugo

Magonjwa mengi ya mifugo husababishwa na vyanzo kutoka nje ya mwili wa mnyama mfano; mazingira machafu anayoishi mnyama, vitu vinavyopelekea vidonda (vitu vyenye ncha kali) ambavyo husababisha vidonda na baadaye vimelea vinaweza kukaa.

Pia mnyama anaweza kupata ugonjwa kutokana na hali za ndani ya mwili kama upungufu wa lishe, mfano; madini na magonjwa ya kurithi.

Wadudu waenezi wa magonjwa ni kama vile;

Vimelea(bakteria)

Mfano wa magonjwa yanayosababishwa na vimelea ni kama vile chambavu, black quarter, kimeta, kifua kikuu, brucellosis, ugonjwa wa kiwele, na ng’ombe dume kuvimba mapumbu.

Virusi (virus)

Mfano wa magonjwa yanayosababishwa na virusi ni kichaa cha mbwa (rabies), ugonjwa wa midomo na miguu (foot and mouth disease) nansotoka (rinderpest).

Protozoa

Magonjwa yanayosababishwa na protozoa ni kama ndigana baridi, ndigana kali, ndigana mkojo damu na ndigama maji moyo na nagana.

Lishe duni

Upungufu wa viinilishe katika chakula cha mifugo husababisha madhara katika mwili kama ifuatavyo;

• Husababisha majike kutopata joto mapema

• Ndama kuzaliwa na viungo visivyokomaa

• Upungufu wa uzalishaji wa maziwa

• Kiwango cha uzalishaji kushuka.

Vidonda/michubuko

Kupitia vidonda au michubuko, wadudu wasababishao magonjwa huingia mwilini mwa mnyama na kuleta madhara.

Magonjwa ya kurithi

Kama mmoja wa wazazi ana magonjwa au ugonjwa wa kurithi basi kuna uwezekano mkubwa wa mmoja wa ndama watakaozaliwa kurithi ugonjwa huo.

Utunzaji bora wa afya ya mifugo

Uogeshaji

Mifugo waogeshwe mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa yaenezwayo na kupe pamoja na ndorobo. Uogeshaji unaweza kufanyika kwa kutumia pampu za mgongoni au kwa kuwatumbukiza katika josho lililotiwa dawa ya kuogesha.

Kuwapa dawa za minyoo

Mifugo wapatiwe dawa za minyoo mara kwa mara ili kuhakikisha ukuaji wao na utoaji wa maziwa uendelee vizuri. Mifugo wapewe dawa za minyoo kila baada ya miezi mitatu.

Kuhasi

Ndama dume wasiohitajika kwa ajili ya kuzalisha baadaye, wahasiwe kwa njia ya upasuaji au kwa kutumia koleo au badizo iwapo ndama ni wakubwa.

Kuwapa ndama alama za utambulisho

Ndama wapewe namba au alama za utambulisho mara wafikiapo miezi 6 tangu kuzaliwa na utambulisho huu unaweza kuwa wa chuma au wa plastiki chenye namba kwenye sikio.

Kuondoa vishina au vichomozo vya pembe

Ndama waondolewe pembe katika mwezi wa kwanza tangu kuzaliwa kabla vishina havijakomaa na kusababisha kushindwa kutoka kwa miezi ya mbeleni. Tumia chuma cha moto kutoa vichomozo vyote vya pembe na hii husaidia ndama kukua katika mwonekano mzuri na kutokuwa na pembe zinazoweza kuumiza wenzake pindi ziwapo kubwa.

Kuondoa kwato

Kwato za ndama ziondolewe miezi mitatu ya mwanzo, ili kusaidia kupunguza kuondokana na magonjwa ambukizi ambayo husababishwa na kukatika kwa kwato zikiwa kubwa pindi awapo malishoni au akiwa katika banda lenye sakafu ya saruji.

Kwa maelezo zaidi kuhusiana na ufugaji pamoja na makala hii wasiliana na mtaalamu kutoka SUA Bw. Agustino Chengula kwa simu namba 0767 605 098.

Andika maoni mpya

Plain text

  • Hakuna vishikizo vya HTML vinavyokubaliwa
  • Anuani ya ukurasa kwenye mtandano na anwani za barua pepe hubadilika kuwa viungo moja kwa moja.
  • Mistari na aya zinajipanga zenyewe.